The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Hotuba Kamili ya Rais Samia Akizindua Tume ya Uchunguzi Matukio ya Oktoba 29, 2025: ‘Nina Matumaini Makubwa na Tume Hii’

Kwenye hotuba yake hii, Rais Samia anataja kazi ambazo anatarajia tume hiyo ya watu nane itafanya, akisisitiza umuhimu wa kuwa na tume ya ndani kabla ya kualika zile za nje.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam – Mnamo Novemba 20, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi Tume ya Uchunguzi yenye jukumu la kuchunguza kwa kina matukio ya Oktoba 29, 2025, ambayo yalijumuisha maandamano ya raia na matumizi makubwa ya nguvu ya vyombo vya dola kukabiliana na maandamano hayo.

Ifuatayo ni hotuba kamili Rais Samia aliyoitoa kwenye hafla iliyoandaliwa kwa ajili ya kuzindua Tumee hiyo, Ikulu ya Chamwino, Dodoma:

Uundwaji wa tume huu ni kuendana na sheria yetu, Sheria ya Tume za Uchunguzi, ya mwaka 2023, Sura ya 32, ndiyo inanipa mamlaka ya kuunda tume mbalimbali za kufanya uchunguzi kwa mambo mbalimbali ndani ya nchi yetu. 

Sasa, kwenye hili lililotokea, nikaona kabla ya kuletewa tume za nje, tuwe na tume yetu wenyewe ndani, ifanye kazi, na za nje zikija zitakuja kuzungumza na tume mwenzao ambayo tayari walishaanza hiyo kazi.

Kwa ufupi, kilichotokea hakikutarajiwa kitokee ndani ya nchi yetu kwa sababu ya historia tuliyo nayo ya usalama na utulivu wa kisiasa ndani ya nchi. Hata kama kuna vipindi ambapo hatukuwa na usalama wa kisiasa [kama nchi], [hali] haikuwahi kufikia kiasi hiki kilichofikia. 

SOMA ZAIDI: Tume Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29, 2025: Serikali Iepuke Vishawishi vya Kutaka Kujistiri na Badala Yake Ijikite Kwenye Kuliponya Taifa 

Kwa hiyo, tume hii itakakabidhiwa makabrasha ya kufanyia kazi, watakabidhiwa na hadidu za rejea za kwenda kuziangalia wakati wanafanya kazi yao. Lakini, kwa ufupi, labda mimi niseme yafuatayo. 

Kwanza, nadhani tume tunaitarajia ikatuangalizie sababu hasa iliyoleta kadhia ile, sababu hasa ni nini, kiini cha tatizo ni nini? 

Lakini, jambo lile lilipotokea, vijana waliingizwa barabarani kudai haki, tunataka kujua, haki gani ambazo vijana hawa wamezikosa, na kwa umoja wao waliingia barabarani kuidai haki hiyo. Lengo la wale vijana kuingia barabarani [ni nini], ni haki gani wanadai ili tuweze kuifanyia kazi na wapate haki yao. 

Lakini jingine, tunapofanya hii kazi hebu twende tukaangalie matamshi ya vyama vya upinzani, wale waliokuwa wakisema “Lazima kiwake,” “Hapakaliki,” “Lazima aondoke,” “Lazima kiwe hiki,” “Uchaguzi hautafanyika.” Kitu gani hasa kilichowapelekea kufanya vile? 

Lakini katika kufanya hivyo, tuangalie uhusiano wa hicho chama na tume yetu ya uchaguzi. Uhusiano wao ulikuwaje katika kipindi hicho mpaka ikawapelekea waseme maneno yale?

SOMA ZAIDI: Oktoba 29, 2025: Tulichoka Hekima na Busara, Tukajaribu Ujinga, Tumeona Matunda Yake 

Lakini jingine, tuangalie mchango, ukiacha vyama vya siasa vilivyoingia kwenye huo mgogoro, NGOs zetu, za ndani na za nje. Tunaambiwa kwamba vijana wale walioingia barabarani kudai haki walilipwa fedha kwanza ndiyo wakaingia barabarani, na wengi wao waliingia barabarani kuendana na hizo fedha walizopewa.

Je, fedha zilitoka wapi, zilitoka wapi? Kwa hiyo, haya tukayaangalie. NGOs za ndani na za nje, wamechangia nini kwenye mambo haya? 

Lakini niseme, hata kama kulikuwa na changamoto baina ya Tume [Huru ya Taifa ya Uchaguzi] na vyama vya siasa, Msajili [wa Vyama vya Siasa] na vyama vya siasa, Serikali na vyama vya siasa, je, hakukua na njia nyingine nzuri zaidi, njia ilikuwa ni ile moja peke yake, ya kuingia [barabarani], kuchoma nchi, kuchafua nchi, kusababisha vifo kwa wananchi? Hakukua na njia nyingine ya kurekebisha hizo kasoro? Hebu twendeni tukaangalie pia.

Lakini, tukaangalie sasa, jambo limetokea, watu wameingia barabarani, vurugu zile, na kilichokuwa kinaimbwa ni kwamba kama kilivyokuwa Madagascar, itakuwa hapa pia. 

Sasa, tukaangalie njia zilizochukuliwa kukabiliana na lile vurugu, na zenyewe, na ndiyo maana hapa ndani kuna mstaafu jeshi, mstaafu polisi, mstaafu mwingine, kwa hiyo twendeni tukaangalieni njia zilizochukuliwa zilikuwaje.

SOMA ZAIDI: Tanzania Baada ya Oktoba 29, 2025: Tunarejeshaje Kisiwa cha Amani?

Halafu, katika kuifanya kazi hii, pamoja na hadidu rejea nyingine ambazo mtapewa, mimi nimetoa tu vile vidokezo hapa, lakini katika kuifanya kazi hii tutapangiana muda. Lakini kama alivyosema CS [Katibu Mkuu Kiongozi] kwamba yuko tayari kuiwezesha tume kwa vitendea kazi na muda, mtakapokaa naye atawaleza vyema.

Tutawapa pia sekretarieti ambayo itakuwa inawasaidia kuandika, na mambo mengine yote ya oganaizesheni ambayo yatakuwa yanatakiwa kufanywa ili tume ifanye kazi yake vizuri. 

Kama mnavyojua, wakati nafungua Bunge, niliahidi -, wakati nazindua kampeni – niliahidi kwamba ndani ya siku 100 nitaunda Tume ya Maridhiano tuangalie sababu za changamoto za kisiasa ndani ya nchi yetu, tupatane, na tuende vizuri.

Lakini, kwa hili lililotokea, tumeona tuunde tume hii kwanza, ifanye kazi yake, imalize, mapendekezo yatakayotoka huku ndiyo tutakayokwenda kuyafanyia kazi kwenye tume ile ya maridhiano. Kwa hiyo, mapendekezo yenu ndiyo yatafanya agenda za kwenye Tume ya Maridhiano.

Kama nilivyosema, kazi hii siyo ndogo, tutaanza na muda nadhani wa miezi mitatu, halafu tutaangalia kazi inavyokwenda. Lakini niseme kwamba nina matumaini makubwa na tume hii. 

SOMA ZAIDI: Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Wahimiza Uwajibikaji Juu ya Mauaji ya Oktoba 29

Jana [Novemba 19, 2025] nilikuwa nasoma makala fulani, [nikaona] wenzetu wapinzani wanasema hawana imani na tume yoyote ya ndani, wanataka tume itoke [Umoja wa Mataifa] UN, tume itoke [Umoja wa Afrika] AU, tume itoke Umoja wa Ulaya [EU], ndiyo zije zifanye kazi hapa kwetu Tanzania.

Lakini mimi nina imani sana, kwa ubobezi na uzoefu wenu, nina imani sana na tume hii, na ni matumaini yangu [kwamba] mapendekezo [yenu] yatatutoa [hapa tulipo], tusogee mbele. 

Sasa, baada ya kusema hayo, niseme tu kwamba tume hii nimeizindua rasmi, na nawatakia kazi njema.

Asanteni sana!

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×