The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Utata Kupotea Kwa Kiongozi Mwingine wa CHADEMA. Polisi Rukwa Wasema Hakuna Utekaji

Kabla ya kupotea kuna watu walifika nyumbani kwake wakimtafuta na kujitambulisha kuwa wanatoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa

subscribe to our newsletter!

Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa SACP Shadrack Masija amesema kuwa jeshi la polisi mkoani humo linachunguza tukio la kupotea kwa Dioniz Kipanya ambaye ni Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Sumbawanga  aliyetoweka toka tarehe 26 Julai 2024.

Hata hivyo kamanda huyo alikanusha taarifa za kuwa kiongozi huyo alitekwa akiwa nyumbani kwake na watu wanaodhaniwa kuwa ni askari huku akisema kuwa kiongozi huyo alitoka nyumbani kwake mara baada ya kupigiwa simu na kuiaga familia yake akidai anaenda kuonana na mtu aliyekuwa na miadi naye.

“Tumewasiliana na familia pamoja na ndugu zake ambao walikuwa naye mpaka hizo dakika mwisho ni kwamba yeye alipigiwa simu akaondoka akawaambia jamani tutaonana baadaye.Basi ndiyo hakurudi tena mpaka leo kuanzia hiyo tarehe 26 Julai lakini masuala ya kwamba katekwa sijui na jeshi la polisi hiyo yote ni uzushi tu,” alieleza SACP Shadrack Masija Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa.

“Kwa hiyo tunaendelea na uchunguzi tukishirikiana na ndugu na watu wengine wote labda niwatake tu watakaokuwa na taarifa kumhusu huyu bwana  basi watupe ili tuendelee kumtafuta,” alifafanua zaidi Masija akiongea na mwandishi wetu.

Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Gwamaka Mbughi amethibitisha kupotea kwa kada huyo wa CHADEMA ambaye amezoeleka kwa ushiriki wake kikamilifu katika kampeni mbalimbali mtandaoni hasa za hivi karibuni za kutafuta watu waliopotea au kutekwa.

“Tangu tarehe 26 mwezi uliopita alikuwa hajulikani yuko wapi na alipaswa kuwa sehemu ya watu wanaoratibu ziara ya viongozi wa mkoa wa Rukwa. Baada ya kutoonekana kwenye hiyo ziara walilazimika kufuatilia kwenye familia, kwenye familia wakajuzwa kwamba aliaga kwamba kuna mtu anaenda kuonana naye, tangu ameaga ameenda kuonana na huyo mtu hajarejea,” alieleza Mbughi.

Moja ya utata anaoueleza Mbughi ni kuwa kabla ya kupotea kwake kuna watu walifika nyumbani kwake wakimtafuta.

“Kabla ya hapo kuna watu walijatambulisha kwamba wametoka kwenye ofisi ya RPC Mkoa wa Rukwa ambao walifika nyumbani kwamba wanamtafuta. Wakaambiwa Kipanya hayupo ametoka mara moja,” anaeleza Mbughi.

Mpaka sasa simu za Kipanya hazipatikani na  familia yake na chama hakuna anayejua alipo, ambapo jambo hili limeripotiwa Polisi kwa kumbukumbu namba SUM/RB/3447/2024. Kutokana na tukio la kupotea kwa kiongozi huyo, baadhi ya watu wamekuwa wakihusisha na harakati zake ambazo amekuwa akizifanya kupitia majukwaa mbalimbali.

Boniface Jacob, Meya wa zamani wa Manispaa ya Ubungo ni mmoja wa watu waliotoa taarifa kuhusu tukio hilo, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter), Jacob ameandika kuwa Dioniz Kipanya amekuwa akipaza sauti dhidi ya Janga na uhalifu wa utekaji kila mara unapotokea akiwataka wadau na wananchi kupaza sauti juu ya tukio la kupotea kwake. 

“Tusikae kimya tutamsaliti Dionizi Kipanya, Dioniz  amekuwa akipaza sauti dhidi ya janga na uhalifu wa utekaji kila mara unapotokea. Amewahi kupaza Sauti kupitia akaunti yake ya X watu wengine wanapotekwa kama vile Kombo Mbwana Twaha, Edger Edson Mwakabela (Sativa),” Alindika Jacob.

Tukio hili linatokea ikiwa ni wiki chache toka kada mwingine na kiongozi wa CHADEMA huko mkoani Tanga, Kombo Mbwana kupotea baada ya kuchukuliwa kwa nguvu nyumbani kwake mnamo Juni 15,2024 ambapo hakufahamika alipo mpaka Julai 29,2024, ambapo Polisi walitoa taarifa kuwa walikuwa wakimshikilia kwa makosa ya kutumia laini bila usajili wa taarifa zake.

Kwa sheria za Tanzania, Polisi wanatakiwa kumpeleka mtuhumiwa Mahakamani ndani ya saa 24. Lakini pia ndugu wa mtuhumiwa wana haki ya kujua alipo ndugu yao. Mpaka sasa Kombo Mbwana ameendelea kushikiliwa na Polisi pamoja na kuwa Mahakama ilishatoa amri ya kupewa dhamana.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts