Waasi wa M23 wanaowezeshwa na Rwanda wameweza kuushika mji mkubwa wa Goma kwa mara ya pili toka mwaka 2013 walivyofurumishwa na kutoka katika mji huo. Kwa mwaka 2013, waasi hao walioushika Goma kwa mwaka mmoja, waling’olewa na kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa kilichokuwa kikiongozwa na aliyekuwa mnadhimu mkuu wa Jeshi la Tanzania, Luteni Jenerali James Aloizi Mwakibolwa.Operesheni hiyo maalum ilichukua miezi mitatu, na kuacha M23 wakikimbilia Rwanda na Uganda.
Kwa wafuatiliaji wa mgogoro huu, kukamatwa kwa Goma sio jambo la kushangaza. Kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2024, kikundi cha M23 kikisaidiwa moja kwa moja na Rwanda,kiliweza kukamata maeneo mengi kwa kasi katika eneo la Kivu Kaskazini. Kuanzia kipindi hicho, eneo aliloshika M23 likawa ni kubwa zaidi kuwahi kutokea.
Kuna mambo kadhaa yanayoonesha lengo la M23 ni kubwa zaidi ndani ya Congo. Moja, katika kujiimarisha zaidi, M23 imeanza kuungana na vikundi vingine vya wapiganaji ndani ya Congo, pili M23 ina taasisi inayofanya kazi kama chama cha siasa, yaani Congo River Alliance (AFC), taasisi hii imekuwa ikifanya kazi ya kusafisha muonekano wa kikundi hiki ili kukipa uhalali zaidi.
Tatu kwa sasa M23 imeweza kupata vyanzo vipya vya mapato makubwa, hii ni baada ya kikundi hicho kukamata eneo lenye utajiri wa madini muhimu ya Coltan, eneo la Rubaya, eneo hili linatajwa kuwa na migodi mikubwa zaidi ya Coltan duniani, madini muhimu kwa ajili ya vifaa vya kielektroniki. Kukamata eneo hili kunafanya M23 kuwa na uhakika wa mapato zaidi ya bilioni 2 kwa mwezi, M23 kukamata mji wa kibiashara wa Goma inamaanisha itapata mapato zaidi. Pia M23 imekua ikiongeza idadi ya wapiganaji katika vikosi vyake kwa kasi kubwa kwa kutumia mbinu za propaganda, siasa, na hata kutumia nguvu, na ikiwemo kutumia watoto kama sehemu ya vikosi vyake.
Hatua hizi za M23 ikiungwa mkono na Rwanda zimeendelea kuigawanya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuongeza kutoaminiana, na kwa sasa SADC pia imefikiwa na iko katika hali ya wasiwasi juu ya yajayo katika ukanda wa maziwa makuu.
SAMIDRC: Misheni imeshindwa?
Mnamo Disemba 2023, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ilituma vikosi vyake nchini Congo kwa misheni maalum iliyojulikana kama SAMIDRC, ikihusisha vikosi vya Afrika Kusini, Tanzania na Malawi.
Kutokana na hali kubadilika Congo, mnamo Januari 31, 2025, Wakuu wa nchi za SADC walikutana katika kikao cha dharura juu ya hali ya Congo, Wakuu hao wameeleza katika tamko lao kuwa vikosi vya SADC vimekuwa vikishambuliwa na Jeshi la Rwanda na M23. Hata hivyo leo February 02, 2025, Rwanda imetoa tamko la kupinga madai ya SADC, ikidai kuwa jeshi lake limekuwa likilinda mipaka yake. Wakuu hao pia wameeleza malengo ya misheni yao hayajafanikiwa, hii ikimaanisha misheni inaendelea.
Swali kubwa linalobakia ni: Baada ya mwaka mmoja wa operesheni ndani ya DRC, kwanini misheni ya SADC imeshindwa kufanikisha kile ambacho kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa ilikifanikisha ndani ya miezi mitatu mwaka 2013?
Kwa kuanza ni muhimu kuangalia muundo wa misheni ya SAMIDRC, hasa ilivyoundwa kwa ulazima wa kushikiana operesheni na Jeshi la Congo (FARDC). Takwa hili inaonekana kuwa la kimkakati hasa katika kumuhakikishia Raisi wa Congo Félix Tshisekedi juu ya dhamira ya dhati ya SADC, hasa ukizingatia kuwa tayari Rais huyo alikatishwa tamaa na kutoamini vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuvitaka viondoke nchini kwake.
Tatizo kubwa ni kuwa Jeshi la Congo lina matatizo makubwa ya kimsingi hasa juu ya wanajeshi wake wengi kuwa na pande mbili, yaani kutokuwa na uthabiti juu ya imani yao kwa Congo. Jeshi hilo liloloundwa kwa kuunganisha vikundi vya wapiganaji mbalimbali, limekuwa likikutana na matukio mengi ya usaliti, ambapo maafisa wake ikiwemo viongozi wa juu wamekuwa wakienda kwenye vikundi vya mapigano na hata kuanzisha vikundi vipya.
Kwahiyo, misheni ya SADC tayari kwa msingi wake ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha taarifa na mipango yake inakuwa salama, na taarifa wanazopokea kutoka Jeshi la Congo zinakuwa sahihi na sio za kuwapotezea muda au kuwauza. Changamoto hii ya Jeshi la Congo kutoaminina wao kwa wao ndiyo inayosababisha wapiganaji wa Congo kupewa vifaa vya mapigano kwa kupimiwa sana ili kuhakikisha wanajeshi hao hawaviuzi kwa vikundi vya wapiganaji au hawapati vishawishi vya kuanzisha vikundi vipya.
Hii shida ya kuaminiana inaweza kuelezea kwa nini Congo hawana kambi kubwa za kijeshi kwenye maeneo yenye changamoto, hasa Mashariki ya Congo, lakini inaweza kuwa sababu ya Rais wa Congo kuruhusu majeshi ya mamluki kulinda maeneo ya wawekezaji mbalimbali. Ikumbukwe pia, mwishoni mwa mwaka 2024, Rais wa Congo alibadilisha uongozi wa juu wa Jeshi la Congo, hali halisi katika uwanja wa mapambano inawezekana ilichangia hali hii.
Changamoto nyingine iliyowakumba SADC ni ushiriki wa moja kwa moja wa majeshi ya Rwanda kwenye uwanja wa mapambano. Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inaonesha takribani wanajeshi 3000 mpaka 4000 wa Rwanda wameingia ndani ya Congo toka Disemba 2023, na wanajeshi hawa wakipigana bega kwa bega na M23. Inategemewa wanajeshi zaidi wa Rwanda wanawezekana kuwa wameingia kutokana na maendeleo mapya, hasa kutokana na ukweli M23 hawana uwezo wa kudhibiti maeneo waliyoyashikilia.
Ushiriki wa wa Rwanda ulibadilisha uwanja wa vita hasa matumizi ya njia za kiteknologia za kisasa za vita na vifaa vya kisasa. Vifaa vya kukata mawasiliano ya anga (jamming and spoofing systems) vilianza kutumika, hii ikimaanisha ndege, helikopta na droni hazikuweza kutumika, jambo ambalo lilifanya hata serikali ya Congo kulalamika juu ya jambo hili, huku ikieleza kuwa ndege za abiria zinaweza kuathirika vibaya.
Pia matumizi ya mitambo ya kuzuia mashambulizi ya anga (SHORAD), kurusha mizinga ya 122mm, lakini matumizi ya makombora maalumu ya kushambulia mizinga anti-tank guided missile, pia kipekee M23 kutumia droni za kukusanya taarifa, kutumia wadunguaji, lakini kuweza kuwa na vifaa vya kufanya mapigano nyakati za giza, yote haya yalikuwa mabadiliko katika uwanja wa mapambano.
Kama alivyoeleza Jenerali mstaafu wa Jeshi la Afrika Kusini Maomela Motau, kuwa M23 kuitwa wapiganaji wa msituni ni kiini macho kutokana na vifaa wanavyotumia. M23 ya sasa ni tofauti kabisa na M23 ya mwaka 2012-2013 ambapo viongozi wake yaani Bosco Ntaganda na Kamanda wa sasa wa M23 Sultani Makenga walikuwa wakihasimiana na hata kuigawanya M23, na utofauti unao onekana sio kwa sababu ya uwezo wa kikundi hicho , bali ni kwa sababu ya ushiriki wa Rwanda.
Jeshi la Congo pia linachangamoto nyingine ya kutokubalika sana miongoni mwa watu. Kutokana na wanajeshi wake kulipwa kiduchu au kutokulipwa kabisa, wamekuwa wakitumia mbinu za kikandamizaji kupata fedha kwa wananchi na hata kutoka kwa wafanyabiashara. Lakini pia, maamuzi ya Serikali ya Congo kufanya kazi na vikundi vya wapiganaji maarufu kama Wazalendo, inafanya mambo yanakuwa magumu zaidi, hasa kutokana na ukatili na ukandamizaji wa vikundi hivi.
M23 amekua akijinasibu kama mkombozi akitumia mambo haya kama sababu, hata hivyo kukubalika kunakodaiwa na M23 ni geresha na propaganda tu, hii ndio sababu bado inabidi kutumia uongo na nguvu ili watu kwenye maeneo wanayoshikilia wajiunge na kikundi hiki. Hata hivyo, kodi ndogo wanayotoza M23 inawapa nafasi ya kipekee juu ya jeshi la Congo na Wazalendo
Ukijumlisha mambo hayo unaweza kuona ugumu wa misheni ya SADC, pia tofauti na M23 na wafadhili wao, vikosi vya SADC vinabidi kufuata sheria za kimataifa, katika mbinu na mikakati, jambo ambalo sio shida kwa M23. Hii ndio sababu vikosi vya SADC vilivyoanza kutumia mizinga mikubwa mnamo Februari 2024, Jumuiya ya Kimataifa iliweka shinikizo, hata hivyo shinikizo hili kwa upande wa M23 wanaweza kujifanya hawaoni, na walikua wakitumia mizinga hii.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wako katika hali ya mtanziko kutokana na hali ya Congo. Kwa mfano, Rwanda na Burundi wako katika hali ya kuhasimiania kila mmoja akimshutumu mwenzake kuwaunga mkono mahasimu wake ndani ya DRC. Burundi anamshutumu Rwanda kwa kushirikiana na Red Tabara vikundi vinavyotaka kuleta mabadiliko ndani ya Burundi. Lakini pia, Rwanda inaona ushiriki wa Burundi ndani ya Congo kama kusalitiwa, na pia inawaona Burundi kushirikiana na mahasimu wake CNRD-FNL, Wanarwanda waishio uhamishoni na wanaotaka mabadiliko ndani ya Rwanda kama hali mbaya zaidi ya uhasimu.
Pia, wakati Uganda na DRC wanashirikiana katika Operesheni Shujaa, operesheni maalum ya kumaliza vikundi vya Allied Democratic Forces (ADF), vikundi vinavyohatarisha usalama ndani ya Uganda na kujificha Congo, M23 wanatajwa kuwa wako huru kutoka na kuingia Uganda kama wanavyoweza, pia vikundi vya Zaïre/ADCVI ambavyo ni washirika wa M23 wanatajwa kuweka kituo chao kwa ajili ya kusafirisha wapambanaji wao katika shamba moja huko katika wilaya ya Hoima, karibu na ziwa Albert.
Kenya nayo imekua katika hali ya kutoaminika na Congo toka ambapo mkutano wa kuzindua mwamvuli wa kisiasa wa M23 ulivyofanyika jijini Nairobi mnamo Disemba 2023. Mwamvuli huo wa kisiasa unaofanya kazi kama taasisi ya kisiasa unafahamika kama Ushirika wa Mto Congo-Alliance Fleuve Congo (AFC). Mwamvuli huu ulianzishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Congo Corneille Nangaa. Wakati akizindua mwamvuli huo, Nangaa alikua amevalia suti nyeusi maridadi huku akijinasibu kuwa AFC ina nia ya kuwaunganisha Wacongo na tayari walikua na vikundi 70 chini yake.
Tokea wakati huo AFC imekuwa kama tawi rasmi la kisiasa la M23, ambapo Nangaa anaelezwa kupokea maelekezo kutoka kwa Kamanda wa M23, Sultani Makenga. Kwa sasa Nangaa amebadili muonekano wake, amefuga ndevu na anavalia kombati za kijeshi, hii ni katika juhudi za kujionesha kama mpigania uhuru wa msituni, ingawa makazi yake yanatajwa kuwa Uganda. Nangaa emeendelea kusisitiza kuwa lengo lao ni kufika Kinshasa na kuiangusha serikali ya Tshisekedi.
Mambo haya yanaonesha mgogoro huu umefikisha SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika hali ya mkwamo mkubwa. Katika hali ya kipekee ni Congo na Tanzania pekee ambao ni wanachama wa Jumuiya hizi. Tanzania ni mwanachama mwenye ushawishi katika Jumuiya zote, lakini pia Tanzania ina maslahi ya msingi ya kiuchumi na ulinzi ndani ya Congo. Hii inafanya Tanzania kuwa kwenye nafasi ya kipekee, yenye changamoto, lakini muhimu, hasa uwezekano wa kuwa msuluhishi.
Yanayoendelea Congo na nafasi ya Tanzania
Wakati tunaona Rwanda wakirushiana maneno makali ya vitisho na Afrika Kusini, Rwanda imeendelea kuwa kimya kuhusu Tanzania ambao pia wanachangia majeshi Congo, na hili linaonekana kuwa ni jambo la kimkakati. Sababu kubwa amabayo ninaiona ni mradi wa kimkakati wa SGR walionao kati ya Tanzania na Rwanda, mradi ambapo mnamo Disemba 2024, Benki ya Afrika ilisaini mkataba na Tanzania na Rwanda kuwatafutia zaidi ya Trilioni 2 kwa ajili ya mradi huu.
Jambo lingine ni ukaribu uliojengeka wakati wa Magufuli na pia jitihada na msimamo wa Tanzania kuhakikisha kuna mahusiano ya kuheshimiana kati ya Tanzania na Rwanda.
Hatahivyo, mambo yanayoendelea ndani ya Congo Tanzania haiwezi kuepuka kuyaangalia. Kwa sasa nategemea kuwa Tanzania itaongeza vikosi vyake ndani ya Congo, ikiwa kama ni jambo halijafanyika mpaka sasa. Kwa kuangalia Congo kwa darubini ya kiuchumi, Congo ndio mteja mkubwa wa kwanza wa bandari ya Tanzania katika nchi zote za maziwa makuu, hii ikifanya utulivu wa Congo kuwa wa muhimu sana kwa Tanzania kiuchumi.
Kauli za M23, pamoja na namna Corneille Nangaa anaandaliwa na kuwekwa kama Lurent Kabila wa sasa, pamoja na namna M23 inavyoongeza vikosi vyake kwa kasi na hotuba ya Januari 16, 2025 ya Kagame akiongea na wanadiplomasia, akionesha kuwa Tshisekedi hana uhalali wa kuongoza Congo kwa kusema kuwa hajachaguliwa kihalali inaonesha kuwa kuna uwezekano mkubwa tukaona jaribio la kufika Kinshasa. Hali mbaya yeyote ndani ya Congo lazima itiathiri Tanzania, hasa kwenye nyanja ya ulinzi, kutokana na uwezekano wa kuwepo wakimbizi wengi tena.
Tanzania ina nafasi kubwa ya kufanya jambo,hasa katika usuluhisi nje na ndani ya nyenzo zilizowekwa na kupitia mazungumzo ya moja kwa moja na nchi usika. Tanzania inaweza pia kuhusika kutengeneza jukwaa lisilofungamana na yeyote kwa mataifa mengine nje ya Afrika kuzungumza hasa juu ya utofautiano wa maslahi ya kiuchumi ya mataifa haya ndani ya Congo, jambo ambalo linaonekana kuathiri kabisa Congo. Tanzania inabidi pia ijiandae juu ya mazingira ya hali mbaya kama yakiitokea.
Ni muhimu kuelewa mgongano wa kimaslahi wa mataifa makubwa ndani ya Congo. Kuna ushindani na mvutano mkubwa kati ya China na mataifa ya Magahribi kuhusu madini mkakati au madini adimu, madini yanayotumika kwenye magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki na vifaa vya ulinzi.
Zaidi ya asilimia 50 ya madini yote ya Kobalti yanayopatikana duniani yapo Congo, haya ni madini muhimu kwa ajili ya magari ya umeme, ndege vita, nyambizi na vifaa vingine vya ulinzi. Kwa sasa zaidi asilimia 70 ya uzalishaji wote wa Kobalti duniani unafanyika Congo, na hii inategemewa kuongezeka. Zaidi sana asilimia 70 ya madini mengine muhimu kwa ajili ya simu na kompyuta, yaani Koltan, yanapatikana Congo.
Ripoti ya Benki ya Dunia inaonesha kuwa China kwa sasa ndio anadhibiti asilimia 85 ya mzunguko wa kobalti duniani, hii ni kutokana na China kupitia kampuni yake ya China Molybdenum kumiliki migodi mingi zaidi ndani ya Congo. Hili ni jambo ambalo mataifa ya magharibi wanataka kulirekebisha, hasa kutokana na umuhimu wa madini haya.
Hali hii ya mazingira ya mvutano wa kimaslahi wa mataifa ya magharibi inaacha maswali juu ya mgogoro huu juu na juu ya muitikio wa jumuiya ya kimataifa na kama kutakuwa na nia ya dhati ya kuhakikisha mgogoro huu unaisha.
Je Jumuiya ya Kimataifa inaona kuwepo kwa mgogoro ndio njia pekee yakufikia madini ya kimkakati hasa upande wa mashiriki ya Congo? Kama jibu la swali hili ni ndio, hatua zinazotegemewa; ni China ambayo kwa sasa ina migodi mingi ndani ya Congo itachukua hatua za kulinda mslahi yake, hasa kwa kutumia nyenzo za kifedha na kidiplomasia kushawishi mataifa rafiki katika ukanda huu kuweza kuhakikisha mslahi yake yanazingatiwa. Pia mataifa ya magharibi yatafanya vivyo hivyo, hii ikimaanisha kuwa Congo itarudishwa rasmi enzi za vita baridi. Uwepo wa mamluki ndani ya Congo inafanya mambo yanakuwa magumu zaidi ikimaanisha mambo yakiharibika, yataharibika kabisa.
Mazingira haya yanahitaji suluhisho la dhati kutoka kwa viongozi wa Afrika. Hali ya kusalitiana na kuw ana ndimi mbili lazima ikome. Je, mataifa katika ukanda wetu yanaona vita ya wazi kama njia sahihi ya kulinda maslahi yake? Kwa Rwanda inaonekana kuna mategemeo kwamba ni lazima ikiiambia Congo iruke, Congo inatakiwa iruke bila kuuliza kwa nini. Matarajio ya Rwanda kwa Congo ni kama yale ya mtumwa na bwana wake, Rwanda inaona Congo ni kama koloni lake, jambo ambalo halikubaliki.
Lakini kwa kuongeza, jambo kubwa ni udhaifu wa serikali ya Congo, udhaifu wa dola ya Congo. Congo ina jeshi lenye jina la nchi lakini linafanya kazi kama vikundi, udhaifu wa uongozi na makundi yenye ubinafsi kama M23, FDLR na vikundi vingine zaidi ya 100 vinafanya Congo kuwa janga la kuumiza kichwa. Mwisho, uchumi wa migogoro, yaani hali ambayo vijana wengi wanaamini bila migogoro hawawezi kufanya maisha, hawawezi kupata mkate inafanya Congo iwe katika mtego mkubwa.
Hali ya kutegana, ubinafsi, hali ya kujifanya kutokujua kinachoendelea na ndimi mbili miongoni mwa wafanya maamuzi,inaweza kufanya ukanda wetu kuwa uwanja wa majaribio wa silaha na vikundi mbalimbali vya mapigano. Mkutano wa pamoja kati ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki lazima utoe suluhu ya uhakika, vinginevyo siku za ukanda wetu zinaenda kuwa katika giza kali, na hali ya kutotabirika.
Tony Alfred K ni mchambuzi na mwandishi anayefanya kazi na The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tony@thechanzo.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.
5 responses
Uchambuzi mzuri. Eneo hili la maziwa makuu halitabaki salama kama baadhi ya nchi katika maeneo haya zinatumika kama wateja wa mataifa mengine. Kama ni madini, je hayawezi kupatikana bila vita? Au kuna nchi inataka kuongeza eneo lake kujumuisha eneo lenye utajiri mkubwa wa madini?
Congo ni muhimu ianze KWANZA yenyewe kuwa na jeshi linaloaminika Kwa Serikali na Wananchi wake. Kinyume na hapo Serikali ijitathmini Kwa upya Juu ya Utendaji wake na ikibidi itafute suluhu na vikundi vya waasi. Rwanda kuwasaidia waasi na Uganda kuwa Base ya vikundi vingine vya waasi, taarifa Hizo zifanyiwe kazi haraka na Muungano wa SADC na East Africa Community. Vinginevyo tuna jumuiya zisizo na maslahi halisi Kwa Wananchi wa Nchi ambazo siku zote hazina amani Kwa watu wake
Nadhani kuilaumu Rwanda kwa migogoro ambayo chanzo chake ni udhaifu wa mifumo na taasisi za kidola ndani ya DRC ni kuisaidia serikali ya DRC kukwepa wajibu wake wa kulinda haki za za binadamu na usalama raia wake yenyewe ndani ya nchi. Ni ukweli usiopingika kwamba kuna wadau wengi (wa nadani na nje ya Congo) wenye maslahi ndani ya Congo kwa sababu ya utajiri wake mwingi wa maliasili za madini, misitu na ardhi yenye rotuba.Moja ya wadau hao ni Serikali yenyewe ya Congo, ikijumuisha warasimu, watawala na wanasiasa ndani ya serikali ya Congo ambao kwa sehemu kubwa wanahudumia maslahi ya makampuni na mataifa makubwa ya dunia.
Kwahiyo, suluhu ya mgogoro huu itategemea sana utayari wa serikali ya sasa na zijazo za Congo, kujenga na kuimarisha mifumo na taasisi shirikishi za utawala wa nchi, ikiwemo ujenzi wa jeshi la wananchi wa Congo lenye sura ya kitaifa, lisilo na ubaguzi kwa misingi ya kikabila au kitabaka.
Suluhu nyingine itahitaji serikali ya Congo (na washirka wake) kushughulikia haki za uraia wa jamii ya Banyamulenge kwa kuzingatia ukweli wa kihistoria na maingiliano ya jamii husika zinazoishi Mashariki mwa Congo. Hii itahusisha serikali ya Congo na Rwanda kuzungumza bayana namna ya kumaliza tishio la RFDA na masalia ya Intarahamwe ambao walijihusisha kwenye mauwaji ya kimbali ya mwaka 1994 kule Rwanda.
M23 Leader Corneille Nanga cheered while walking around the streets captured in Goma.
Kama kweli M23 ni wavamizi iweje wakaribishwe na kushangiliwa na wananchi walipoikomboa Goma?
https://www.bing.com/videos/riverview/relatedvideo?q=M23%20welcomed%20cheered%20in%20goma&mid=8979DF22AECC0BBA30AB8979DF22AECC0BBA30AB&ajaxhist=0
M23 Leader Corneille Nanga cheered while walking around the streets captured in Goma.
https://www.bing.com/videos/riverview/relatedvideo?q=M23%20welcomed%20cheered%20in%20goma&mid=8979DF22AECC0BBA30AB8979DF22AECC0BBA30AB&ajaxhist=0