The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

2025: Uchumi Utaimarika, Imani Katika Siasa Itadorora Kabisa Tanzania

subscribe to our newsletter!

Mara nyingi inapofika mwisho wa mwaka wataalamu na wafuatiliaji wa sekta mbalimbali za kijamii hutoa tathmini za kuangalia mwaka unaokuja. Wengine husema ni ubashiri wa mambo, hata hivyo wengi hufanya chambuzi tu, jambo ambalo nitalifanya kwenye makala hii.

Kwa kufuatisha kanuni ya sababu na matokeo, kwamba mambo hayatokei bila kisababishi, uchambuzi wangu wa kuangalia mwaka 2025, utajikita katika kuangalia matokeo yanayowezekana kutokea kulingana na hali ya mambo kwa sasa.

Uchumi

Mwaka 2024 haukua rahisi katika sekta ya uchumi, msongo mkubwa hasa wa upatikanaji wa dola uliwalaza macho wazi watunga sera na wataalamu wa uchumi. Shilingi ilikua ikishuka kwa kasi, na dola hazikua zikipatikana, hii ilifanya hali kuwa tete juu ya gharama za madawa, mbolea, mavazi, vifaa vya viwandani, mafuta na kwa ujumla mzigo wa gharama kwa mwananchi.

Hata hivyo hali imeimarika kuanzia mwezi wa kumi, huku shilingi ikirudi kupata nguvu ya kipekee; katika Makala ya The Chanzo kuhusu dola tuliweza kuonesha sababu na uelekeo kwa nini dola haitakuwa adimu tena.

Moja ya jambo la kipekee katika suala la dola ni ‘uhuru’ ambao wataalamu wa Uchumi hasa kutoka Benki Kuu waliweza kuwa nao katika kutoa suluhu na muitikio wa kitaalamu bila siasa kuingilia kupita kiasi. Uhuru wa wataalamu wa uchumi (autonomy) hasa ya Benki Kuu ni ishara nzuri katika mawanda yetu ya Uchumi, kuthamini utalaamu hujenga imani ya kuvutia mitaji zaidi. 

Suala lingine ni uwekezaji, hasa mategemeo ya kumalizika kwa majadiliano ya mradi wa LNG, ambapo unategemewa kuwa moja ya uwekezaji mkubwa katika historia ya Tanzania. Kwa mwaka 2023, uwekezaji kutoka nje ulikua kufikia dola bilioni 1.3, hii ikimaanisha kasi imeendelea kukua, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi ndani ya miaka sita, hata hivyo bado Tanzania iko nyuma ya Uganda, DR Congo na Kenya.

Tukiangalia na hali nzuri ya hewa iliyokuwa mwaka 2024, kuimarika kwa mauzo nje, kwa ujumla ninauona uchumi wa Tanzania ukiimarika zaidi kwa mwaka 2025.

CCM 

Mwaka 2024 ulikua ni mwaka wa matukio kweli kweli, ikiwemo kutamkwa rasmi maridhiano kati ya CHADEMA na CCM kuwa yamevunjika, watekaji wanaoonekana kuwa juu ya sheria walitamba, wakifanya watu kuishi kama digidigi, na pia ulikua ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa.

Moja ya kitu ambacho nategemea kukiona katika mwaka 2025, hasa nusu ya kwanza ya mwaka, kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuwa hali ya kutoaminiana itazidi, ikichochewa na wasiwasi juu ya uchaguzi wa 2025. 

Mwingiliano kati ya dola na chama utazidi, huku kwa kiwango kikubwa nyenzo za chama zikipoteza ushawishi juu ya dola, hii italeta hali ya viongozi wa chama katika ngazi mbalimbali kuishi kwa tashwishwi, wale wajanja wanaojua kucheza na dola na chama, watakua na mkono wa juu kuamua mambo.

Kuna uwezekano mkubwa tukaona fagio likipitishwa ndani ya CCM hasa kutokana na hali ya wasiwasi juu ya mustakabali wa 2025, kwa kifupi CCM nao wajiandae na safari ya kasi yenye mabadiliko ya haraka haraka. 

Moja ya kitu ambacho naona kinaweza tokea katika nusu ya mwaka ni kuvuja kwa nyaraka mbalimbali kutoka serikalini, uzoefu unaonesha kukiwa na mkinzano wa kimaslahi kati ya CCM chama na CCM dola, umma hushirikishwa kupitia kuvuja kwa nyaraka za siri na zisizokuwa za siri, ikiwemo matumizi makubwa ya teknologia kihalali na isivyokuwa kihalali.

Uchambuzi wangu katika haya juu ya serikali na CCM unatokana na mabadiliko ya mara kwa mara yanayo onekana kufanyika serikalini na pia hali ya wasiwasi iliyo oneshwa juu chaguzi za kupitisha wagombea wa kusimama kwenye uchaguzi 2025.

Baadhi ya vyombo ambavyo vimeonesha kuwa na motisha ya hali ya juu kushiriki katika siasa ikiwemo Polisi, siwaoni wakiacha kufanya hili, ingawa na wao watapata tabu hasa za kuelewa wamsikilize yupi hasa katika ngazi za majimbo. Mategemeo juu ya kupewa bajeti zaidi na fursa zingine itazidisha hili, hii itaathiri utendaji na mahusiano yao na raia.

Watekaji

‘Jamii ya Watekaji’ ambao wanaonekana kuwa katika ‘misheni’ ya kubadili tamaduni ya Watanzania kupitia hofu, nao nawaona wakiwa na sehemu ya pekee katika kuichonga Tanzania ya 2025. Kwa mwaka 2024, kwa kiwango fulani ,watekaji wamefanikiwa kufanya sehemu kubwa ya watu kuogopa siasa, lakini pia wamedhihirisha wako juu ya sheria, tamaduni na kila kitu ambacho Watanzania tunafahamu kuwa ni Utanzania.

Shida kubwa kuhusu Watekaji, ni kuwa dalili zinaonesha  mlango walioufungua unaweza kuja na mambo ambayo yatakuwa magumu kwa kila mtu, na Mungu atusaidie wote, nitaeleza zaidi.

Jambo la kwanza ambalo tunaliona ni wameweza kufikia hofu za ndani za ujumla za jamii yetu, kufanya mtu mmoja akaogopa ni jambo moja, ila kufanikiwa kufanya watu milioni 60 wakaishi kwa hofu ni jambo la kipekee, na asili ya binadamu katika hofu kuna matatu; kukimbia, kukubali matokeo na tatu kupambana, katika mambo yote hayo ustaarabu wa kawaida haufutishwi, hisia huwekwa mbele. Watekaji wamefanikiwa kuyaleta mambo yote hayo katika jamii yetu.

Angalia: Nani Aliyewateka, Kuwapoteza Watanzania Hawa

Wakati tumeona upande mmoja Watanzania wakilia na kuhuzunika,na kubaki wamenyong’onyea, upande mwingine tumeona  jamii ikilipuka wakati mwingine kwa namna ambayo hazina msingi. Hii ni dalili kwamba kuna kipande katika jamii yetu kinaibuka cha visasi, na kujibu mapigo, na kadri watekaji wanavyojiimarisha ndivyo muitikio wa pande zote mbili unaimarika.

Hofu yangu kubwa ni kuwa kuna hatari ya jamii ya namna hii kuwa uwanda mzuri wa kupandikiza mbegu za mambo mengi ikiwemo kutoka katika makundi hatari yanayozunguka katika ukanda wetu. 

Hata hivyo, sidhani kama ni jukumu la hao watekaji kufikiria haya, labda kwa sasa wanazisafisha safisha Landcruiser zao nyeupe kwa wale wanaozitumia hizo kwa mwaka mpya wa utekaji na kufanya jamii yetu kuishi kwa udhalili. Zaidi sana, hakuna nia ya dhati wala kujali kwa wenye madaraka kukomesha vitendo hivi.

Vyama vya Upinzani

Vyama vya upinzani vina hatari kubwa ya kupoteza ushawishi wake kabisa. Nitaelezea zaidi kwa vyama viwili vikubwa yaani ACT Wazalendo na CHADEMA.

Kutokana na matarajio makubwa waliyonayo ACT Wazalendo juu ya kuvuna viti vya Ubunge kupitia siasa za Zanzibar, wataendelea kuwekeza katika kuwa na mahusiano ya dhati na Rais Samia ,hasa kutokana na kuwa Rais Samia amewahi kuonesha ana uelewa na ustahimilivu wa siasa zao.

Katika mahusiano haya,  ACT Wazalendo ina uwezekano mkubwa wa kutoa kuliko uhalisia wa hali ya siasa au kuliko inachokipata kutoka kwa mshirika wake kwenye serikali ya Zanzibar, CCM. Hii itaishia kuwasukuma wafuasi wake na wafuasi watarajiwa mbali zaidi na chama hicho, hasa kwa upande wa bara. 

CHADEMA, katika hali ya pekee chama hiki kimefikia katika kipindi ambacho kinaamini kina kinga dhidi ya watu kupoteza imani juu yake, tofauti na ilivyokuwa kwa vyama vingine vilivyoanguka. Mtifuano kati ya Mwenyekiti Freeman Mbowe na Tundu Lissu, umeleta katika umma maswali mengi juu ya udhati wa chama hiki katika sera inazozitangaza kwa Watanzania.

Kama uchaguzi unaokuja wa Januari 2025, utaonekana kutokuwa na udhati juu ya misingi ya kidemokrasia, CHADEMA inaweza ikaingia mwaka 2025, ikiwa na fedha za uchaguzi, ikiwa na wagombea wengi kuliko kipindi chochote ila ikakosa imani ya watu. Chama cha upinzani kilichokosa imani ya watu ni chama kilichokufa, na hakuna kinga dhidi ya hili, historia ya vyama inaonesha hii inaweza kumfika yeyote.

SOMA: CHADEMA Kuelekea 2025: Mivutano Hii Itaiacha Salama?

Ukichanganya matukio haya niliyoelezea na uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024, dalili zinaonesha kwamba tunaingia katika kipindi ambacho mifumo ya siasa itakosa uhalali na imani ya wananchi kwa kiasi kikubwa. Vyama vya upinzani ambavyo huonekana kuwa sehemu ya kupumua wananchi wanapokosa ahueni kutoka kwenye dola na chama tawala vinaonekana na vyenyewe viko au vinaingia katika utelezi mkali.

Sioni dalili zozote zinazo onesha kuwa serikali itaendesha uchaguzi wa mwaka 2025 tofauti na uchaguzi wa mwaka 2024, hii ikimaanisha mwaka 2025 ni mwanzo au mwisho wa utungu wa siasa zetu. Kwamba kuna uwezekano mkubwa kitu kipya ambacho hatujawahi kukijua kikazaliwa au tukawa katika siku ndefu za utungu wa siasa zilizopoteza uhalali na zisizoaminika, huku watekaji wakitamba kama nchi ni uwanja wao wa kupiga danadana.

Tony Alfred K ni mwandishi na mchambuzi anayefanya kazi na The Chanzo, anapatikana kupitia barua pepe tony@thechanzo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts