Mwaka 2003, Adam Shafi, moja kati ya waandishi wanaoheshima Tanzania, aliandika kitabu alichokipa jina la Haini. Baada ya Kigogo kuuwawa, ulipita msako na kamatakamata ya watu 655.
Baada ya miezi mingi ya washukiwa kukaa gerezani, kesi ilipofika mahakamani ikasemwa wazi kuwa mshukiwa mkuu ni Kubwalao aliyekuwa Dar es Salaam. Shafi amejihami kwa kukiita kisa hiki cha kubuni. Nami naogopa kuwataja ninaodhania ni watu fika katika mkasa huu.
Maana kama ilivyo kwenye riwaya hii, mtu yeyote na muda wowote anaweza kugeuzwa mhaini. Haijalishi kama unashukiwa wewe, ama kama ilivyowakuta wahusika Hamza na Edi waliosekwa ndani kwa kufahamiana tu na washukiwa wakuu.
Makomredi na uhaini
Watawala na mabwana daima wanawachukia wakomunisti. Wana hofu na mali na vyeo vyao kuchukuliwa. Kwenye kesi ya uhaini, mwendesha mashitaka wa Serikali, Bwana Chopra, anawang’ang’aniza washitakiwa kuwa wao pamoja kiongozi wao aliyekuwa Dar es Salaam (Kubwalao) walikula njama ya kumuua Kigogo.
Hofu ya watawala iko nje nje kiasi kwamba japo kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuwahusisha wakomunisti na mauaji hayo, Chopra anashupalia ukomunisti kupingana na ucha Mungu, jambo ambalo halihusiani kwa namna yoyote na kesi. Leo wanasiasa wa chama tawala wanaitana komredi na hawaamini ukomunisti!
SOMA ZAIDI: Utenzi wa Mwanakupona na Jitihada za Kumpumbaza Mume Kudumisha Ndoa
Utamtambuaje mhaini? Kwa jinsi tu watu walioshukiwa kuwa wahaini walivyokamatwa unajua tu sote tulioko uraiani tuko salama tu kwa sababu hatujakutwa na tuhuma za uhaini. Wengi waliokumbwa na kupelekwa walikuwa raia wa kawaida waliokuwa wakihangaika na shuguli za kila siku.
Wachache walikuwa ni watu wa vyombo vya usalama na wenye kuhusika moja kwa moja na mauaji ya Kigogo. Ghafla wote walijikuta wanateswa kama majasusi wa kivita walioangukia mikononi mwa maadui zao. Picha linaanza siku walipongizwa gerezani wanadhalilishwa kwa kupigwa msako wakiwa watupu.
Kisha wakapitia mateso ya kila aina ili kukubali kwamba walikula njama ya uhaini. Mwishowe mwendesha mashitaka wa Serikali Bwana Chopra aliyaita mateso hayo “kufinywa tu.”
Kwa “kufinywa tu” wanaume watu wazima wanakuwa na maisha magumu mpaka wanakaa kama watoto wanaosoma shule ya bweni na kuanza kupiga soga za maandalizi na upishi wa vyakula wakati wakisubiri kuletewa chakula chao kibovu.
Uhuru ndani ya gereza
Kabla ya kesi kuanza kusomwa, wapo waliofariki. Ila wale waliobaki walipewa mateso ya kuhakikisha wanakikaribia kifo ili tu wakubali kuwa walishiriki uhaini, ama waliwafahamu watu waliokula njama hiyo. Kama haitoshi, washukiwa walipoteseka sana waliachwa wapone kwanza na kisha zoezi lianze upya.
SOMA ZAIDI: Utendi wa Fumo Liyongo: Kama Watawala Hawataacha Kutengeneza Hila, Nasi Tuendelee Kubuni Mbinu za Ukombozi
Mateso ya mwili yaliendana na ulaghai wa nafsi. Mara kadhaa waliosuka kesi ya uhaini waliwalaghai washukiwa kwa kuwapa ubinadamu kidogo tu kama kuvaa nguo safi, kula chakula kilichopikwa vizuri, au hata kunywa soda tu ili wakumbukie uhuru waliokuwa nao nje ya gereza.
Endapo mshukiwa hakuonesha dalili za kuhadaika, alipewa mateso makali kuliko mwanzo. Juhudi hizi zilizaa matunda kwa washukiwa tisa kukubali na kutoa ushahidi wa uongo mahakamani.
Wakati wakisubiri kuanza kwa kesi watu hawa tisa walilishwa chakula kizuri na kuishi kwa staha. Baada tu ya kutoa ushahidi walikuwa wa kwanza kuhukumiwa adhabu ya kifo. Kweli kimfaacho mtu chake, lakini sio ukiwa mhaini kwani lolote laweza kutokea.
Ulipoingia mwezi wa Ramadhani washukiwa uhaini walipewa uhuru kwa kuruhusiwa kufuturu kwa pamoja badala ya kupelekewa vyakula vyumbani. Na kama ilivyo kwa mkaidi, nao siku ya Iddi walifaidi pilau. Uhuru huu mdogo wa kiutamaduni ndani ya gereza una maana gani wakati walishikiliwa kwa muda mrefu bila hata kufunguliwa kesi ili waachiwe wazipate haki zao?
Matumaini na faraja
Mwanzoni tu mhusika mkuu Hamza anapohamaki kuwa kukamatwa kwao ndio mwisho wao, Abdul anamtia moyo kwa kusema: “Humu gerezani hakuna kaburi. Utatoka tu. Kama hutatoka mzima, itatoka maiti yako. Tutatoka tu!”
SOMA ZAIDI: Inkishafi ya Sayyid Abdallah Bin Ali Bin Nasiri: Kutoka Utajiri Hadi Ufukara
Sururu yeye hakuwa na imani kuwa watatendewa haki, ama wataachiwa huyu. Hivyo, pamoja na kukamatwa alipojaribu kutoroka gerezani, aliendelea kupanga mbinu na kubadilisha mikakati ya kutoroka mpaka kesi ilipopelekwa mahakamani.
Pamoja na mateso yote, washukiwa walio wengi walikataa kusema uongo, wakiamini ukweli utakuja kujulikana. Kesi ilipofikishwa mahakamani pamoja na kwamba hawakuruhusiwa kuwa na mawakili wala kujitetea kwa njia ya maandishi, washitakiwa walibaki na matumaini kuwa mahakimu watatenda haki na kuwaachia huru.
Shafi anaonesha ni kweli mateso yanaweza kudhoofisha mwili, lakini mara nyingi hayawezi kufifisha uwezo wa binadamu kuendelea kutumaini jema litakuja, na hivyo kuendelea kupambana na hali aliyomo.
Nilianza kuwa na mashaka kuwa hapatakuwa na mazungumzo wala mawazo ya mapenzi kwani Shafi haitangulizi mada hii kwenye sura za mwanzo. Lakini inasikitisha kuona njia pekee ya Khadija aliyebaki uraiani na Hamza aliyeko mahabusu kukaribia mapenzi ni kuonana ndotoni.
Washukiwa uhaini huishi kama mahabusu. Hivyo walikuwa na tumaini na maisha. Lakini kwa wafungwa, Shafi hajaficha kwamba kwao mapenzi ya jinsia moja ni kawaida.
Fundi Shafi
Unaweza usikubaliane na msimamo wa Shafi kwamba mhaini ndiye huzusha kesi ya uhaini kwa sababu yeye ndiye mwenye jembe na yeye ndiye ameshika mpini. Atalima atakapojisikia yeye, atatupa jembe kwa nguvu anazotaka yeye. Ni kama amejipa umungu-mtu wa kuyapanga na kuyachezesha maisha ya binadamu kama wanasesere.
SOMA ZAIDI: ‘Sanaa ya Ushairi’ Inavyomdhihirisha Shaaban Robert Kama Mshairi Mbobevu
Lakini huwezi kukataa kwamba Shafi ni bingwa wa kujenga taswira. Anavyotaja aina za miti inayotengeneza samani, rangi zinazovipa vitu uhalisia na kisha akakuelezea vitu vilivyomo kwenye chumba unajiona kabisa uko mle.
Mfano mzuri ni tofauti iliyomo ofisi za gerezani ambapo watu wa vyombo vya usalama hukutana ni kama mbingu na vyumba vya wafungwa ni kama jehanam. Fundi Shafi akikuelezea nywele, uso, rangi, umbo hadi unadhifu wa mhusika ukikutana naye tena unavyozidi kusoma unamjua kama mtu uliyewahi kumuona.
Hivyo, ukilisoma tena jina lake unaingiwa na hisia kali za hasira ama huruma. Japo Haini ni riwaya, ni kama fasihi simulizi. Unaposoma ni kama vile unasikiliza tu mazungumzo. Mazungumzo hayo yamepangiliwa vyema, kila sura ikibeba kisa mahususi.
Kwa ujumla Haini ina maudhui mengi sana yanayopaswa kuchambuliwa tena na tena. Hapa nimegusia tu baadhi ya mambo hayo. Ningefurahi kuona tukijadili uhuru wa mahakama, hali duni ya uchumi, watu kupotea na wananchi kujaribu kuunga unga taarifa ili kujua mustakabali wa ndugu na jamaa zao.
Roho yangu hata sasa inasononeka kuwaza jinsi ilivyodaiwa kuwa Kubwalao ndio haswa aliyebuni na kuratibu zoezi la mauaji ya Kigogo. Kwa nionavyo mimi aliangushiwa jumba bovu.
SOMA ZAIDI: Kwaheri Amir Sudi Andanenga, Tanzania Itakukumbuka Daima
Watawala walijua fika kuwa walilitumia dola kujinufaisha wao waliogopa nguvu ya ushawishi wa ukomunisti na mrengo wa kushoto vilikuwa na uwezo wa kuwafanya watu wajenge vuguvugu la mapambano na kuwapindua.
Hivyo, kifo cha Kigogo kikawa tu ni mkasa uliotumika kumdondosha Kubwalao kwani kisa walikuwa nacho tayari. Na wewe ndugu yangu, ni kisa, ama mhusika, gani hutakaa umsahau kwenye Haini?
Diana Kamara hupenda kujitambulisha kama binti wa Adria Kokulengya. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia dianakkamara@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.