The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

‘Hatuna Sehemu Nyingine ya Kwenda’: Wakazi wa Nyatwali, Bunda Walia Kuhamishwa Kwenye Eneo Lao la Asili Bila Kusikilizwa

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Sijawahi kuona tukio kama hili tangu nizaliwe, ni maneno aliyonieleza, Boazi Kikohi Maswi, mkazi wa kata ya Nyatwali, akielezea kuhusu Sakata la wao kuhamishwa kutoka katika ardhi walioyoishi vizazi na vizazi.

Pamoja na malalamiko juu ya kuhamishwa bila fidia, kilichomuacha na bumbuazi Boazi ni uhamishaji wa makaburi, bila ridhaa yao.

“Sijawahi kuona tukio kama hili tangu nizaliwe mpaka nimefika umri huu. Nimeona baba yangu anafukuliwa pale mifupa inadondoka. Jambo ambalo sikulitegemea katika maisha yangu,” anaeleza Boazi.

“Sikutegemea katika maisha yangu kwamba nitaona baba angu tena wanakimbia naye, barabarani mifupa inadondoka,” anafafanua zaidi. “Ni kitendo cha ajabu, wafu wanauzwa. Sikutegemea kwamba baba yangu amezikwa 1993, ana miaka kwenye 30 [tangu afariki], angefukuliwa.”

Haya ni baadhi ya Makaburi ambayo tayari yamefukuliwa na watu wamewahamisha wapendwa wao.

Boazi Kikohi Maswi, ni mzaliwa wa kata ya Nyatwali iliyopo iliyopo wilaya ya Bunda, mkoani Mara, eneo lililopo karibu na mpaka wa Serengeti lakini pia ni karibu na ziwa Victoria. Toka mwaka 2022, serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa kuwahamisha wakazi wa eneo la Nyatwali kupisha mpango wa Serikali kuanzisha ushoroba wa wanyama kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwenda katika eneo la kata hiyo.

Jamii hii ya wana-Nywatali wengi wao wana historia ya miaka zaidi ya 400 katika eneo hilo, kama anavyoeleza Mzee Alfred Malagila, Mzee wa miaka 80, ambaye ukoo wake wote umekuwa ukiishi katika eneo hili.

“Mama amaeolewa hapa Tamau,  baba nimemzika hapo, babu nimemzika hapo, na kizaa babu nimemzika hapo; tulikua watoto sita lakini nimebaki pekee yangu,” anaelezea Malagila.

“Nilikuwa niko hapa naumwa, sasa wakaniambia we Mzee Malagila tunafukua kaburi, sasa nikawaambia hii maiti mnapeleka wapi, nitaizika wapi? wakamaliza [kufukua], wakafukia,” anaeleza Malagila akizungumzia zoezi la kufukua makaburi lilivyofanyika.

Hakukua na Makubaliano

Mpango  wa kukuwahamisha wananchi hao unatekelezwa katika kata hiyo yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 14,250, na kwa mujibu wa sensa ya 2022 ina wakazi zaidi ya 7,000. Sehemu kubwa ya wananchi hawakukubaliana na zoezi hilo wakilalamika fidia ya Shilingi 490 kwa kilomita moja ya mraba ya ardhi, haikuwawezesha wao kuhama na kupata makazi stahiki.

Wananchi hao pia wanalalamika kuwa Serikali mkoani humo ilitumia mabavu kuwahamisha, ambapo wananchi wanaeleza kuwa walitakiwa kutia saini makubaliano ya kuondoka kwenye eneo hilo mbele ya polisi wenye silaha.

“Mimi nilikua sijawai kujua kuwa bomu la machozi linafananeje,” anasema Mahoni Musa Gidion wakati akizungumza na The Chanzo Juni 8, 2025, ndani ya kata hiyo, mtaa wa Kariakoo sehemu ambayo yeye na wenzake walikusanyika kwa ajili ya kuzungumza nasi. “Niliona askari wamevaa vitu vyeupe tumboni, nikauliza hivyo ni nini? Wakaniambia hujui hizo ni silaha.”

“Tukauliza imekuwaje wakasema mnatakiwa mpishe hili eneo. Tukauliza tena twende wapi? Wakasema hatujui mtakakokwenda, lakini mpishe hili eneo. Sasa sisi ni wakazi wa hapa na ni wakulima wa hapa na tumezoea kulima mashamba yetu hapa. Hatujawahi kuomba msaada wowote kwenye Serikali kwamba mtusaidia chakula. Tunalima mashamba yetu leo tunahama tunaenda wapi?” alihoji Gidion.

Baadhi ya nyumba ambazo tayari zimebomolewa.

Malongo Mashimo ni Diwani kata ya Nyatwali, ambapo aliiambia The Chanzo kuwa hali si shwari kwenye kata yake kutokana na na hali hiyo waliyokumbana nayo wananchi ya kulazimishwa kuondoka kwenye maeneo yao huku wakiwa wamepewa fidia ndogo na wengine hawajapewa kabisa.

“Ulioyasikia ni sahihi kabisa,” anasema Mashimo wakati akizungumza na The Chanzo kwa njia ya simu. “Tumelipwa fidia chini ya kiwango na hakukuwa na muafaka. Hakukuwa na nafasi ya mazungumzo ya maana. Mtu mwenye hekari mbili au tatu, analima mara mbili au tatu kwa mwaka kwa kumwagilia anaweza kupata milioni tano hadi sita, lakini analipwa milioni nne, ananunua wapi kiwanja?”

“Kweli wananchi walichokisema ni kweli kabisa, wameonewa. Hali siyo nzuri. Na wananchi wako pale wengine wameshindwa, walipolipwa zile fedha walienda kununua viwanja. Wengine wakakomea kununua viwanja, wengine wamejenga misingi tu, ni shida, ni shida kwa kweli,” aliongeza.

Mei 22, 2025, baadhi ya wananchi wa Nyatwali walifika jijini Dodoma kwa lengo la kuonana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, ambapo baada ya kuzungumza nao, Waziri alieleza kwamba katika kuwasikiliza kuna vipengele ambavyo wanaweza kuvifanyia kazi kwa haraka.

Waziri aliwaahidi kuwa ndani ya wiki moja kutoka siku hiyo kutakuwa na mchakato ukiendelea wa kufanyia kazi yale wananchi hao wanayahitaji ili kutafuta suluhu ya changamoto zilizopo kwenye kata hiyo.

Juni 20, 2025, The Chanzo ilimtafuta Ndejembi ili kufahamu mchakato wa kutafuta suluhu juu ya changamoto zinazoendela Nyatwali umefikia wapi, ambapo alieleza kwamba bado wanaendelea kulifanyia kazi suala hilo.

“Mei 22, 2025, nilikutana na wawakilishi wa baadhi ya wananchi wa kata ya Nyatwali waliofika ofisini kwangu na kuwasikiliza,” alisema Ndejembi kwa njia ya ujumbe mfupi. “Kwanza, walifika kuishukuru Serikali kwa kulipa jumla ya Shilingi bilioni 48.4 kwa wananchi takriban 3,800.”

“Pili, nilipokea changamoto za madai ya fidia kwa baadhi ya wananchi na niliahidi kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na mamlaka zingine za Serikali. Malipo hayo yamefanyika ili kuwezesha wananchi kupisha shughuli za uhifadhi kwenye eneo hilo la Ghuba ya Speke kama ilivyokusudiwa.”

The Chanzo ilimtafuta pia Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana, ili kufahamu kama kuna uthibitisho wa kisheria wa kuifuta kata ya Nyatwali ili kupisha uhifadhi na ni kwa nini wamekuwa wakiondoa huduma za kijamii katika eneo hilo licha ya kuwa bado idadi kubwa ya watu ipo?

Mpaka tunachapisha habari hii tulikuwa hatujapokea majibu yoyote kutoka kwake mara baada ya kutopokea simu na kutojibu ujumbe mfupi wa maandishi.

Huyu ni miongoni mwa wakazi wa Nyatwali ambao nyumba zao tayari zimebomolewa, anaishi kwenye chumba cha darasa kilichosalia.

Hakuna huduma

Tangu kuanza kwa mchakato wa kuwahamisha wananchi Nyatwali, Serikali imekuwa ikitekeleza mambo mbalimbali katika kuhakikisha wakazi wa kata hiyo wanahama. Kwa mfano, tangu mwaka 2022 zaidi ya nyumba 900 tayari zimevunjwa.

Si hivyo tu, Serikali pia imesitisha huduma za msingi za kijamii kama vile elimu na afya, hiyo ni baada ya kuvunja shule tatu za msingi zilizokuwa kwenye kata hiyo ambazo ni shule za msingi Tamau, Nyatwali na Serengeti pamoja na shule moja ya sekondari ya Nyatwali.

Kituo cha afya Nyatwali kilichopo kwenye kata hiyo kwa sasa kimesitisha huduma zake, hivyo wananchi wa kata hiyo kwa sasa wanategemea duka moja tu la dawa lililosalia kwenye eneo hilo kwa ajili ya matibabu.

Ngewa Kikohi Maswi, ni mama mjane mwenye watoto sita ambaye licha ya kuwa katika kipindi kigumu pamoja na familia yake, bado nia na matumaini yake ni kuona wanaye wanasoma katika mazingira mazuri ili wapate elimu ambayo anaamini kuwa itawakomboa.

“Kuna mtoto mwingine alikuwa anasoma kidato cha kwanza, kwa sababu ya mazingira ya shule kubomolewa hapa Nyatwali nikajaribu kutafuta shule Geita ili mtoto aingie shule nikakosa. Wakasema mfumo umejaa. Mtoto amerudi nyumbani.  Nitaokoa nini au nitavuna nini kwa huyo mtoto?” anauliza Ngewa katika hali ya masikitiko.

“Mimi mwenyewe mjane. Nitaenda wapi na hawa watoto? Mwingine yuko Mwanza, nasikia tu sijamuona,” Ngewa anaeleza. Inamaanisha hakuna mtoto katika kata hii ambaye angeweza kusoma awe mbunge, diwani, au Rais? Watoto wetu wamerudi nyuma kimasomo kabisa,” aliendelea kueleza.

Hiki ni kituo cha Afya Nyatwali ambacho kimesimamisha huduma kwa sasa na hakuna matibabu ambayo yanaendelea katika jengo hili.

Ngewa anaendela kusisitiza:  “Ningeomba Serikali itusikilize, sisi siyo wakimbizi sisi ni wazaliwa wa kata ya Nyatwali, ni wazaliwa watutendee haki. Kwenye mikoa mingine tunasikia wanatendewa haki, kwani sisi ni kondoo au ni watu gani? Sisi ni wakimbizi? Sisi ni wazaliwa kwa nini wasitutendee haki na sisi.”

Kitendo cha huduma kusitishwa kwenye kituo cha afya kilichokuwa kwenye kata hiyo kimeacha simulizi isiyosahaulika kwa Maswi, hiyo ni baada ya mwaka huu kumpoteza mtoto wake baada ya mke wake kukosa huduma wakati akijifungua.

Mke wake alijifungulia nyumbani bila ya usaidizi wa mtaalamu wa afya hali ambayo haikuwa salama, na walishindwa kumuwaisha kituo cha afya cha karibu kwa sababu kutoka kwenye kata hiyo hadi kituo cha afya cha karibu kuna umbali wa zaidi ya kilomita 25.

“Sasa hivi hatutibiwi tunategemea maduka ya raia tu yaani ya watu binafsi. Hospitali iliyoletwa na nguvu zetu sisi wenyewe haifanyi kazi,” Maswi anasimulia. 

“Sasa tunaonekana kama wanyama. Februari 4, 2025, kwa mfano mimi na mke wangu tulimpoteza mtoto wakati wa kujifungua baada ya kukosa huduma, alikosa sehemu ya kujifungulia. Hilo ndilo lilichangia mtoto kufariki.”

“Mimi najua kwamba hata kama ni vita watu au unasikia mataifa yanapigana lakini bado huduma zinapelekwa, wanaangalia wanapeleka chakula, wanapeleka misaada mbalimbali ya kibinadamu, sasa hapa ni kata ni watu wanakaa walikuwa wanaishi katika maisha yao ya kawaida sasa kwa nini uondoe huduma kama hizi,” Maswi anahoji.

Moja ya jambo ambalo halifichiki ukifika eneo la Nyatwali ni hali ya kukata tamaa, kupoteza matumaini juu ya hatma yao iliyowazunguka wakazi hawa. Wengine hawana mahali pa kulala, wengine hawana uhakika wa kula na wale ambao nyumba zao zimebomolewa basi wanafamilia wametawanyika huku na huko kutafuta malazi.

Shughuli za kilimo na biashara zimesitishwa ndani ya Nyatwali kiasi kwamba kuna wakati nilijisikia kiu nikahitaji kupata soda, mmoja wa wananchi aliniambia duka linapatikana ndani ya nyumba ya mtu kwa sababu haitakiwi kuonekana kuna duka, hivyo alichukua pesa na kwenda kuninunulia ndani ya nyumba hiyo.

Hii ni shule ya Msingi Nyatwali iliyobomolewa mwezi Januari 2025.

Mambo mawili

Kwa sasa wakazi wa Nyatwali wana mambo mawili makubwa wanayoyatazamia kutoka kwa Serikali. Jambo la kwanza ni Serikali kuwaachia ardhi yao ili waendelee na maisha na shughuli zao kama ilivyokuwa awali na jambo la pili ni Serikali kama inataka kuwatoa basi iwape eneo lingine la kwenda na iwaongezee kiwango cha fidia.

Wananchi hao wanaeleza kuwa licha ya kuwa wapo tayari kukaa kwenye meza moja ya mazungumzo na kujadiliana na Serikali ili kuweza kupata muafaka wa changamoto wanayopitia.

Hii pia ni shule ya msingi Serengeti nayo imebomolewa mwezi Januari 2025.

“Nilikua naiomba Serikali ingetuachia eneo letu, Serikali ingetuachia eneo letu. Na hususani ingetaka kutwaa hili eneo, Serikali ingetupatia hela ya kutosha ya hata ukienda unakoenda usiwe na mawazo. Lakini sasa hivi Serikali imetuua, hususani mimi imeniua.”

“Vinginevyo tumekataa kutoa hayo makaburi kwa sababu ya hayo mashamba. Hatuwezi sisi kuacha mashamba yetu tukaondoka tukaacha mashamba eti kwa ajili tunakubaliana na Serikali. Serikali kama imependa eneo ilipe watu wake vizuri ili watoke. Serikali iwalipe fidia watu kwa wakati na kwa muda mfupi,” anasema Benjamin Yacob.

Joseph Kirati ni mwandishi na mtayarishaji wa maudhui wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia barua pepe: Jkiraty14@gmail.com

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×