Mzazi au mlezi, umejiandaaje kuimarisha uhusiano wako na mtoto wako mwaka huu?
Je, kwa mtoto ambaye ni mkorofi sana au mpole na mkimya sana, ni mikakati gani uliyoiandaa kama mzazi kumlea mtoto huyu katika njia iliyo sahihi isiyoweza kuathiri uhusiano wako na wa mtoto wako?
Ni ukweli usiopingika kuwa, majukumu ya kujitafutia vipato yanaendelea kuongezeka na kupelekea kutingwa sana kwa wazazi. Suala hili limesababisha wazazi kukosa muda wa kukaa na watoto vizuri ili kujenga ukaribu na kuwafahamu watoto kwa undani zaidi.
Ni vyema kutambua kwamba aina ya mahusiano kati ya mzazi, au mlezi, na mtoto unachangia kwa kiwango kikubwa maendeleo chanya au hasi ya tabia ya mtoto kimwili, kihisia na kisaikolojia.
Uhusiano wa karibu na mtoto wako unakuhitaji wewe kuingia katika ulimwengu wa kufikiri na kuwaza kama mwanao awazavyo. Kama mzazi, ni muhimu kutambua kwamba kati ya vitu ambavyo mtoto atakumbuka katika maisha yake, ni vitu vikuu viwili: upendo na kiasi cha muda aliotumia na wazazi au walezi wake.
SOMA ZAIDI: Tuzungumze Kuhusu Umuhimu wa Lishe Bora kwa Watoto na Misingi Yake
Kwa hiyo, ni muhimu kwa mzazi au mlezi kujitahidi anampatia vitu hivi mtoto wake. Mzazi au mlezi unaweza kufanikisha hili kwa kujifunza kuwa msikivu zaidi kuliko muongeaji.
Watoto wana tabia ya kuongea mara kwa mara yale yote yanayowasumbua, lakini wazazi, au walezi, wengi wamekuwa wakipuuzia na kuona watoto bado ni wadogo na hawana uwezo wa kuelewa na kuongea yale wanayoyasema.
Pata muda mzuri wa kucheza na mtoto wako, michezo anayofurahia ili anapoendelea kukua akukimbilie wewe kama rafiki na mshauri wake mkuu, na si kama adui yake anayempiga na kumgombeza kila wakati.
Jifunze kumrekebisha mtoto kwa kumwelekeza zaidi kuliko kumkaripia, kumtukana, au kumpiga kila anapokosea; mwelekeze kwa ustarabu ili asikutii kwa kuoga bali kwa kuhofia madhara atakayoyaleta kulingana na matendo yake.
SOMA ZAIDI: Kama Mzazi, Unawezaje Kujali, Kulinda Afya Yako ya Akili?
Mtoto anatakiwa akuheshimu kama mzazi na siyo kukuogopa. Mtoto anatakiwa afurahie uwepo wako na siyo kuhuzunika au kujitenga mbali na wewe uwapo karibu yake.
Njia nyingine nzuri ya kuunda ukaribu huu ni kwa kujenga mahusiano ya kihisia kupitia ishara za kimwili kama kumkumbatia mtoto, kumwambia maneno mazuri ya kumsifia, kumtia moyo na kumpatia ujasiri.
Mzazi jiwekee utaratibu wa kujua siku ya mtoto wako iliendaje kwa kumuuliza maswali, kujua hisia zake na vitu vinavyomfanya asijiamini na vinavyomkosesha furaha hata kama ni vidogo kiasi gani, kwani vitu vidogo ndivyo vyenye matokeo makubwa kwa maendeleo ya tabia ya mtoto, kuwa chanya au hasi.
Ni vyema ukaweka utaratibu wa kukaa na mtoto kwa muda maalumu, kama utaratibu wa kusali kwa pamoja upo basi fanya hivyo, au pia unaweza kumsimulia hadithi fupi muda wa kulala.
SOMA ZAIDI: Vitu Muhimu vya Kufanya Kwa Ajili ya Mtoto Wako Akiwa Shuleni
Watoto ni zawadi tuliyopewa na Mwenyenzi Mungu, Hivyo basi, wazazi na walezi tunapaswa kuwalea na kuwatunza watoto wetu kwa ukaribu kadri tuwezavyo.
Familia na watoto wetu wanapaswa kuwa kipaumbele kwetu, tupunguze sababu ya kutingwa na majukumu yetu ya kimaisha yanayotufanya tusahau uzuri wa watoto maishani mwetu.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.