Wanaharakati pamoja na wadau wa haki wamejitokeza kulaani hali inayoendelea katika maeneo ya wafugaji hasa Loliondo na Ngorongoro ambapo mifugo mingi ya wafugaji imeendelea kutaifishwa kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kuingia katika maeneo ya hifadhi.
Novemba 08, 2023, wanaharakati kutoka mashirika 16 walilaani hali ya utaifishaji wa mifugo ambayo imekuwa ikiendela katika maeneo mbalimbali nchini, wakieleza kuwa hali imekuwa mbaya zaidi katika eneo la Loliondo na Ngorongoro, ambapo waliwashutumu wahifadhi kuvunja haki za msingi za wafugaji.
Serikali imekuwa ikiendesha operesheni mbalimbali zinazotajwa kulenga kuzuia wafugaji kuingiza mifugo katika eneo la hifadhi, ambalo ni takribani asilimia 32.5 ya ardhi yote ya Tanzania. Kupitia Ripoti ya Hali ya Uchumi 2022, Serikali ilionesha kuwa kwa mwaka 2022 pekee iliweza kukamata mifugo 30,030 kupitia doria mbalimbali ilizozifanya.
Wafugaji, wanaharakati na wadau wengine wameendelea kulalamika kwamba mazoezi ya utaifishaji wa mifugo yamejaa uonevu, huku wengi wakieleza ni kama mradi wa kufilisi jamii za wafugaji nchini.
Utata mifugo 1,000 ikipigwa mnada
Moja ya matukio ambayo yameibua gumzo kubwa katika jamii ya wafugaji ni tukio lililotokea Novemba 1, 2023, ambapo Serikali ilipiga mnada zaidi ya mifugo 1,026, ikijumuisha ng’ombe 806, kondoo 120, na mbuzi 100 huko Serengeti.
Akizungumza Bungeni Novemba 09, 2023, Mbunge wa Ngorongoro (Chama cha Mapinduzi – CCM) Emmanuel Ole Shangai, alieleza kuwa kuna mambo kadhaa yenye utata katika utaifishaji huu wa mifugo, moja ya utata huo ukiwa ni askari wa TANAPA kuswaga na kuiingiza mifugo hifadhini kutoka kwenye maeneo ya kijiji.
“Mifugo walikamatwa tarehe 26 mwezi wa kumi kwenye eneo linaloitwa Orkimbai, kijiji cha Kisalo,” alieleza Ole Shangai. “Ng’ombe hao walikamatwa muda wa saa nane na nusu mchana na asakari wa TANAPA wakiwa wanachungwa na vijana watano.
“Askari wale waliswaga wale ng’ombe pamoja na wale vijana wakawaweka chini ya ulinzi na kuwapeleka mpaka kwenye eneo la Olobo, Hifadhi ya Serengeti.”
Pamoja na utata wa kama mifugo hii ilikuwa hifadhini au la, taarifa ya Ole Shangai inaonesha kuwa idadi ya mifugo 757 haionekani katika idadi ya mifugo iliyopigwa mnada.
Ole Shangai alieleza jumla ya mifugo, kwa mujibu wa wamiliki, ilikua ni ng’ombe 1,033 na mbuzi 750 ambazo zilikuwa zikimilikiwa na familia ya Oloomukrusas (ng’ombe 460) na familia ya Sinjorematika (ng’ombe 573) na familia ya Ndagusakooros (kondoo na mbuzi 750).
Utata mwingine ambao ulionekana ni kuwa kesi hii iliendeshwa katika usiri na uharaka, ambapo pamoja na wamiliki kufuatilia kila hatua, hawakushirikishwa, jambo lilopelekea mifugo hii kupigwa mnada kwa kile kilichodaiwa kutotambulika kwa wamiliki wake.
Kwenye taarifa yake hiyo aliyoitoa Bungeni, Ole Shangai alieleza hata kabla ya mifugo kupigwa mnada alishaongea na ngazi zote za Serikali, ikiwemo wahifadhi, Naibu Waziri, na Waziri wa Maliasili, hivyo amebaki kutahamaki mifugo kuuzwa kwa kutokua na mwenyewe.
“Adhabu tunayowapa wananchi wetu ni kuwafilisi?” alihoji Mbunge huyo wa Ngorongoro. “Mpaka sasa kwenye jimbo langu zaidi ya ng’ombe 2,000 wameshataifishwa na wananchi zaidi ya 400 sasa ni maskini wa kutupwa.”
Mmoja wa waathirika wa zoezi hilo la utaifishaji, Amani Lengume, ambaye ni mzee mwenye zaidi ya miaka 65, ameeleza kuwa familia yake imerudi kwenye dimbwi la umasikini ambapo kwa sasa hata chakula hawawezi kumudu.
“Tuna watoto 107 kwenye familia zetu, watoto wamerudi toka shule, hatuna chakula,” alieleza Lengume kwenye kikao cha kijamii Novemba 12,2023, ambapo wanajamii walikusanyika kuwachangia waliopoteza mali zao.
Katika tamko lake mashirika 16 ya wanaharakati yalihoji namna suala zima lilivyoendeshwa kwamba amri ilitolewa Novemba 1, na siku hiyohiyo mnada ukaendeshwa huku wamiliki wa mifugo hiyo wakihaha sehemu mbalimbali, ikiwemo Mhakamani bila kusikilizwa na yeyote.
Akieleza jinsi walivyosumbuka, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mondorosi, Joshua Maakoo, anaeleza walifika mpaka Mahakama ya Musoma na kukutana na mwanasheria wa serikali na wahifadhi ambao walikataa kuwa hakukua na kesi inayohusu mifugo. Maakoo, anaenda mbali zaidi na kusema wana ushahidi baadhi ya mifugo iliuzwa hata kabla ya mnada.
Akijibu hoja ya Mbunge, Novemba 9, 2023, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, alieleza kuwa suala hilo lilimalizwa kwa maamuzi ya Mahakama na kwamba kiasi cha Shilingi 166,264,000 kilipatikana baada ya mifugo hiyo kuuzwa.
“Tarehe 1 mwezi Novemba, hukumu ilielekeza dalali wa Mahakama ateuliwe kwa ajili ya kuweza kupiga mnada wa hadhara kwa kufuata taratibu kama ambavyo sheria yetu ya wanyamapori ya mwaka 2009 lakini vilevile sheria yetu inayosimamia hifadhi ya taifa zinavyoelekeza,” alifafanua Kairuki.
Akiendelea kutolea ufafanuzi zaidi juu ya sakata hilo, Novemba 10,2023, Kairuki alieleza kuwa Wizara imeamua kuchunguza shauri hilo ili kujiridhisha juu ya maelezo yaliyotolewa.
Lakini pia kuhusiana na shauri la Mahakama, Wizara inasubiri hukumu ya Mahakama juu ya shauri la marejeo ya lilofunguliwa Novemba 8 ambapo hukumu inatakiwa kutolewa Novemba 10, 2023.
Utata ndani ya Loliondo
Moja ya eneo ambalo limeendelea kuzua utata huku likiwaacha wafugaji wengi katika hali ya sintofahamu ni eneo katika tarafa ya Loliondo, eneo ambalo lilibadilishwa na kufanywa kuwa pori tengefu na kisha kubadilishwa tena na kuwa hifadhi ya taifa.
Eneo hili lilifanywa kuwa pori tengefu la Pololeti kupitia tangazo la Serikali lililotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Namba 421 la mwaka 2022. Hata hivo, Oktoba 14, 2022, eneo hilo lilitangazwa kuwa pori la akiba kupitia tangazo la Serikali lilotolewa na Rais alitangaza tena eneo hilo kuwa ppori la akiba la Pololeti.
Eneo hili lilizua mzozo kati ya wafugaji na Serikali, ambapo Juni 10, 2022, askari mmoja aliuwawa huku wananchi wengi wakikimbia makazi yao. Serikali iliamua kulitangaza eneo hilo la kilomita za mraba 1,500 kuwa pori tengefu na kisha kuwa hifadhi.
Eneo hili ambalo moja ya shughuli yake kubwa ni uwindaji, kwa wananchi wanalitaja kama eneo muhimu la malisho kwao hasa nyakati za ukame.
Hivyo, baada ya Serikali kulifanya pori la akiba na kisha hifadhi, wananchi walikimbilia Mahakamani ambapo Mahakama ilieleza kuwa uundaji wa pori tengefu haukufuata sheria, na pia Mahakama ikaagiza utekelezaji wa tangazo la pori la akiba usitishwe
Kutokana na amri hiyo ya Mahakama, wananchi wanaamini wana haki ya kutumia eneo hilo, hata hivyo mifugo yao imeendelea kukamatwa.
Latajewo Sayori ni mmoja ya wakazi wa Loliondo walioshiriki kwenye shauri lililoweza kuwapa ushindi, anayedai kwamba kuna kudharau amri za Mahakama.
“Mamlaka zinazosimamia eneo lile, kwa maana ya NCCA, imekuwa ikikiuka na kutoheshimu maamuzi ya Mahakama,” alisema Sayori kwenye mkutano na waandishi wa habari. “[NCCA] imeendelea kushika mifugo na kuwakamata toka Oktoba 4, 2023 baada ya amri ya mahakama.
“Mpaka tunapoongea hivi sasa, kijiji cha Olesosokwan wameshikiliwa ng’ombe wapatao 754 na kata ya Arash wameshikiliwa ng’ombe 327 pamoja na kondoo na mbuzi wapatao 645,” alifafanua zaidi Sayori.
Kutokana na hali hii ya mashaka, wanakijiji wa kijiji hicho wameeleza kuwa wameendelea kufukarishwa na kufanywa wanyonge kupitia utaifishaji unaofanywa.
“Sisi rasilimali zetu tunategemea mifugo,” aliongeza mwanakijiji mwingine, Kaiyayo Siringeti, kwenye mkutano huo na wanahabari. “Kwamba upeleke mifugo mnadani tupate mahindi ya watoto tunaathirika sana.”
Wanaharakati wanaeleza kuwa hali inaendelea kuwa mbaya Ngorongoro, ambapo watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wanadaiwa kuinyima mifugo wanayoikamata maji na malisho kama njia ya kutoa shinikizo kwa wafugaji kulipa faini ya Shilingi 100,000 kwa mfugo.
Hali hii ya utaifishaji wenye maswali imekuwa ikilalamikiwa maeneo mengi nchini, ikiwemo Lindi, Mbarali na Tarime. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikijitetea kwa kueleza kwamba lengo la utaifishaji ni kulinda hifadhi, maliasili na uoto wa asili wa Tanzania.