The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tume ya Haki za Binadamu: Baadhi ya Vituo vya Polisi Vinatumika Mahsusi Kwa Ajili ya Kutesa Watuhumiwa

Chombo cha kikatiba cha kulinda haki za binadamu Tanzania, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kimeeleza kuwa baadhi ya vituo vya Polisi Tanzania vinatumika mahsusi kwa ajili ya kutesa watuhumiwa

subscribe to our newsletter!

Dodoma.Chombo cha kikatiba cha kulinda haki za binadamu Tanzania, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kimeeleza kuwa baadhi ya vituo vya Polisi Tanzania vinatumika mahsusi kwa ajili ya kutesa watuhumiwa wakati wa mahojiano kabla ya kuwafikisha katika vituo vingine vya Polisi.

Haya yameelezwa leo Julai 19,2024, katika taarifa yake ya utendaji. Ambapo katika kipindi cha Julai 01,2023 mpaka Mei 30, 2024, Tume hiyo ilikua inashughulikia jumla ya malalamiko 1020, ambapo ilikamilisha uchunguzi wa malalamiko 230.

Katika moja ya lalamiko ambalo Tume hiyo ilipata taarifa kutoka katika vyombo vya babari ni tukio ambalo The Chanzo ilishapisha habari zake mnamo Disemba 20,2023,tukio lilomhusisha mkazi wa Dodoma, kata ya Makole na Polisi wa kituo cha kati Dodoma.

Katika tukio hilo mkazi huyo aliyefahamika wa jina la Kalamba Ramadhani Mnenge mwenye umri wa miaka 38 alielezea The Chanzo namna Polisi walivyomvua nguo na kumpiga mpaka kupoteza fahamu kwa madai kuwa alimuibia jirani yake.

“Kulikuwa kuna nyumba wakaniingiza huko ndani wakanivua nguo zote. Walivyonivua, wakanivalisha tena pingu miguuni na mikononi wakaniingiza lile chuma katikati. Yule jamaa mmoja akawa anakunywa maji huku kanivua nguo ananimwagia maji kwenye makalio. Wakanipiga sana, mpaka nikapoteza fahamu damu zikawa zinatoka puani,” alieleza Kalamba.

Katika uchunguzi wake Tume imethibitisha kutozingatiwa taratibu za kisheria wakati wa ukamataji na kumshikilia mtuhumiwa huyo ikiwa ni pamoja na kutopatiwa dhamana, kufanyiwa vitendo vya kikatili kwa kupigwa na kuteswa.

“Aidha THBUB ilibaini baadhi ya vituo vya Polisi vinatumika mahsusi kwa ajili ya kuwatesa watuhumiwa wakati wa mahojiano kabla ya kuwafikisha katika vituo vingine vya Polisi,” ilieleza taarifa hiyo ya Tume.

Pia Tume hiyo ilielezea tukio lingine huko Wilayani Mbarali, Mbeya ambapo imethibitika kuwa Polisi walimfanyia vitendo vya kikatili mfanyabiashara mmoja ambapo aliwekwa mahabusu bila ya kupewa dhamana kwa zaidi ya siku ishirini, huku akipitia mateso yaliyomsababishia majeraha mbalimbali katika mwili wake ikiwemo kupata kidonda kikubwa katika unyayo wake.

Ripoti inaeleza kuwa pamoja na madhila hayo mwananchi huyo alinyimwa haki ya kupata matibabu kwa wakati.

Katiba ya Tanzania Ibara ya 13(6)(e) inakataza watu kuteswa, “Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha,” inaeleza Katiba ya Tanzania. Hii ikimanisha matukio yote haya ni makosa ya jinai yaliyotekelezwa na Polisi.

Katika ripoti yake hiyo tume imetoa mapendekezo kadhaa, kwanza Mkuu wa Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua za kinidhamu Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi waliohusika katika vitendo ya kuwapiga na kuwatesa watuhumiwa kama ilivyobainishwa.

Pili Mkuu wa Jeshi la Polisi kuweka CCTV Camera katika vituo vya Polisi, hususan kwenye kaunta (CRO) zote za Vituo vya Polisi ili kubaini matukio yote yanayoendelea kwa mahabusu na raia wanaofika katika vituo hivyo kwa sababu mbalimbali.

Na tatu Mkuu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha Askari wanapata mafunzo ya mara kwa mara ya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ikiwemo mafunzo ya haki za binadamu na utawala bora ili kuwajengea weledi katika kutekeleza majukumu yao.

Kwa mujibu wa Ibara 129 na 130 ya Katiba, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imepewa mamlaka ya kusimamia masuala yote ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora Tanzania ikiwemo mamlaka ya kuchunguza jambo lolote linaloashiria au kuthibitisha uvunjwaji wa haki za binadamu au ukiukwaji wa misingi ya utawala bora nchini.

Kwa sasa Mwenyekiti wa Tume hiyo ni Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina Mwaimu.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *