Inafikirisha unapokuta mtoto anakosa heshima kwa dada anayemlea na kukaa naye nyumbani pale wazazi wanapokuwa kazini. Na mara nyingine mzazi anaona ni sawa tu na wala hamkemei mtoto wake kwa tabia hizo.
Unakuta mtoto anamuona dada wa kazi kama mtu asiye na thamani na wa kudharaulika tu.
Akiamka asubuhi wala hamsalimii, anatupatupa vitu ovyo, akijua kuna mtu wa kuviokota. Akila anaacha vyombo hapohapo mezani na kumuamuru dada wa kazi avitoe na anaongea naye kwa lugha ya dharau.
Yaani mtoto mdogo anaweza kumgombeza dada wa kazi kama wamelingana vile, hali ambayo si sawa.
Mtoto akiachiwa kuendelea kuonyesha dharau kwa msichana wa kazi ambaye anakaa naye kila siku na kumlea, atajenga tabia ya ukorofi na kudharau mtu yeyote anayehisi yuko chini yake.
SOMA ZAIDI: Je, Unamshirikisha Mtoto Wako Katika Kufanya Maamuzi ya Kifamilia?
Hii itampelekea kuwa na mahusiano mabaya kuanzia shuleni, kazini hadi kwenye familia yake huko mbeleni. Ni vizuri mtoto tangu akiwa na umri mdogo afahamu kuwa watu wote ni sawa na hakuna mtu bora zaidi ya mwingine.
Jinsi mtoto anavyoishi na dada wa kazi inategemea kwa kiasi kikubwa na mfano anaoupata kutoka kwa mzazi wake. Je, unawapa dada wa kazi heshima stahiki? Unawapa ujira wao vyema? Unakumbuka kuwanunulia nguo? Anapata muda wa kupumzika? Akiugua unajali?
Kama hufanyi hivi vitu vyote usitegemee mtoto wako kufanya vinginevyo. Mara nyingi familia ambazo huishi na dada wa kazi kama mmoja wa familia huwa na watoto wanaoonyesha upendo na kuwaheshimu wafanyakazi hao.
Tukitathmini, kuna mambo madogo madogo huwa tunajisahau hasa yanayowahusu hawa mabinti.
Mfano, unakuta familia ina watoto wadogo wengi, hiyo adha ya kuwahudumia wote, kusafisha nyumba, kupika, kufua halafu tukirudi nyumbani muda wote tunawafokea.
SOMA ZAIDI: Fahamu Maadili Mema Yanavyojenga Mwenendo Mzuri wa Maisha ya Mtoto
Ama unakuta familia imekwenda matembezi, wamevaa kwa kupendeza na watoto wao, halafu msichana wa kazi anayekulelea watoto kavaa kama chokoraa. Hii siyo sawa.
Tukumbuke kuwa mabinti hawa siyo watumwa, tujitahidi kuishi nao na kuwalea kama unavyotaka mwanao alelewe. Ikiwa uwezo wa kipato unaruhusu watafutie namna ya kuwandeleza.
Kozi za kompyuta, ufundi cherehani, ususi, nakadhalika zinaweza kuwa msaada mkubwa kwao. Haya ni mambo madogo madogo ambayo yanawapatia heshima akina dada wanaotusaidia katika familia zetu.
Tuwafundishe watoto na wanafamilia kuwaheshimu hawa wasaidizi, kwa kuwaonyesha upendo, kuwaongelesha kwa heshima, kuwajali na kuishi nao kwa amani. Tusisahau kwamba hawa ndiyo watu wanaotusaidia kuwalea watoto wetu wakati hatupo.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.