Jeshi la Polisi limeuzuia mkutano wa waandishi wa habari uliopangwa kufanyika asubuhi ya leo, Juni 17, 2025, ambapo Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche alitegemewa kuzungumza.
Polisi waliofika katika eneo la mkutano walieleza kuwa, shughuli hiyo haikutakiwa kufanyika kutokana na kuwa kuna amri ya Mahakama iliyositisha shughuli zote za chama hicho.
Brenda Rupia, ambaye ni Afisa Habari wa CHADEMA, alijaribu kuelezea kuwa mkutano huo haukuwa moja kwa moja wa shughuli za chama, jambo ambalo polisi waliofika walionekana kutoridhika nalo na kusisitiza jambo la kusitisha mkutano huo ni amri.
Shughuli za CHADEMA zimesitishwa kwa muda usiofahamika kufuatia malalamiko ya wanachama watatu wa chama hicho kutoka Zanzibar yaani; Said Issa Mohamed aliyekua Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kwa miaka 15 mpaka Januari 2025, Ahmed Rashid, aliyekuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini CHADEMA, na Maulidah Anna Komu aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini CHADEMA mpaka mapema mwaka huu.
Wanachama hao waliitaka Mahakama kusitisha shughuli zote za CHADEMA kwa kueleza kuwa kumekua hakuna mgawanyo sawa wa mali ndani ya CHADEMA, kati ya Tanganyika na Zanzibar. Pia walieleza kumekua na ubaguzi wa kidini, kijinsia na wa kimakazi; na walieleza wanachama wa CHADEMA kutoka Zanzibar wamekuwa wakibaguliwa katika fursa mbalimbali.
Katika hukumu aliyoitoa Jaji Hamidu Mwanga mnamo Juni 10, 2025, alieleza kuwa shughuli za chama hicho zinazuiwa pamoja na kuzuia chama hicho kutumia mali zake zote mpaka pale kesi ya msingi itakapoamuliwa.
“Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanazuiwa au kupigwa marufuku kuandaa, kushiriki kwenye shughuli zote za siasa mpaka uamuzi wa kesi ya msingi utakapotoka,” ilieleza hukumu ya Mahakama.
“Kwamba wajibu maombi, yaani Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), watumishi, wafanyakazi, mawakala au yeyote anayefanya kazi kwa niaba yao wanazuiwa kutumia mali na rasilimali za chama hadi pale uamuzi wa kesi ya msingi utakapotoka,” ilieleza zaidi hukumu hiyo.