Wamiliki wa hospitali binafsi wametangaza kurudisha huduma kwa wateja wanaotumia Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF), hii ikiwa ni siku moja toka kuanza mgomo wa kutopokea bima hizo mnamo Machi 01,2024.
Hospitali hizo zilifikia maamuzi hayo baada ya kutokubaliana na maamuzi ya NHIF kubadili bei ya huduma mbalimbali zinazotolewa kupitia bima.
Mapema asubuhi ya leo Machi 02,2024, The Chanzo iliitembelea vituo binafsi mbalimbali katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Dodoma na kukuta wateja wa NHIF wakishauriwa kulipa kwa fedha taslimu huku kadi za NHIF zikikataliwa kupokelewa.
Hata hivyo mpaka jioni ya leo tayari hospitali zimeanza kutangaza kurudisha huduma kwa wateja wa NHIF.
Katika tamko lao la pamoja Uongozi wa Bodi ya Wamiliki wa Vituo vya Afya Binafsi (APHTA) na Jumuiya ya Wamiliki wa Hospitali Binafsi Zanzibar (ZAPHOA) wamesema wamefikia uamuzi huo baada ya serikali kuonyesha utayari wa kurudi katika meza ya mazungumzo.
“Tunapenda kusisitiza kwamba lengo la APHTA ni kutoa huduma bora za afya katika mzingira ambayo yanazingatia hali ya soko na uhalisi wa gharama za uendeshaji. Kamwe, dhamira yetu si kuwaumiza wananchi wahitaji ambao ni wanachama wa NHIF,” limeeleza sehemu ya tamko hilo.
Mfuko wa Bima ya Taifa una watumiaji takribani milioni 4.9 nchi nzima.