Bajeti ya kulipa deni la Serikali kwa mwaka 2024/2025 yaongezeka
Kwa mwaka wa fedha ujao wa 2024/2025 Tanzania inatarajiwa kutumia Shilingi trilioni 13.13 kwa ajili ya kulipa madeni, kiwango ambacho kimeongezeka kutoka Shilingi trilioni 10.48 ambacho Serikali ilipanga kutumia kwa mwaka wa fedha unaoisha wa 2023/2024.
Taarifa hiyo imetolewa leo Juni 4, 2024, na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, bungeni jijini Dodoma, wakati alipokuwa anawasilisha hotuba Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa 2024/2025.
Mwigulu amesema kuwa Serikali imetenga kiasi hicho cha fedha ikiwa ni kwa ajili ya urejeshaji wa mikopo iliyochukuliwa kwa wakopeshaji mbalimbali kupitia deni la Serikali.
Aidha, hadi kufikia Aprili 2024 wizara hiyo ilikuwa imelipa kwa wakati notisi za madai ya deni la Serikali lililoiva jumla ya Shilingi trilioni 8.48, sawa na ufanisi wa asilimia 81 ya lengo la mwaka.
Kwa mujibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hadi kufikia Juni 2023, deni la taifa lilikuwa ni Shilingi trilioni 82.25 sawa na ongezeko la asilimia 15 kutoka Shilingi trilioni 71.31 lililokuwepo kwa mwaka 2021/22.
Mkopo wa Tanzania wa Shilingi trilioni 6.2 kutoka Korea Kusini waibua gumzo mitandaoni
Wadau mbalimbali wameitaka Serikali iweke wazi mkataba wa mkopo wa dola za Kimarekani bilioni 2.5, sawa na takribani Shilingi trilioni 6.2 ambazo Tanzania inategemea kuzipata kwa makubaliano ambayo hayajawekwa wazi na nchi ya Korea ya Kusini.
Hatua hiyo inakuja kufuatia taarifa iliyotolewa jana Juni 3, 2024, na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VOA) ikieleza kuwa Tanzania itapokea mkopo huo na kutoa sehemu ya bahari yake na madini, jambo ambalo liliibua hisia kali miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Mavura, aliibuka na kukanusha madai hayo huku akidai kwamba Tanzania haijasaini mkataba wowote na taifa ilo wenye kipengele cha kutoa sehemu ya rasilimali zake.
Mavura aliongeza kuwa mkataba uliosainiwa ni mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za Kimarekani bilioni 2.5 kwa ajili ya miradi ya miundombinu.
Hii siyo mara ya kwanza kwa wadau mbalimbali kushinikiza Serikali iweke wazi mikataba inayoingia. Oktoba 2023 suala kama hili liliwahi kushinikizwa mara baada ya Serikali kuingia mkataba wa uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam na kampuni ya Dubai ya DP World.
Mkataba ambao uliingiwa licha ya kuwa kulikuwa na upinzani mkali dhidi yake lakini Serikali ikadai kuwa kabla ya kusainiwa ilisikiliza maoni ya watu wote.
Tanzania, Indonesia kushirikiana kuutangaza utalii
Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Indonesia zimepanga kushirikiana kwa pamoja kuutangaza utalii ili kupanua wigo wa mazao ya utalii na kukuza utalii wa nchi zote mbili.
Mpango huo umekuja kufuatia kikao kilichofanyika kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki na ujumbe kutoka Bunge la Indonesia ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikiano wa Mabunge wa Bunge la Jamhuri ya Indonesia, Fadli Zon, kilichofanyika leo Juni 4, 2024, jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho waziri Kairuki amesema kuwa Tanzania na Indonesia inaweza kushirikiana katika kutangaza utalii wao kwa kuunganisha vifurushi vya utalii na kutangaza kwa pamoja nchi hizo mbili ili kuongeza idadi ya watalii.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Indonesia kuwekeza nchini katika huduma ya malazi kwenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji ndani ya hifadhi na nje ya maeneo ya hifadhi.