Dodoma. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanzisha mfumo mpya wa kuhakiki taarifa zake zinazotolewa kwa umma kwa lengo la kudhibiti na kuzuia uenezaji wa taarifa za uongo hususani katika mitandao ya kijamii.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Gabriel Makalla, Julai 21, 2025 amewataka wananchi kutumia nembo maalum ya ‘QR Code’ itakayokuwa kwenye vipeperushi vya taarifa rasmi za chama hiko kwa ajili ya kuhakiki taarifa.
“Taarifa yoyote ya uongo, ambayo watu wenye malengo ovu wanakuwa wameitengeneza kwa ajili ya kuzua tafrani na kupotosha jamii, msomaji ‘aki-scan’, hawezi kupelekwa, wala hawezi kuikuta kwenye vyanzo rasmi vya vyama, iwe tovuti au kurasa za mitandao ya kijamii,” imeeleza taarifa hiyo.
Hatua hii ya CCM inakuja kipindi ambacho hivi karibuni kumekuwa na taarifa nyingi zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambazo uongozi wa chama hiko umekuwa ukilazimika kutoka hadharani kukanusha kuwa ni taarifa za uongo na upotoshaji.
Moja ya taarifa hizo ambazo ililazimu CCM kukanusha ni kipeperushi kilichosambaa mitandaoni Juni 20, 2025 kilichokuwa na nembo za chama na kutoa taarifa kwa wananchama wa CCM kuwa mchakato wa kumpata mgombea mwingine wa Urais unatarajia kufanyika.
Taarifa hiyo ambayo ilikuja kukanushwa ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kwa kasi ikizingatiwa ilisambazwa siku moja baada ya taarifa ya CCM kusogeza mbele kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa(NEC) ambacho kilikuwa na ajenda ya uteuzi wa mchujo katika mchakato wa kupata wagombea ubunge wa majimbo na viti maalum watakaopeperusha bendera ya chama hiko kwenye uchaguzi wa Oktoba.
Taarifa ya CCM imeeleza kuwa mfumo wa ‘QR Code’ utamrahisishia mtu yeyote kujiridhisha na ukweli wa taarifa bila kupotoshwa na maudhui ya udanganyifu yanayosambazwa na watu wenye nia ovu.