Dar es Salaam. Tanzania na Zimbawe zimekubaliana kukuza uhusiano wa kiuchumi kwa kuangazia maeneo ya mbalimbali ikiwemo madini, kilimo na namna mataifa hayo mawili yanavyoweza kuwahamasisha wananchi wake kutumia fursa ya Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) pamoja na Soko Huru la Biashara la SADC ili kukuza biashara kati ya mataifa hayo.
Hayo yamejiri kwenye mazungumzo kati ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Kembo Campbell Mohadi ambaye yupo kwenye ziara ya kizazi nchini Tanzania kwa siku mbili.
Katika mazungumzo ya viongozi hao yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Jumamosi, Agosti 30, 2025, Dkt. Mpango amewakaribisha wafanyabiashara wa Zimbabwe kununua bidhaa zinazozalishwa kwa wingi nchini Tanzania ikiwemo chakula kama vile mchele na bidhaa za viwandani kama mabati na saruji.
Uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Zimbabwe zilianzisha ulianza mwaka 1980 baada ya uhuru wa Zimbabwe na mwaka 1982 nchi mbili kwa pamoja zilianzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika nyanja za ulinzi, biashara, kilimo, utalii, madini, afya, elimu, na utamaduni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Tanzania na Zimbawe pia zimekubaliana kuendeleza ushirikiano wa kihistoria ulioanza tangu wakati wa vita vya ukombozi vya wananchi wa Zimbabwe vilivyoplekea uhuru wa taifa hilo lililopo ukanda wa kusini mwa Afrika.
SOMA ZAIDI: Sasa ni Wakati wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania Kuwa ya Kijasiri Zaidi
“Tanzania na Zimbabwe zimekubaliana kuendeleza uhusiano uliopo pamoja na kutunza historia ya mataifa hayo,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika kuimarisha mshikamano na msimamo wa pamoja katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa zimekubaliana kuendeleza ushirikiano kwenye maslahi ya pamoja kimataifa ikiwemo kuendelea kupinga vikwazo vilivowekwa dhidi ya Zimbabwe.
Biashara baina ya nchi mbili imekuwa ikiongezea ambapo Tanzania imekuwa ikiuza zaidi nchini Zimbabwe kutoka Shilingi Bilioni 21.1 mwaka 2017 hadi kufikia Bilioni 115.9 kwa mwaka 2023 huku mauzo ya Zimbabwe nchini Tanzania kwa mwaka 2023 yakiwa takribani Shilingi Bilioni 25.