The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Rais Samia Ataka Kuimarishwa Kwa Mfumo wa Haki Jinai na Madai Nchini

Rais Samia amesema kuna uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria hususani katika maeneo ya ardhi, matunzo ya watoto, ndoa ,mirathi, ukatili wa kijinsia na madai

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuna umuhimu wa kuimarishwa kwa mfumo wa haki jinai na madai nchini kutokana na ucheleweshaji wa mashauri na kukosekana kwa msaada wa kisheria miongoni mwa wananchi. 

Rais Samia amezungumza haya katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika makao makuu ya nchi jijini Dodoma, Alhamisi, Februari 1, 2024. 

Katika hotuba yake Rais Samia amesema kuna uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria hususani katika maeneo ya  ardhi, matunzo ya watoto, ndoa ,mirathi, ukatili wa kijinsia na madai kwa mujibu wa taarifa ya kampeni ya msaada wa kisheria wa mama Samia.

“Katika mahakama wanasema kwamba inachukua hadi miezi 12 kwa shauri lililopo katika mahakama ya wilaya na mahakama ya hakimu mkazi kusikilizwa hadi kuhitimishwa,” amesema Rais Samia.

“Sasa hii inachukua muda mwingi wa wadau wanaohusika kwenye mashauri haya na wanapoteza muda wa kufanya mambo mengine muhimu.” 

Rais Samia pia amesisitiza usikilizwaji haraka wa kesi zinazohusu masuala ya kibiashara ili kuwezesha mazingira bora ya kufanya biashara nchini, kwani wawekezaji huangalia masuala ya kisheria na utatuzi wa migogoro ya kibiashara wanapotaka kuwekeza.

“Mfumo wa haki madai na kwenyewe pia kuna malalamiko, kesi zinacheleweshwa, mzunguuko ni mkubwa,” 

Kutokana na hali hiyo, Rais Samia amewataka wadau wa Haki Jinai na Madai kufanyia kazi changamoto zinazopelekea ucheleweshaji wa mashauri hayo.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yalianza Januari 24, 2024 na yamehitimishwa Februari 1, 2024, huku kauli mbiu ikiwa ni “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau Katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.”

Taasisi za Haki Jinai zikubali kutathminiwa

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo  Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema katika kuhakikisha wanazimaliza changamoto zinazoikabili Mahakama, wamekuwa na utaratibu wa kutumia taasisi za nje kuwatathmini.

Katika tathmini ya mwisho kuhusu utendaji kazi wa Mahakama iliyofanywa na taasisi ya Research on Poverty Alleviation in Tanzania (REPOA), Jaji Prof. Ibrahim ameeleza kuwa ingawa viwango vya hisia vya rushwa dhidi ya Mahakama vimepungua, bado kuna malalamiko mengi kwenye mahakama za wilaya na hakimu mkazi.

Kutokana na hilo Jaji Prof. Ibrahim  amesema, taasisi za haki jinai zinapaswa kukubali kutathminiwa na taasisi za nje ili kuweza kubaini mapungufu yake na kuyafanyia kazi.

“Kujitathmini wenyewe ni ngumu kuona baadhi ya mapungufu yao.” Alisema Jaji Prof. Ibrahim.

Kutokana na matokeo ya utafiti na mambo yaliyoibuliwa na REPOA katika tathmini yake ya mwisho kwa Mahakama, Rais Samia ametoa rai kwa Mahakama kuzingatia yale yaliyoibuliwa na kuzitaka taasisi nyingine nazo zikubali kufanyiwa tathmini.

“Naomba taasisi nyingine zote tushirikiane kujitathmini tubaini mapungufu na tuchukue hatua kwa pamoja.” Amesisitiza Rais Samia.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts