The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Sarahani bin Mantwar: Bingwa kati ya Mafanani Afrika Mashariki

Aliingia kwenye sanaa ya ushairi kwanza kwa kuhifadhi Qur’an na kisha kusoma Kiarabu, fasihi za kiarabu na fani nyingine za dini ya Kiislamu.

subscribe to our newsletter!

Naweka maslahi yangu wazi: napenda sana ushairi wa Sarahani. Katika lugha ya ushairi usio wa karne hii anaongea kitu unahisi kabisa unakisikia kwenye mwili wako. 

Akiuelezea ukoloni unaanza kuogopa kama vile unawaona askari wakipiga doria. Bwana huyu anakuteka kwa mashairi unapotelea Pemba. Ndio maana Sarahani bin Mantwar ni kati wa washairi maarufu pwani ya Afrika Mashariki. 

Sarahani aliishi kati ya mwaka 1841-1926 huko Pemba. Aliingia kwenye sanaa ya ushairi kwanza kwa kuhifadhi Qur’an na kisha kusoma Kiarabu, fasihi za kiarabu na fani nyingine za dini ya Kiislamu. 

Unapomtaja Sarahani huwezi kumuacha Kamange maana ndio hasa nusu ya umaarufu wake kwa uhasimu wao wa kishairi. Mashairi ya Sarahani yamechapishwa pamoja na hasimu wake Kamange kwenye Kale Ya Washairi wa Pemba

Ushairi wa Sarahani kwa ujumla unamuonesha kuwa mtu mwenye utulivu na kujaribu kutumia fikra kuliko anapolikabili jambo. Anapoandika kuhusu mabavu ya serikali ya kikoloni ni mchango wake katika mapambano lakini hawi na tabia za kumfanya ajikute mikononi mwa serikali. 

SOMA ZAIDI: ‘Kale ya Washairi wa Pemba’ na Ufundi wa Mshairi Mahiri Kamange

Ndio maana kweye shairi la Lizamu na Darizeni anamuonya Kamange ambaye alikamatwa na kutiwa korokoroni wakati mmoja kwa kutembea usiku. Na hata kwa jamii nzima ni mtu mwenye kuonya dhidi ya maovu yanayotendwa bila kificho kama uzinzi kwenye shairi la Nini Kufanyiwa Shindi na kughushi nasaba Muwongo wa Uwongoni

Kwa jinsi Sarahani anavyotumia maneno ya dini katika mapambano dhidhi ya mkoloni ni tofauti kubwa wa harakati za ukombozi za karne ya 19 na ya 20, hasa baada ya Uhuru. Sarahani anatumia mawaidha ya dini ya kiislam na vifungu vya Qur’an kwenye shairi la Rabbi Ondowa Nakama. Ameandika shairi zima kwa kufuata mpangilio wa alfabeti ya kiarabu. 

Shairi hili linawataja kwa majina maafisa wa serikali ya kikoloni, vitendo vya uonevu kama kupora mashamba na hali ya kujengewa uoga kwani ungeweza kukamatwa muda wowote. Lakini katika yote anamuomba Mungu awaondolee hii kadhia ya kutawaliwa. Baada ya Uhuru, kwa sababu nisizozifahamu kwa hakika, mashairi mengi yamekuwa ya kitaifa ili kukwepa udini na ukabila.  

Mtandao wa Waswahili

Kadiri ya masimulizi ya waliokusanya mashairi haya, Sarahani alikuwa ni sehemu ya mtandao wa Waswahili wenye kujenga utamaduni wao. Alikuwa akiwatembelea wanazuoni, mshehe na washairi wa miji ya Pwani mzima ya Afrika Mashariki. Na aliendeleza mahusiano nao mpaka mwisho wa maisha yake. 

Tunaona kuwa Waswahili japo walikuwa katika hali ngumu ya kutawaliwa na Waomani na Waingereza waliendeleza jadi zao za kidini na kisanii. Ilipokuja kwenye utamaduni hakukuwa na vikwazo vya dola, changamoto za lahaja wala umbali mrefu waliopaswa kusafiri. 

SOMA ZAIDI: Funzo Kutoka Riwaya ya ‘Haini’ ya Adam Shafi: Mtu Yeyote, na Muda Wowote, Anaweza Kugeuzwa Mhaini 

Nisiwasemee wenzangu mimi ni mshairi ambaye hata sijawahi kujisajili UKUTA. Sijawahi hata kufika Mombasa wala kuizulu yema Tanga. Sasa hata nikisema niende Pemba, naenda kwa nani ambaye ni mshairi? Maisha ya Sarahani ni mfano mzuri wa ukitaka kwenda haraka, nenda peke yako. Ukitaka kwenda mbali nenda na mwenzako. 

Hata bila kujadili wanawake katika ushahiri wa Sarahani tunajua bado ni watu muhimu katika ufanikisha kazi yake. Kadiri ya masimulizi baba yake Sarahani alifariki na kumuacha akiwa na mwama mmoja tu. Mama yake Sarahani aliyeitwa Bi. Aiye Binti Jadi bin Nasir Ruqeishy ndiye aliyefanya Sarahani awe hafidhi. 

Hakuishia hapo. Alimpeleka kusoma taaluma za kiislamu hapo hapo Pemba na baadaye Unguja. Sarahani alikuwa na wake watatu, wangemvuruga sidhani kama tungepata mashairi haya leo.

Nadhani wanawake wa kipindi hiki walifaidi. Fikiria mpenzi wake si mshairi, lakini anampelekea beti la shairi la Sarahani Mlangilangi na Mkadi:

Yashinda yote mauwa, unabakiya pekee,

Miafu nimeing’owa, sipendi kwangu ikaye, 

Bure kuweka matuwa, mara hwisha harufuye, 

Mlangilangi rihiye, unafadhili mauwa.

Kama shairi hili hapo juu Sarahani ameandika mashairi mengine ya mapenzi. Kwa ujumla, yeye ni mtu anayemini mapenzi ni maridhiano kushinda chochote. Wapendanao wakiweka utayari wa kuwa pamoja basi uzuri wa sura, umaarufu ama wingi wa mali havitawatenga na watafurahia kuwa pamoja. Rejea shairi la Itifaki ni Aula

Mjadala

Sijui kama ni jambo la kutatiza ama ni suala la kuzua mjadala. Mwanamke anayempenda kwa macho Sarahani ni mwenye asili ya weupe na nywele za singa. 

SOMA ZAIDI: Utenzi wa Mwanakupona na Jitihada za Kumpumbaza Mume Kudumisha Ndoa

Niruhusu Twaliyani ameandikiwa mwanamke mwenye rangi ya pera yaani mweupe. Baada ya kumuoa mke wa tatu Mwana Aisha Sarahani aliandika hivi kuhusu nywele zake 

Nywele zimelala singa, zimependeza nyeusi, 

Kwa mafuta huzifunga, zimewashinda wasusi, 

Muwili ameviringa, hasha hakutayabasi, 

Anitosha yeye basi, sitaki mwingine tena.

Ikiwa leo wanawake bado tunahangaika kutafuta namna ya kurefusha na kulainisha nywele, na kuongeza weupe, je ni macho ya wanaume kama Sarahani ndio yanaendelea kutuponza? Au nisitahayari kwa sababu Sarahani anaishi kwenye jamii yenye na mchanganyiko wa rangi?

Kwa jinsi Sarahani alivyoomboleza kwa kifo cha Kamange watu walijua dhahiri wawili hawa walipendana. Sarahani aliandika mashairi ya kumlilia Kamange. Hata baada ya mashabiki wa pande zote mbili kuendeleza ushindani baina yao, Sarahani hakujihusisha na ushairi huo kwa heshima ya mtani wake. 

Kuna shairi limenikumbusha watu wanaopenda kujisifu kwa kuweza kukaa macho wakistarehe usiku kucha. Wenyewe hujiita popo, na kukesha hukuita amsha popo. Sarahani ana ujumbe wenu:

Wendao ni maluuni, taweleza kwa majina,

Mchawi na shaitwani, mwivi na swahibu zina, 

Na wao hawakutani, daima hukimbiana,

Sasa takwenda mchana, naapa usiku siendi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×