Ndege mpya ya Boeng B 737-9 kuwasili nchini kesho
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, leo Machi 25, 2024, amesema kuwa ndege mpya aina ya Boeng B 737-9 Max itawasili hapa nchini kesho kuanzia saa 4:00 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ikitokea nchini Marekani.
Chalamila aliyezungumzia maandalizi ya mapokezi ya ndege hiyo kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ametoa rai kwa Watanzania wote hususani wakazi wa Dar es Salaam, viongozi mbalimbali kwenda kwa wingi kushuhudia mapokezi hayo.
Kuongezeka kwa ndege hiyo kunalifanya shirika hilo liwe na jumla ya ndege 14 ambapo, kati ndege hizo moja ni ya mizigo na zinazobakia zinabeba abiria.
Mawasiliano ya barabara ya Dar es Salaam na mikoa ya kusini yarejea
Mawasiliano ya barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kwenda ya mikoa Lindi na Mtwara yamerejea leo mchana mara baada ya kukamilika kwa ukarabati wa daraja la Somanga lililokatika tangu jana majira ya saa 12 jioni.
Akitoa taarifa hiyo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Lindi, Injinia Emil Nzengo, amesema tayari magari ya abiria na mizigo na vyombo vingine vya usafiri vimeruhusiwa na kuanza kupita upande mmoja wa daraja hilo ambalo lilikuwa halipitiki.
Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, changamoto hiyo ambayo imewaathiri kwa kiasi kikubwa watumiaji wa barabara hiyo imesababishwa na mvua kubwa iliyonyesha kwenye maeneo hayo siku za hivi karibuni.
Hii ni mara ya pili kutokea tukio kama hili katika barabara hiyo. Machi 4, 2024, katika eneo la Maili Mbili barabara ya Mingoyo-Masasi, daraja lilisombwa na maji na kupelekea mawasiliano kukatika kati ya Masasi, mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Dar es Salaam.
Mwanza: Mgomo wa wafanyabiashara Misungwi waingia siku ya nne
Mgomo wa wafanyabiashara wa wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, umeingia siku ya nne tangu ulipoanza Machi 22, 2024.
Wafanyabiashara hao wamesitisha kutoa huduma kwenye maduka kwa sababu hawakubaliani na ushuru wa huduma ambao wanadai kuwa umekuwa ukikusanywa pasipo utaratibu maalumu.
Baada ya kuanza kwa mgomo huo, wafanyabiashara hao waliahidiwa kuwa Machi 23, 2024, mkuu wa wa Mwanza, Amos Makalla, angewafuata na kuwasikiliza kero zao.
Ahadi hiyo imekwenda hadi leo Machi 25, 2024, mkuu wa wilaya ya Misungwi, Johari Samizi, alipokutana na wafanyabiashara hao na kuwasikiliza ambapo, ameahidi kufanyia kazi madai waliyoyaibua huku akiwataka wafungue maduka yao.