Mpango wa kuja na namba moja ya utambulisho kwa Watanzania toka kuzaliwa imeanza kufanyiwa kazi na inategemewa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2025. Haya yameelezwa mnamo Machi 08,2024, katika mkutano wa taasisi za kifedha, mkutano uliofanyika jijini Arusha.
“Rais ametoa maagizo kuwe na namba moja ya utambulisho maalum kwa Watanzania wote na kazi hii imeanza chini ya Wizara ya Mawasiliano na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa,” alieleza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Injinia Benedict Benny Ndomba.
“Wanafanya kazi pamoja kuileta Jamii Namba, namba maalum ya utambulisho kwa kila Mtanzania kuanzia anapozaliwa, na kwa wageni kuanzia wanapoingia nchini mpaka wanapoondoka,” aliongeza Ndomba.
Ndomba alikuwa akijibu swali toka kwa washiriki wa mkutano kuhusu ikiwa serikali ina mpango wa kufanya namba ya NIDA kupatikana kwa watoto.
Rais Samia Suluhu alitoa agizo la kuja na namba moja ya utambulisho mnamo Agosti 10,2023, hii ni baada ya kuonesha kutokuridhishwa na utitiri wa namba za utambulisho zinazotumika na watanzania.
“Lakini niseme na watoa huduma ndani ya Tanzania, mabenki, Wizara ya Elimu inayoandikisha Watanzania wakiwa wadogo, lakini Wizara ya Afya inayotibu Watanzania na wizara nyingine zote zinazotoa huduma, hebu sasa twendeni tukatumie namba moja tu ya Mtanzania,” alieleza Rais Samia.
“Namba moja tu ya Mtanzania. Anapoambiwa Samia Suluhu ni namba 20 ndani ya Tanzania basi taarifa zangu zote, taasisi zote zikivuta namba 20 awe Samia Suluhu mmoja yule yule taarifa zile zile,” alifafanua zaidi.
Katika mkutano huo wa taasisi za kifedha wadau kutoka katika kampuni za simu na mabenki walionesha kusikitishwa na kasi ya utoaji wa vitambulisho vya taifa , suala linalofanya watu kutumia vitambulisho visivyo vyao katika kutafuta huduma mbalimbali.
Kwa sasa ni mapema kuweza kuona picha kamili ya namna Jamii Namba itakavyotolewa na kufanya kazi, ingawa timu inayohusika na uundaji wa namba hii tayari wana imani kubwa.
Akifafanua juu ya maendeleo ya kazi hii, Dk John Sausi ambaye ni Mkurugenzi wa Mifumo ya TEHAMA toka Wizara ya Fedha ameeleza kuwa kazi hii inategemewa kuisha mwishoni mwa mwaka 2025.
“Tunavyoongea sasa hivi tayari wataalamu wameshamaliza kuandaa muundo wa namba hiyo, hii inafanyika kwa mashirikiano kati ya RITA, NIDA na Zanzibar ID. Tunategemea kazi hii itaisha mwishoni mwa mwaka 2025,”alieleza Dr Sausi