Imewahi kukutokea unasoma kitabu na hutaki kukiweka chini? Nakutahadharisha ukianza kumsoma Kamange hutatamani hata kuitwa. Anajua kusuka maneno mpaka unajikuta ukidunda naye na kitabu kikisogea.
Usiseme naongopa, msome mwenyewe kwenye Kale ya Washairi wa Pemba. Kitabu hiki ni mashairi ya Kamange na Sarahani yaliyokusanywa na Abdurrahman Saggaf Alawy na Ali Abdalla El-Maawy; na kuhaririwa na Abdilatif Abdalla.
Ali bin Said bin Rashid Jahadhmiy, almaarufu Kamange, ni mshairi wa Pemba aliyeishi kati ya miaka ya 1830-1910. Alitoka kwenye familia yenye kumiliki mashamba ya minazi na mikarafuu.
Hivyo, walikuwa na uwezo wa kumsomesha Qur’an na dini. Athari hii aliyoipata katika elimu inajidhirisha kwenye ushairi wake wakati anatumia moja kwa moja maneno ya Kiarabu ama vifungu vya Qur’an. Hii haimaanishi aliandika tu kuhusu nasaha za kidini, alikuwa mshiriki wa siasa na maisha ya kila siku ya watu wa Pemba.
Kamange ni fundi haswa kiasi kwamba kila ubeti unaousoma unatamani kuuchukua na kuutumia mahali. Kama sio kumuandikia mpenzi, basi kumtania mtu. Ni mtu mwenye hisia na misimamo mikali.
SOMA ZAIDI: Funzo Kutoka Riwaya ya ‘Haini’ ya Adam Shafi: Mtu Yeyote, na Muda Wowote, Anaweza Kugeuzwa Mhaini
Akifurahia nawe msomaji utafurahi. Kwa mfano, anapoandika mashairi ya kumsifu mwanamke unajua tu anampenda sana maana anamsifu kila kitu kuanzia sura, umbo hadi tabia. Rejea mashairi ya Muwacheni Anighuri na Uhai wa Swifridi. Unaweza kuhisi mashairi haya wameandikiwa wanawake malaika.
Lakini Kamange akichukia utatamani ukae naye mbali. Na siku moja nyumba yake ilianguka. Nduyu yake akaahidi kuja kuitengeneza bila kutokea. Kamange akamtwanga shairi:
“Hukuweza kata puwa, wajihi kuunga,
Wajizuzuwazuzuwa, juso govi kimalenga,
Hali yangu waijua, siri ya ndani ni kunga,
Mwenyewe ‘tafungafunga, nipate hema nilale.” (Uk 36)
Japo alikuwa mtu wa tabaka la waliohodhi ardhi, hakuacha kuandika mashairi ya kupinga dola kutumia mabavu. Palikuwa na askari aliyekuwa mkatili, hivyo Kamange akaandika shairi Mashumu Yangu, akimuombea mwisho mbaya.
Utamaduni wa majibizano
Sehemu ya umaarufu wa Kamange inatokana na kuwepo kwa utamaduni wa majibizano ya ushairi. Japo kuna wakati alishiriki na washairi wengine, jambo la wazi ni kuwa katika jadi hiyo Kamange mtani wake wa jadi ni Sarahani. Walijibizana kwa namna mbili. Namna ya kwanza ni pale mmoja wao anapopatwa na kisa halafu hadithi ile ikamfikia mwenzie.
SOMA ZAIDI: Utenzi wa Mwanakupona na Jitihada za Kumpumbaza Mume Kudumisha Ndoa
Inasemekana Sarahani alifunga ndoa ya siri. Siku moja usiku alipokaribia kwa mkewe huyo walitokea watu ambao Saharani aliwakimbia ili wasimuone. Kamange akaandika shairi Ulipita ‘shi na Yombe kumtania.
Aina ya pili ya majibizano ilikuwa ni pale wanapoandikiana ubeti baada ya ubeti. Kwenye shairi la Mitambuuni Si Shamba, Kamange alikuwa akimnanga Sarahani kwamba mahali anapoishi sio pazuri atafute pengine. Saharahi naye anakomaa kuutetea uzuri wa Mitambuuni.
Japo walionekana kama mahasimu, Kamange na Sarahani waliheshimiana sana. Inavyoonekana kuna watu hawakuamini kwamba majibizano yale hayana chuki ndani yake. Ndio maana Kamange alipofariki Sarahani aliandika mashairi ya kilio, akithibitisha urafiki wao. Katika shairi la Naliya Leo Sinaye, Sarahani anasema:
“Katwa hatukugombana, mwinzangu ni radhi naye,
Dhihaka tukibishana, pasi na achukiwaye,
Ametuwachiya umba, mwenye kheri aonaye,
Naliya leo sinaye, yaa mawadda na swafawa!”
Lakini wapo washairi waliojua ukweli wa ukaribu wao. Saharani alipoanza kukubaliana na hali ya kifo cha Kamange, kama vile kuvunja tanga, aliandika Kadhwa Haina Mganga. Yaani kifo hakiepukiki. Ruweihy alimjibu kwa shairi la Haachi Huzunika, Mtu Kwa Mpenzi Wake.
Mahusiano ya mume na mke
Pamoja na ushabiki na visa vya kisiasa, Kamange, kama alivyofanya Mwanakupona kabla yake, anatuelezea kuhusu mahusiano ya mume na mke. Mshairi aliyekuwa maarufu kwa jina la Paka Shume anamuomba ushauri Kamange juu ya mwanamke gani ni sahihi kuwa naye kwenye shairi la Wamuhajiri au Wakhatimu Naye?
SOMA ZAIDI: Utendi wa Fumo Liyongo: Kama Watawala Hawataacha Kutengeneza Hila, Nasi Tuendelee Kubuni Mbinu za Ukombozi
Shairi hili laweza kuleta mjadala mpana kwa wanaoamini na wasioamini ufeminia. Paka Shume anataja wanawake wa kila hali, ikiwemo kama inafaa kuwa na mwanamke tajiri, kuoa mitara na hata kuoa mke wa mtu. Kwa kila hali, Kamange anampa jibu.
Suala la mwili na hali za mwanamke kuchambuliwa na wanaume ni sawa ama si sawa? Na vipi kama washairi hawakuwa haswa na kiu ya kujua kuhusu mwanamke yupi afaa bali walikuwa wanajinoa tu kisanii? Haya ndio maswali makuu mawili niliyojiuliza. Natumaini atakayesoma kitabu hiki naye atapata maswali zaidi na kuendeleza mjadala juu ya matumizi ya wanawake kwenye ushairi huu.
Lugha iliyotumika kwenye mashairi sio ngumu kiasi cha msomaji kugugumia. Pia, mhariri amefanya kazi nzuri ya kuweka msamiati mwanzo wa kila shairi na maelezo yake mwisho wa ukurasa ili msomaji asipate taabu ya kufunua kurasa mbele na nyuma.
Kitabu hiki kinatuonesha uzuri na ukuu wa Kiswahili kwa sababu ya wingi wa lahaja zilizotumika kwenye kitabu. Kamange mwenyewe alikuwa Pemba karne ya 19 na mwanzo wa karne ya ishirini. Mhariri na wakusanyaji wa mashairi wakiwa wazaliwa wa Mombasa karne ya ishirini. Na msomaji unakuja ukiwa na lahaja na athari za lugha mbalimbali, kama lugha mama na Kiingereza.
Lakini sote tunajumuika bila kujali umbali wa wakati na mahali kufurahia ushairi. Labda wakati umefika kwa sisi Waswahili kutia nia ya dhati ya kukipenda na kukilinda Kiswahili kama Kamange akisiavyo kwa Swifridi:
“Dhamiri na niya yangu, numfuge kwa juhudi,
Nizivunje njia zangu, nituwe nikifaidi,
Mihongere ndege wangu, peke yake asizidi,
Uhai wa swifridi, sipendi ndege mwingine.”
Diana Kamara hupenda kujitambulisha kama binti wa Adria Kokulengya. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia dianakkamara@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.