Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu ametangaza kuwa tayari amekiandikia chama chake juu ya nia ya kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake.
“Niseme tu kwamba mimi ni mtia nia rasmi wa Urais kupitia chama changu,” alieleza Lissu katika mahojiano maalum na mtandao wa Sauti ya Watanzania katika jukwaa la kimtandao la Club House jana Agosti 16,2024.
“Nikisema mtia nia rasmi nina maana kwamba nimeshatoa notisi kwa Katibu Mkuu wa chama changu kwamba nina nia ya kugombea Urais mwaka ujao, Katiba na kanuni zetu ndivyo zinavyotaka,” aliongeza zaidi Lissu.
Lissu anatangaza nia yake katika kipindi ambapo katika upande wa Chama Cha Mapinduzi tayari wanachama wameanza kuchochea vuguvugu la Rais Samia kugombea tena kwa kuchangisha fedha za kuchukua fomu na kuhamasishana huku na kule. Rais Samia alitangaza toka Septemba 2021 kuwa atagombea kwa msimu wa pili.
Mwaka 2020,Tundu Lissu alikua mgombea wa Urais kupitia CHADEMA akichuana na Hayati Rais John Magufuli. Katika uchaguzi huo ambao wengi wanauelezea kama uchaguzi uliokuwa na kasoro nyingi kupita chaguzi zote za Tanzania, Lissu alipata kura 1,933,271, huku Rais Magufuli akitangazwa mshindi kwa kura 12,516,252.
Lissu ameeleza pia kuwa atagombea katika uchaguzi wa ndani kupigania cheo chake cha Umakamu wa Mwenyekiti.
“Nimeshatoa taarifa ya kusudio la mgombea wa Urais na kusudio la kugombea nafasi yangu ya Makamu Mwenyekiti kwa mara ya pili, itakuwaje kwenye hizo nia zangu mbili vikao vya chama vitaamua kama ambavyo vimeamua miaka yote,” alifafanua zaidi Tundu Lissu.