Dar es Salaam. Tupo kwenye msimu wa uchaguzi, huku maandalizi mbalimbali yakiendelea kufanyika kuelekea tukio la Oktoba 29, 2025, ambapo Watanzania wenye sifa watatakiwa kuwapigia kura Rais, wabunge na madiwani.
Michakato ndani ya vyama vya siasa ya kuwapata wagombea wa nafasi hizo inaendelea, na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inategemewa kutangaza wale itakaowateua kugombea nafasi kwenye nafasi hizo.
Wateule hao wa tume, hata hivyo, mwisho wa siku watalazimika kwenda kwa wananchi kwa ajili ya kuomba kura, zoezi ambalo INEC imesema litaanza kufanyika kati ya Agosti 28 hadi Oktoba 28 kwa Tanzania Bara, kabla ya zoezi la kupiga kura lifanyike hapo Oktoba 29, 2025.
Tulitembelea eneo la Kimara, wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam kuzungumza na baadhi ya wananchi, tukiwataka watutajie changamoto zinazowakabili wao kama wananchi na maeneo yao ambayo wangetamani wagombea hawa wazijadili watakapokwenda kuwaomba kura.
Martine, ambaye ni mwajiriwa, alisema changamoto ya kwanza ambayo angependa mgombea atakayekwenda kumuomba kura anapaswa kuijadili ni ile ya barabara ya mtaa wao ambayo, licha ya kubolewa kwa ahadi ya kufanyiwa ukarabati, imeendelea kubaki bila kufanyiwa matengenezo, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wake.
SOMA ZAIDI: Kwa nini Mwaka wa Uchaguzi 2025 ni wa Kihistoria na Sababu za Hitaji la Muafaka wa Kitaifa Kabla ya Uchaguzi
“Wamekuja wamevunja, kama unavyoona, wamevunja, walivyovunja wakasema kwamba tunakuja kuweka zege, lakini toka wamevunja mpaka sasa hivi hakuna kitu kimefanyika,” alisema mwananchi huyo.
“Kwa sasa ina miezi miwili, na tangu imebomolewe hapa waliahidi kwamba wanabomoa na kuweka zege, yaani wanabomoa ndani ya wiki moja, halafu inakaa wiki, wiki inayuofuata wanapiga zege, lakini mpaka sasa hakuna zege ambayo imewekwa,” aliendelea kulalamika Martine.
Amiri Hamza anaishi mtaa wa Matangini, Kimara, na ni mfanyabiashara mdogo, anayetamani mgombea atakayekwenda kumuomba kura agusie changamoto za elimu.
“Watoto wanachukuliwa michango ya kila aina, mara leo mtihani, mara kesho mtihani,” anasema Hamza. “Kwa hiyo, sisi wazazi tunaumia sana.”
Mary Kavishe, mkazi wa King’anzi, Kimara, ambaye anasema amekwenda hapo kibiashara, amelia na changamoto ya maji.
SOMA ZAIDI: Wananchi Wachambua Usahihi Zawadi za Wagombea Kipindi cha Uchaguzi
“Unakuta wanawake tunatoka saa kumi [au] saa tisa, tumebeba mindoo tunaenda kutafuta maji, unaambiwa tuchangishe hela kuna mabomba yatakayovutwa ambayo yatakayotuletea maji hatutokuja tena kupata shida ya maji,” anasema mwanamama huyo.
“Lakini maji hakuna King’anzi, ukifika kama siku ya leo watu wengi wameweka mindoo kichwani ni maji ya chumvi,” aliongeza. “Tunauliza, hivi hapa tuko Dar es Salaam au tuko sehemu gani.”
Changamoto hii ya maji ilitajwa na watu wengi tuliozungumza nao, akiwemo Isabela Amani Mayenge, mkazi wa Michungwani, Kimara, sehemu aliyosema amekuwa akiishi kwa miaka 12 sasa na mpaka leo hawana huduma ya maji.
“Tunalazimika kuchota maji kwa majirani,” anasema Mayenge. “Ukija uongozi mwingine tutaomba utusaidie kwa upande wa maji.”
Chaula Adam Chaula anaishi King’ong’o, Njiapanda ya Goba, akijishughulisha na kazi ya kuendesha bodaboda. Kijana huyu amelia na usumbufu yeye na bodaboda wenzake wanakabiliana nao kutoka kwa wanaojiita askari jamii anaodai wameenea kila sehemu jijini.
SOMA ZAIDI: Wananchi Dar Waeleza Sifa za Mwakilishi Wanayemtaka Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
“Tukienda huko barabarani kuna nyumbu wengi sana sasa hivi wanajiita polisi jamii,” alilalamika Chaula. “Bodaboda hawana uhuru wa kufanya kazi. Wanaogopa kufanya kazi kwa sababu ya hao wanaojiita polisi jamii.”
“Wanakamata, wanamtoza mtu Shilingi 50,000, sijui shilingi ngapi,” aliongeza kijana huyo. “Wanapita hadi mitaani, wengine wanapita na mabunduki huku kwa ajili ya kukamata bodaboda. Sasa tunashindwa kuelewa kwa nini imekuwa hivi?”
Erik Jacob Sauli ni mkazi wa Kimara Mwisho anayejishughulisha na biashara ndogondogo katika ene hilo. Yeye analia na wamachinga wenzake, akisema: “Machinga wengi wanapata shida sana, umeona? Mara kuhamishwa huku na huku, kwa hiyo ni shida, tunapata shida.”
Anna Mlengo ni mkazi wa Kimara Baruti anayejishughulisha na biashara ya kuuza majiko ya umeme.
“Kwenye sekta ya elimu pia haiko vizuri,” anasema Mlengo. “Kwa sababu, shuleni watoto ni wengi darasa moja, unakuta wamekaa chini. Kwa hiyo, hali siyo nzuri.”
Veronica Ezekia ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia veronikaezekia22@gmail.com.