The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mkataba wa Bandari: Matukio Muhimu Kuhusu Suala Linalogawa Maoni ya Watanzania

Mikataba mitatu ya uwekezaji yasainiwa huku baadhi ya wadau wakiendelea kuukosoa vikali mkataba huo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan hapo Jumapili alishuhudia utiaji saini wa mikataba mitatu ya uwekezaji kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Serikali na kampuni ya masuala ya lojistiki ya Dubai ya DP World juu ya uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.

Hafla hiyo iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini, vyama vya siasa na sekta binafsi, iliashiria nia ya Serikali ya kuendelea na mkataba wake na Dubai kuhusu uendelezwaji wa bandari hiyo licha ya kuwepo kwa ukinzani mkali kutoka kwa makundi mbalimbali ya Watanzania.

Akizungumza punde baada ya kushuhudia utiaji huo wa saini, Rais Samia alisema hatua hiyo ya Jumapili ilikuja baada ya Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wale wote waliozungumza kuhusu mkataba huo, akisema hakuna kundi ambalo maoni yake yalipuuzwa.

“Serikali, kwa upande wake, ilisikiliza michango na maoni mbalimbali iliyotolewa na Chama cha wanasheria wa Tanganyika, vyama vya siasa, asasi za kiraia, wanaharakati huru na vyombo vya habari,” alisema Rais Samia. “Pia, tuliangalia maoni katika mitandao ya kijamii. Tumewasikiliza viongozi wetu wa dini na baadhi ya viongozi wetu wastaafu.”

Hata hivyo, hatua hiyo ya jana inakuja baada ya mivutano na kashi kashi nyingi kati ya wale wanaouunga mkono na kuukosoa mkataba huo. The Chanzo inakuwekea hapa baadhi ya matukio muhimu yaliyougubika mkataba huo na yanayodhihirisha utata wake:

Juni 10, 2023: Bunge lapitisha azimio la pendekezo la kuridhiwa kwa mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai utakaupa kampuni ya DP World kuchukua baadhi ya kazi za uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.

Juni 19, 2023: Jeshi la Polisi lawakamata na kuwashikilia kwa siku mbili watu 18 waliohusika na kuandaa maandamano yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kupinga mkataba wa bandari yaliyoratibiwa na mwanachama wa CHADEMA, Deusdedith Soka. 

SOMA ZAIDI: Sakata la Bandari: Je, Serikali Imepoteza Imani ya Wananchi?

Juni 28, 2023: Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili ya mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio ya Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi Katika Maliasili ya nchi ya mwaka 2017 wasomwa bungeni kwa mara ya kwanza. 

Baada ya kusomwa, Kamati ya Bunge ya Katiba na Masuala ya Kisheria ilialika maoni ya wadau kuhusu marekebisho yaliyotarajiwa kufanyika. Sheria hizi zilitarajiwa kurekebishwa ili kuruhusu uwekezaji katika bandari. 

Julai 3, 2023: Kesi iliyofunguliwa na wananchi wanne – Emmanuel Changula, Alphonce Lusako, Raphael Ngonde na Frank Nyalusi – wakipinga vifungu hatarishi vilivyodaiwa kuwepo katika mkataba wa bandari yatajwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya.

Julai 9, 2023: Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, yabariki mchakato wa uwekezaji katika bandari kwa kile ilichoeleza kuwa ni kwa manufaa ya uchumi wa nchi, ikiitaka Serikali iongeze kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari. 

Julai 14, 2023: Rais Samia atetea makubaliano ya mkataba wa bandari, akieleza kwamba mijadala inayoendelea ya kupinga inatishia fursa ya kukuza uchumi wa nchi. Samia pia alieleza kuwa wakati kukiwa na ukinzani nchini, nchi majirani wameiona fursa hiyo na wamewatafuta watu hao kwa ajili ya kukuza uwekezaji. 

SOMA ZAIDI: Sakata la Bandari: Kamati Yaahirisha Kupokea Maoni ya Marekebisho ya Sheria za Maliasili Ikitaka Ufafanuzi wa Serikali

Julai 28, 2023: Chama cha upinzani CHADEMA chazindua Operesheni +255 Katiba Mpya Okoa Bandari Zetu katika uwanja wa Mayunga, Bukoba. Operesheni hii ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya kwenda kwa wananchi wa maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwataka waupinge mkataba wa uwekezaji katika bandari za Tanzania. 

Agosti 7, 2023: Shirika la kimataifa la haki za binadamu, Human Rights Watch, lakosoa na kukemea ukamatwaji wa wakosoaji wa mkataba wa bandari, ikidai kwamba takribani watu 22 walikuwa wanashikiliwa na kutishiwa na mamlaka tangu Juni 10, 2023. 

Agosti 10, 2023: Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, yatupilia mbali kesi iliyofunguliwa kupinga mkataba wa bandari, ikisema hoja zilizowasilishwa kupinga mkataba huo hazikuwa na mashiko.

Agosti 10, 2023: Wanaharakati waliofungua kesi hiyo – Wakili Boniface Mwabukusi pamoja na Mpaluka Nyagali – watangaza kufanyika kwa maandamano na mikutano ya hadhara ya nchi nzima na yasiyokuwa na ukomo kupinga mkataba wa bandari. 

Agosti 11, 2023: Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camillius Wambura, awaonya watu wanaopanga kuandaa maandamano nchi nzima ili kuiangusha Serikali, akisema vitendo hivyo ni vya “kihaini” na kwamba Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu yoyote anayepanga kuiingiza nchi kwenye machafuko.

SOMA ZAIDI: Jenerali Ulimwengu: Sakata la Bandari Limeonesha Tumepoteza Uwezo Kujadiliana kwa Hoja

Agosti 12, 2023: Jeshi la Polisi lathibitisha kuwakamata Wakili Boniface Mwabukusi na Mpaluka Nyagali kwa ajili ya mahojiano. Mwabukusi na Nyagali walikuwa mstari wa mbele kwenye harakati za kupinga mkataba wa bandari.

Agosti 13, 2023: Dk Wilbroad Slaa, kiongozi mwingine kwenye vuguvugu la kupinga mkataba wa bandari, akamatwa na polisi wakati akiwa nyumbani kwake Mbweni, Dar es Salaam, akidaiwa kupanga maandamano ya kupinga mkataba huo.

Agosti 16, 2023: Kamati ya Bunge ya Masuala ya Kisheria yaahirisha kusikiliza maoni ya wadau kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili ya mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio ya Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi Katika Maliasili ya nchi ya mwaka 2017.

Agosti 18, 2023: Wakili Boniface Mwabukusi, Mpaluka Nyagali pamoja na Dk Wilbroad Slaa waliachiwa kwa dhamana. Mpaka wakati wa kuandika habari hii, hakukuwa na taarifa kuhusu mwelekeo wa kesi hiyo.

Agosti 18, 2023: Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) latoa waraka kupinga mkataba wa bandari kati ya Tanzania na Serikali ya Dubai kupitia kampuni ya DP World, ikisisitiza umuhimu wa Serikali kutoa kipaumbele kwa Watanzania kumiliki na kuendesha nyenzo kuu za uchumi wao.

SOMA ZAIDI: Waraka wa Maaskofu Katoliki Kupinga Mkataba Bandari Wasomwa Makanisani Tanzania

Agosti 20, 2023: Waraka wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) wasomwa katika misa mbalimbali za Kanisa Katoliki nchi nzima. 

Agosti 21, 2023: Akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Rais Samia alikanusha madai ya Serikali yake kuuza nchi kwa wageni, akisema kwamba hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuuza na kuligawa taifa.

Septemba 2, 2023: Chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo kilitoa msimamo wao kuhusiana na sakata hilo, kikipendekeza maboresha kadhaa kwenye mkataba kati ya Tanzania na Dubai ili kuiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na mkataba huo.

Oktoba 4, 2023: Polisi Mwanza wadaiwa kongamano la kujadili mkataba wa bandari na Katiba Mpya uliokuwa ukiratibiwa na  taasisi za Tanzania Transparency, Sauti ya Wananchi na Jukwaa la Katiba. Watu kama Mpaluka Nyagali, Dk Wilbroad Slaa na Wakili Boniface Mwabukusi walitarajiwa kuzungumza katika kongamano hilo. 

Oktoba 8, 2023: Polisi Mbeya ladaiwa kuzuia mkutano wa hadhara wa kujadili mkataba wa bandari na Katiba Mpya uliotarajiwa kufanyika katika kijiji cha Kandete, halmashauri ya Busokelo, wilayani Rungwe. Mkutano huo uliandaliwa na taasisi zilezile zilizoandaa kongamano jijini Mwanza.

Oktoba 22, 2023: Samia ashuhudia utiliaji sahihi wa mikataba mitatu ya uwekezaji kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Serikali na DP World, akisema Serikali imezingatia maoni ya wadau wote waliozungumza kuhusu suala hilo kabla ya kuendelea na hatua hiyo ya kusaini mikataba mahususi ya uwekezaji.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts