The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

TAMISEMI Yaongeza Muda wa Kusikiliza Rufaa, Wagombea Walioenguliwa kwa Kigezo cha Udhamini wa Chama Kurejeshwa

Maelekezo haya ya Mchengerwa yanakuja ikiwa kumekuwepo na malalamiko ya vyama vya upinzani nchini vikiongozwa na CHADEMA na ACT Wazalendo.

subscribe to our newsletter!

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa  ametangaza kuongeza muda wa kamati za rufaa za wilaya wa kupokea, kusikiliza na kutoa uamuzi wa rufaa za wagombea walioenguliwa kwenye nafasi mbalimbali za uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 

Muda huo umeongezwa kutoka siku ya mwisho ambayo awali ilikuwa ni Jumatano, Novemba 13, 2024, umesongezwa mbele na mchakato huo utaendelea hadi Ijumaa, Novemba 15, 2024, saa 12 jioni. 

Katika taarifa iliyotolewa na TAMISEMI imeeleza kuwa Waziri Mchengerwa pia ameagiza kamati za rufaa kufanya mapitio ya fomu za wagombea walioenguliwa ili kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa Sheria na kanuni.

“Nazielekeza kamati za wilaya za rufani kuitisha fomu za wagombea wote walioenguliwa au hawakuteuliwa ili kufanya mapitio na kujiridhisha sababu zilizopelekea wagombea hao kutoteuliwa,” amesema Mchengerwa katika taaifa ya TAMISEMI. 

Maaelekezo haya ya Mchengerwa yanatajwa kufanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 52 ya Tangazo la Serikali Namba 571, 573, 574 na Kanuni ya 50 ya Tangazo la Serikali Namba 572 ya tarehe Julai 12, 2024 yanayompa mamlaka Waziri wa TAMISEMI kutoa maelekezo na miongozo ya uchaguzi.

Vilevile, Mchengerwa ambaye pia ni mbunge wa Rufiji kupitia CCM amewataka wasimamizi wa uchaguzi katika halmashauri zote nchini kuwarejesha kwenye mchakato wagombea wote walioenguliwa kwa sababu ya kutodhaminiwa na vyama vyao katika ngazi za kijiji au mtaa. 

SOMA ZAIDI: Uandikishaji Serikali za Mtaa: Takwimu za Kihistoria au Hamasa ya Kihistoria?

Wagombea hao ni pamoja na wale 51,423 wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, ambao walienguliwa katika mikoa mbalimbali ilihali chama hiko kilieleza kuwa kilishatoa taarifa TAMISEMI kuwa ngazi ya udhamini kwa chama chao ni uongozi wa kata.

Maelekezo haya ya Mchengerwa yanakuja ikiwa kumekuwepo na malalamiko ya vyama vya upinzani nchini vikiongozwa na CHADEMA na ACT Wazalendo kujitokeza hadharani kudai kuwa mchakato huo umegubikwa na sintofahamu kufuatia maelfu ya wagombea wa vyama hivyo kuenguliwa kwa sababu walizodai kuwa hazina mashiko. 

Lakini pia siku ya Jumanne, Novemba 12, 2024, Katibu Mkuu wa chama tawala CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, naye alitoka hadharani kuiomba TAMISEMI ipuuze makosa madogo madogo ya wagombea ili kutoa fursa kwa Watanzania wengi kushiriki uchaguzi huo. 

“Tunaziomba mamlaka zinazohusika na hasa Wizara ya Serikali za mitaa ya TAMISEMI, katika hatua ya mwisho ya rufaa kuyapuuza makosa madogo madogo ili watu wetu wengi zaidi, Watanzania wengi zaidi wapate nafasi ya kugombea. [Labda kama] kuna yale makosa makubwa sana, yale huwezi kuyakubali,” alisema Nchimbi. 

TAMISEMI imetoa wito kwa vyama vya siasa kutumia vizuri muda wa rufaa ulioongezwa kwa wagombea wake kuwasilisha malalamiko yao kwenye kamati za rufaa kama hawakukubaliana na maamuzi yaliyofanywa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi.

SOMA ZAIDI: Vijana Wenzangu, Tusiruhusu Kisingizio Chochote Kituzuie Kushiriki Kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mkuu

Tayari CHADEMA imetoa taarifa kwa umma ya kuwataka wagombea wake walioenguliwa kuendelea kukata rufaa huku kikitoa wito kwa TAMISEMI kuwachukulia hatua wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ambao wengi wao ni watendaji wa Serikali kama watabainika kufanya hujuma kwa wagombea wa vyama vya upinzani.

Chama cha ACT-Wazalendo nacho kimetoa wito kwa watendaji wa TAMISEMI kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya kuwarejesha wagombea walioenguliwa, huku wakitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya watendaji waliohusika kuengua wagombea wa upinzani kinyume cha sheria na kanuni.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajia kufanyika Novemba 27, 2024, na utahusisha vijiji 12,333, mitaa 4,269 pamoja na vitongoji 64,274. Sambamba na nafasi za wenye viti kwenye hayo maeneo, uchaguzi utahusisha pia nafasi za wagombea wa ujumbe  wa halmashauri ya vijiji na mitaa ambao ni sita katika kijiji au mtaa.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts