Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia mashtaka watuhumiwa watatu waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuchoma ofisi za CCM huko Kivule Majohe.
Watuhumiwa hao ni Mohamed Madea(28), Fredy Chacha(21) na Peter Basoti Chobe (48).Akizungumza juu ya shauri hilo, Wakili wa watatu hao, Wakili William Maduhu ameeleza kuwa Ofisi ya Mashtaka ilishindwa kuthibitisha madai hayo.
Watuhumiwa hao watatu wamerudi mahabusu kwa kuwa bado wana shauri lingine la uhaini. Wakili William Maduhu ametoa wito kwa Mwendesha Mashtaka kuliondoa shitaka hilo.
“Ni wito wangu ndugu DPP uyaondoe mashtaka hayo ya uhaini kwa sababu kama umeshindwa mashtaka ya uchomaji sina hakika na sina imani kwamba unaweza ukathibitisha mashtaka ya uhaini,” alieleza Wakili Maduhu.
Familia za washtakiwa pia zimetoa wito kwa Mwendesha Mashtaka kuondoa mashtaka yaliyobaki ya uhaini.
“Imeonekana kwamba watoto wetu hawana hatia, kwa kweli tumetaabika sana,” Sheila Mohamed, mzazi wa mmoja wa watuhumiwa anaeleza.