Dar es Salaam. Wakati polisi na wanaharakati wanatofautiana kuhusiana na ukubwa wa tatizo lenyewe, matukio ya watoto kuripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha yameendelea kutawala vichwa vya habari hapa nchini, yakiwajaza wazazi na walezi hofu kubwa kuhusu usalama wa watoto wao.
Hofu hii ndiyo iliyowasukuma baadhi ya wazazi kutoka Mbande, wilayani Temeke, mkoani hapa kuivamia Shule ya Msingi ya Mbande hapo Julai 17, 2024, baada ya kuibuka kwa taarifa kwamba sare zenye damu za mtoto aliyekuwa ameripotiwa kupotea, Malick Hashim, 6, zilipatikana kwenye eneo la shule, taarifa ambazo polisi walisema hazikuwa na ukweli wowote.
Polisi wameshikilia kwamba hofu hii inachochewa na habari za uongo zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, na mpaka sasa imewashikilia watu kadhaa wanaodaiwa kujihusisha na vitendo hivyo, ikiwemo watu wanne kutoka wilayani Chalinze, mkoani Pwani, waliojirekodi video wakidai uwepo wa gari inayotembea na kuteka watoto wilyani humo.
Wakati The Chanzo imebaini kweli uwepo wa taarifa za uongo zinazochochea kukua kwa hofu hii miongoni mwa wazazi na walezi, kama vile kusambazwa kwa habari za miaka miwili nyuma, uchunguzi wake umebaini uwepo wa matukio kadhaa ya kutoweka kwa watoto katika mazingira ya kutatanisha yaliyoripotiwa tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2024.
Baadhi ya matukio hayo ni kama yafuatayo:
Machi 13, 2024: Mtoto mmoja mkazi wa Mbagala Kuu, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam ambaye jina lake halikufahamika mara moja anaripotiwa kuuwawa baada ya mtu mmoja kumrubuni yeye na mwenzake kwa kuwaambia waende naye akawanunulie chipsi kuku na nguo kwa ajili ya sikukuu.
Baada ya kufika sehemu, mtoto mmoja anasita kuendelea na safari na mwingine anaendelea naye. Baada ya siku mbili, yule aliyekwenda na mtu huyo mwili wake ulipatikana msituni akiwa amebakwa kisha kuuawa.
Aprili 10, 2024: Binti ambaye jina lake halikufahamika mara moja, mwenye umri wa miaka tisa, akiwa maeneo ya Mbagala Zakhiem, anaripotiwa kuchukuliwa na mtu asiyejulikana kisha anapatikana pembeni mwa barabara ya Kilwa akiwa amebakwa na kupoteza fahamu.
Mei 30, 2024: Asimwe Novath, mtoto mwenye umri wa miaka miwili na mwenye ualbino anatekwa na watu wasiojulikana wakati akiwa nyumbani kwao huko katika kijiji cha Bulamula, wilaya ya Muleba, mkoani Kagera. Juni 17, 2024, mwili wake unapatikana ukiwa hauna baadhi ya viongo. Juni 28, 2024, Jeshi la Polisi linawafikisha mahamani watu tisa, akiwemo baba yake mzazi Asimwe, kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.
Juni 15, 2024: Donald Kalist Mboya, mzaliwa wa Ngara, mkoani Kagera, anaripotiwa kupotea wakati akiwa anatoka Ngara kuelekea shuleni Biharamulo. Hadi kufikia Juni 29, 2024, Mboya, 14, alikuwa hajafika shuleni na haikujulikana alipo.
Julai 2, 2024: Ilham Makoye anaripotiwa kupotea na kuokotwa na mwendesha pikipiki maeneo ya Mbezi Kibanda cha Mkaa, wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Julai 5, 2024: Barack Majigeh, 13, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, anaripotiwa kupotea wakati alipokuwa akirudi nyumbani akitokea Shule ya Sekondari ya Abdu Jumbe iliyopo mtaa wa Maweni, kata ya Mji Mwema, wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Julai 5, 2024: Mtoto mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Joshua kutoka mkoani Iringa anaripotiwa kupotea baada ya kutumwa kupeleka chakula katika eneo linalojulikana kama Miyomboni mkoani humo.
Julai 7, 2024: Nusra Omari, anakutwa akiwa ameuawa katika eneo la Kibonde Maji, jijini Dar es Salaam, huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimenyofolewa.
Julai 9, 2024: Yusra Mussa, 6, mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kizuiani, wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, anakutwa akiwa ameuawa na baadhi ya viungo vyake, zikiwemo sehemu za siri, vikiwa vimechukuliwa.
Julai 15, 2024: Sumaiya Issa, mkazi wa Dodoma, anaripotiwa kupotea na mpaka sasa bado hajapatikana.
Julai 15, 2024: Angel Albert Kamugisha, 6, anaripotiwa kupotea katika mazingira ya Shule ya Msingi ya Oysterbay, alikokuwa anasoma, mara baada ya mtu aliyejitambulisha kuwa ni shangazi yake kufika katika shule hiyo na kumchukua. Baada ya taarifa hii kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, Kamugisha alipatikana akiwa hai huko Mikumi, mkoani Morogoro.
Julai 16, 2024: Brighton Amos Emmanuel, mwanafunzi wa shule ya St. Mary’s Tabata, anaripotiwa kupotea na kisha anapatikana eneo la Makumbusho Stendi, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Julai 17, 2024: Theresphoa Mwakalinga, 4, anaripotiwa kupotea mkoani Dodoma na kupatikana akiwa ameuawa na baadhi ya viungo vikiwa vimetolewa.
Je, unafahamu tukio lolote ambalo hatujaliweka kwenye orodha hii? Unaweza kuliwasilisha kwa wahariri wetu kupitia barua pepe editor@thechanzo.com.
Imeripotiwa na Ibrahim Mgaza na kuhaririwa na Lukelo Francis.
One Response
Kazii ya uhakika sanaa👍