The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

ACT Wazalendo, CHADEMA waishutumu TAMISEMI kwa kupoka majukumu ya Tume ya Uchaguzi 

Vyama vya upinzani vya ACT Wazalendo na  CHADEMA vimeishutumu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwa haistahili kusimamia zoezi la uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, kwani kwa kufanya hivyo itakuwa inapoka mamlaka ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC). 

Kauli hiyo imetolewa kufuatia wizara hiyo kuvitaarifu vyama hivyo kuwa vinaalikwa kutoa maoni kuhusu rasimu ya kanuni za uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024, zoezi ambalo limeelezwa kuwa litafanyika Juni 15, 2024, jijini Dodoma. 

Madai haya yanatokana na kile kilichoelezwa kwenye Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2024,  kifungu cha 10 (1) (c ), kuwa tume hiyo ndiyo itakuwa na wajibu wa kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi huo lakini kwa utaratibu utakaoainishwa na sheria itakayotungwa na Bunge. 

Hata hivyo, tangu sheria hiyo ilivyopitishwa Aprili 2024 hakujawa na mchakato wowote wa kupelekwa kwa muswada bungeni ili sheria itakayosimamia uchaguzi huo iweze kutungwa. 

Reli ya TAZARA kufumuliwa kwa ajili ya marekebisho 

Serikali za Tanzania, Zambia na China zipo katika hatua za mwisho za mazungumzo ya mpango wa kuifumua reli ya TAZARA kwa ajili ya kuiboresha na kuimarisha shughuli za usafirishaji. 

Hayo yamebainishwa na leo Juni 12, 2024, bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, wakati akijibu swali mbunge wa Mlimba kupitia Chama cha Mapinduzi, Godwin Kunambi, aliyehoji mkakati wa Serikali kuboresha miundombinu ya reli hiyo inayounganisha nchi ya Tanzania na Zambia. 

Kihenzile ameongeza kuwa mpaka sasa tayari kikao kimeshafanyika kati ya Rais wa Tanzania, China na Zambia kwa ajili ya kufumua, na kukarabati reli hiyo lengo likiwa ni kuongeza uwezo wa kubeba mizigo, kuongeza vichwa vya treni pamoja na mabehewa ya kubebea mizigo ya abiria.

Reli ya TAZARA yenye urefu wa kilomita 1,860 ilijengwa kwa ushirikiano wa mataifa ya Tanzania, Zambia na China na ikaanza kufanya kazi rasmi Julai 14, 1976. Reli hiyo imekuwa kiungo kikubwa cha biashara baina ya Tanzania na Zambia kwani imekuwa ikisafirisha mizigo na raia baina ya mataifa hayo. 

Wizara ya Madini yazindua timu yake ya kuandaa andiko la maudhui ya utafiti wa madini

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, leo Juni 12, 2024, amezindua timu itakayokwenda kuandika andiko la maudhui ya utafiti wa madini lililopewa jina la ‘vision’ 2030, andiko ambalo linatarajiwa kutoa dira ya kufikia asilimia 50 ya utafiti wa madini ifikapo mwaka 2030.   

Akizungumza katika uzinduzi huo ambao umefanyika jijini Dodoma, Mavunde amesema kuwa utafiti wa madini uliofanyika kwa nchi nzima hadi hivi sasa upo kwa asilimia 16 tu, ndiyo maana wakaona haja ya kuunda timu hiyo ili itoe taswira mpya ya sekta hiyo muhimu. 

Waziri huyo ametangza kuwa timu hiyo itaongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ndani yake ikiwa na wajumbe wengine 12 ambao watatakiwa kuzifanyia kazi hadidu za rejea 14 walizopewa. 

Nchini Tanzania, sekta ya madini ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wananchi. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2022/2023, migodi ilifanya manunuzi ya dola za Kimarekani bilioni 1.6, ambapo dola bilioni 1.4 zilihusisha kampuni za Kitanzania na hivyo kufanya zaidi ya asilimia 86 ya manunuzi yote ya migodi katika mwaka huo yawe yamefanywa na Watanzania.