The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kelele Zinazoshinikiza Kufungwa kwa Mitandao ya Kijamii Zinadhihirisha Uwezo Mdogo wa Kufikiria wa Watu Wetu

Watu wanaotaka X ifungwe wangebomoa nyumba ili kumtoa mende aliyekimbilia uvunguni mwa kitanda!

subscribe to our newsletter!

Nimejizuia kutoa maoni yangu kuhusiana na kelele za baadhi ya watu, wakiwemo wanasiasa na viongozi wa dini, zinazoishinikiza Serikali iufungie mtandao wa kijamii wa X, zamani Twitter, eti kwa sababu mtandao huo unaonesha sana maudhui ya ngono, maudhui ambayo waheshimiwa hawa wanadai yanakinzana na maadili ya Kitanzania.

Sababu kubwa kwa nini nimejizua kutoa maoni yangu kuhusu pendekezo hilo ni kwamba mapendekezo hayo, kwanza, yametolewa kutoka kwenye mtazamo wa kijinga, yaani ukosefu wa uelewa wa namna ambavyo mitandao hiyo ya kijamii inafanya kazi, lakini, pili, yametolewa kwa nia ovu na nadhani kuyajadili ni kujaribu kuyapa uhalali.

Ni sawa na kusema ujadili mada isemayo, Kati ya Nyerere na Mwinyi, Nani Alikuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania? Au, Watu wa Kabila Fulani Hawapaswi Kuishi, Nini Maoni Yako? Kwenye mada ya kwanza utakuwa unashiriki kwenye ujinga ambao hautakuwa na faida yoyote zaidi ya kukupotezea muda tu. Kwenye mada ya pili utakuwa unashiriki kuyapa uhalali baadhi ya mawazo ya hatari ambayo, badala ya kujadiliwa, yanapaswa kudhibitiwa.

Lakini nimeona nitumie safu yangu hii ya kila wiki kuzungumzia sakata hili kwani naona ni kielelezo kingine miongoni mwa vielelezo milioni vinavyotukabili kila siku na kudhihirisha uwezo wetu hafifu sana wa kufikiria kama wananchi, hali inayoibua mashaka sana hususan ukizingatia kwamba baadhi ya watu wanaodhihirisha uwezo huu mdogo wa kufikiria mara nyingi hujikuta wakipewa nafasi za uongozi wa umma.

Kwenye sakata hili la kuitaka Serikali ifungie mtandao wa X, uwezo mdogo wa kufikiri wa watu wanaouza hoja hiyo unajidhihirisha kwa kushindwa kwao kuelewa kwamba mtandao wowote wa kijamii una maudhui ya kila aina, na mfumo wa kiufundi wa mtandao huo humpatia mtumiaji aina fulani ya maudhui kulingana na historia ya maudhui anayopenda kula akiwa anatumia mtandao huo.

SOMA ZAIDI: Twitter: ‘Jamhuri’ Inayoitingisha Jamhuri ya Tanzania?

Hii ni kusema, kama unapenda sana habari za mauji ya kimbari ambayo dola la Kizayuni la Israel inayafanya huko Palestine, na unaingia X kutafuta habari hizo, mtandao huo utakupatia aina hiyo ya maudhui. Vivyo hivyo kama unapenda ufugaji wa mbwa au mapishi, na unakwenda X kutafuta maudhui hayo, utapewa na mtandao huo.

Kwa hiyo, kwanza, mimi nawaamini hawa watu wanaosema wakiingia X wanakutana na maudhui ya ngono, ni kwa sababu inaonekana hayo ndiyo maudhui wanayokula wakiwa kwenye jukwaa hilo, na hivyo mifumo yake inawasukumia hayo maudhui kwa sababu historia zao za utumiaji zinaonesha wanafurahia maudhui hayo.

Na inawezekana watu hawa hali hiyo inawatesa kisaikolojia, yaani ni hali ambayo wangependa kuondokana nayo, na wanadhani labda Serikali kuufunga mtandao huo utazisaidia jitihada zao hizo binafsi za kutibu majeraha yao ya kihisia. Ndipo uwezo mdogo wa kufikiri unapokuja hapo, kwamba watu hawa wanashindwa kujua wanaweza kujitibu kisaikolojia bila kushinikiza kufungwa kwa X.

Kuna njia nyingi ambazo watu hawa wangezitumia kujiweka mbali na maudhui wasiyoyapenda endapo tu kama wangekuwa na utayari wa kusumbua bongo zao. Wangeweza kuacha kutumia mitandao ya kijamii kabisa kabisa, au, kama hawawezi kufanya hivyo, wanaweza kuuamrisha mtandao husika usiwaoneshe maneno fulani kwa kuya mute, pamoja na mbinu zingine.

Namna ya pili ambapo maoni ya kuitaka Serikali kufungia X yanavyodhihirisha uwezo mdogo wa kufikiri kutoka kwa wale wanayoyatoa ni kudhani kwamba mabavu ya Serikali yanaweza kweli kutumika kudhibiti kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, ikiwemo ukuwaji wa mitandao ya kijamii.

SOMA ZAIDI: Tuimarishe Mifumo ya Utoaji Haki Ili Wanasiasa Waliojigeuza Masiha Waache Kuwapumbaza Wananchi

Uwezo wao mdogo wa kufikiri unadhirishwa na kushindwa kwao kujua kwamba hata kama Serikali itafungia mtandao wa X, itakuwa imewatangazia tu watu kwenda kwenye mtandao mwingine, kwani kuna mitandao mingi ya kijamii, na kuendelea kufurahia vitu wanavyovifurahia. Na hata kama ingekuwa hakuna, watu wangebuni mtandao wao mpya.

Maoni haya, naendelea kusema, ni kielelezo cha uwezo hafifu sana wa kufikiria unaotukabili Watanzania tuliowengi. Wanaotoa maoni haya wangegundua hili kama wangekuwa tayari kuifuata hoja yao hiyo mpaka mwisho wake kimantiki ambapo wangehitimisha kwamba kufungia mtandao siyo suluhisho ya kuwazuia watu wasile maudhui fulani kwenye intaneti. 

Isingekuwa inatia hofu, angalau kwangu mimi binafsi, kama watu wenye uwezo mdogo kama hawa wangekuwepo tu kwenye jamii, wakifanya shughuli zao binafsi. Kwa bahati mbaya sana, watu hawa, kama ambavyo imedhihirika mara kwa mara, hujikuta wakipewa dhamana ya kuendesha ofisi za umma na kuamua hatma ya mamilioni ya wananchi.

Pengine hiyo inaweza kuelezea kwa nini bado Tanzania imekita mizizi kwenye dimbwi la umasiki wakati mataifa mengine yako mbioni kujitafutia maendeleo. Unadhani ni mchango gani kwenye ujenzi wa taifa mtu anayedhani Serikali inapaswa kufungia mtandao wa kijamii anaweza kutoa?

Tutafakari kwa pamoja namna tunavyoweza kuongeza uwezo wetu, na ule wa wananchi wenzetu, kwenye kufikiri. Uwezo wetu wa kufikiri kama wananchi ndiyo utakaotuwezesha kuja na majibu na suluhu za kweli za matatizo yetu badala ya haya yanayofanana na kukusudia kubomoa nyumba ili tu uweze kumuua mende aliyekimbilia uvunguni mwa kitanda!

Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts