Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi jijini hapa wamefunguka kuhusu matamanio yao binafsi ya maisha, wakiendelea kupambana huku wakisukumwa na imani kwamba wanaweza kuzifanikisha ndoto hizo, wakitamani kuwa na wawakilishi wanaoweza kuwasaidia kwenye mchakato wao huo.
Wananchi tuliokutana nao katika baadhi ya mitaa ya wilaya ya Kinondoni jijini hapa wanafanya shughuli mbalimbali zinazowasaidia kuyaendea malengo yao hayo, wakikataa kurudishwa nyuma na changamoto lukuki zinazowasumbua kwenye maisha yao binafsi na shughuli zao za kujiingizia kipato.
Miongoni mwa wananchi tuliozungumza nao, wengi wao wana ndoto za kumiliki nyumba zao wenyewe ili waondokane na usumbufu wa kuishi kwenye nyumba za kupanga. Wengine wanatamani kukuza mitaji yao ili wapanue bishara zao. Wengine wana ndoto za kuwa na uwezo wa kusomesha watoto wao kwenye shule nzuri na kuwaandaa kwa maisha ya baadaye.
“Mimi ningepata sasa hivi angalau sehemu ya kuweza kunisaidia kufanya biashara niliyoizoea, ningeshukuru zaidi,” alisema Moh’d Abrahaman, mmoja kati ya wananchi tuliowauliza kuhusu matamanio yao ya maisha.
“Ningepata sehemu ya kuweza kufanya biashara sehemu maalumu, hapo ningeshukuru kwa sababu najua haya maisha yangu ningekuwa nayaweza, lakini sasa hivi sina kazi yoyote, nikoniko tu,” aliongeza mwananchi huyo.
SOMA ZAIDI: Wananchi Wachambua Usahihi Zawadi za Wagombea Kipindi cha Uchaguzi
Gracei Castori, mwanamama anayejishughulisha na biashara ya kuuza samaki, angetamani kukuza mtaji wake na kukuza biashara yake hiyo inayohusisha uuzaji wa samaki aina ya perege, kumba, kambale, na samaki wa maji chumvi.
“Kwa maisha yangu sasa hivi, natamani niwe na mtaji mkubwa,” anatueleza Gracei. “Kama nitapata mtaji mkubwa, au sehemu ya kwenda kukopa nipate hela niongezee mtaji, ningefurahi.”
Kwa upande wake, Mwajabu Dadi anatamani kumaliza nyumba yake ili aweze kuhamia haraka kadiri inavyowezekana.
“Mimi yaani ningemaliza nyumba yangu, ningehamia kwenye nyumba yangu, lakini sema kila ninavyojitahidi biashara inakuwa ngumu,” aliongea mama huyo.
“Kwa sababu hapa unaweza ukajitahidi, ukafanya biashara ukaja kupata, inarudi hela ya msingi na labda unapata hela tu ya kupata mia mbili ile ya kula basi,” aliongeza.
“Kwa hiyo, nyumba inazidi kukaa haijaisha, yaani biashara ningekuwa na biashara kubwa tuseme Mungu angenisaidia ningemaliza nyumba yangu tu nikahamia kwangu, basi ndiyo hivyo.”
SOMA ZAIDI: Wananchi Dar Waeleza Sifa za Mwakilishi Wanayemtaka Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
“Kwa mimi ningetamani kupata mtaji mkubwa ili nikuze biashara yangu kwa ajili ya kuwalea watoto wangu, na kumwendeleza huyo anayesoma kwa sasa,” anasema mwananchi mwingine, Maria Mburya.
Mama Jafa, mwenye watoto watano, wa kiume watatu na wa kike wawili, anasema: “Haswa ninachokitamani mimi kukipata katika maisha yangu [ni] niwe na sehemu yangu [ya kuishi], nipate sehemu yangu na mimi, siyo maisha kama ivi kupanga sijui nini, yaani ndiyo tamanio langu.”
Walipoulizwa kuhusiana na uchaguzi unaokuja wa Oktoba 29, 2025, na endapo kama wanaona uhusiano wowote uliopo kati ya matamanio yao hayo binafsi na mchakato huo wa kidemokrasia, wananchi walionekana kuona uhusiano huo, wakieleza matarajio yao kwa tukio hilo kwa hisia tofauti
“Tunataka amani, hatutaki balaa sisi,” Abrahaman alijibu alipulizwa. “Kama hivi unavyoniona mimi, niende wapi, hapa tu nitaweza kukimbia mimi? Basi hata mwenyezi Mungu anichukuwe niwe katika amani.”
“Nawashauri [wagombea] wakishapita watukumbuke na sisi wa hali ya chini, wajasiriamali wadogo wadogo,” ulikuwa ni wito wa Gracei. “Tupate mikopo hata ya bei rahisi isiyokuwa na riba nyingi ili tuweze kukopa na kulipa.”
SOMA ZAIDI: Uchaguzi Mkuu 2025: Fursa ya Kubadili Maisha ya Vijana Tanzania
Mwajabu, kwa upande wake, alionekana kuwa na mashaka kidogo na yale yanayotokea kwenye michakato hiyo.
“Hali ya uchaguzi, kwa kweli hali haieleweki kwa sababu nnavyosema haieleweki yaani, unayemtamani yule labda agombee pale siyo wanaomtaka wao, huko wanapanga wenyewe,” alisema Mwajabu kwa masikitiko.
“Nnachotamani mimi uchaguzi wa mwaka 2025, huo wa mwezi wa kumi, uwe tu uchaguzi wa uhuru na haki,” alishauri Maria.
“Wananchi tujiandae kwenda kupiga kura,” aliongeza. “Viongozi wetu wawe vizuri, kusiwe na vurugu yeyote, tuwe na amani katika nchi yetu kwa sababu nchi yetu tushazoea ni nchi ya amani.”
Vicky Kavishe and Hija Selemani ni waandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Kwa mrejesho, wanapatikana kupitia vickykavishe828@gmail.com na hijaselemani9@gmail.com, mtawalia.