The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mambo Muhimu Wazazi Tunapaswa Kuwafundisha Vijana Wetu

Wazazi na walezi tunapaswa kuchukua nafasi kuwafundisha vijana wetu mambo haya muhimu. Kwa kufanya hivyo, tutawasaidia kujenga maisha yenye mafanikio na maadili mema.

subscribe to our newsletter!

Wazazi na walezi tuna jukumu kubwa katika kulea na kuwaongoza watoto na vijana wetu. 

Elimu na mafunzo wanayopokea nyumbani ni muhimu sana katika kujenga tabia na mwenendo wa maisha yao ya baadaye. 

Kuna mambo muhimu ambayo wazazi na walezi tunapaswa kuwafunza vijana wetu ili kuwasaidia kujenga maisha yenye mafanikio na maadili mema. Moja kati ya mambo haya ni kujiendeleza. Vijana wetu wasiruhusu siku ipite bila kujifunza kitu kipya. 

Wajitahidi kujenga tabia ya kusoma vitabu vya aina mbalimbali na vyanzo vingine vya maarifa kama vile tovuti na mitandao ya kijamii yenye maudhui muhimu ili kujielimisha juu ya namna ulimwengu na tamaduni mbalimbali ambazo hawajifunzi shuleni. 

Kusoma vitabu kutapanua maarifa yao na kuwaandaa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za maisha.

Usafi na utanashati ni muhimu, lakini vijana wakumbuke kuwa tabia zao ni muhimu zaidi kuliko muonekano. Kuwa watu wema, wakweli, na ambao wanaweza kutegemewa. Tabia nzuri, uaminifu na maarifa zitawafungulia milango mingi ya fursa maishani kuliko muonekano wa nje.

SOMA ZAIDI: Tufahamu Kuhusu Ukatili Dhidi ya Watoto, Changamoto Zilizopo na Suluhisho

Vijana wetu wana mengi ya kufanya ili kujenga maisha yao. Mahusiano ya kingono yanaweza kusubiri mpaka watakapokuwa wakubwa na wakati ukifika. Wajikite zaidi kwenye masomo na kujenga msingi mzuri wa maisha yao ya baadaye. 

Tusiache kuwahabarisha juu ya mdhara ya ngono za mepema kiafya na kimaendeleo kwa ujumla ili kuwasaidia kujikita katika mambo muhimu yanayojenga misingi imara ya kujitegemea watakapokuwa wakubwa.

Kuna misemo kwamba Macho na kichwa ni mlango wa moyo na Ubongo uliolala ni karakana ya shetani. Watoto na vijana wafahamishwe kuwa wanachoangalia au kusoma, hasa kupitia mitandao ya kijamii, kinaweza kuathiri mawazo, hisia na matendo yao. 

Wachague kwa makini vitu wanavyoangalia na wasiruhusu mambo mabaya kuathiri mawazo na tabia zao. Wazazi/walezi tunapswa kuanza mazungumzo na watoto wetu juu ya hili wangali wadogo ili kuwatahadharisha na kuwajengea utayari wa kujisimamia na kutokushawishika na msukumo wa makundi rika.

Tuwafundishe watoto kuwa makini na vile wanavyoweka kwenye mitandao ya kijamii. Kumbuka, mitandao haina ‘DELETE’ na haisahau kamwe, maana yake ni kwamba, mtoto afahamishwe kuwa taarifa yake anayoiweka mtandaoni haitafutika kamwe, na hata akijutia baadaye hakutakuwa na namna ya kurekebisha hilo. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Watoto Wanapaswa Kufahamu Kuhusu Siku ya Mtoto wa Afrika?

Wasijibizane na watu wala kuwaonea watu mtandaoni pia; wasipige wala kupakia picha ama video za utupu au za mtu mwingine yeyote katika mitandao ya kijamii.

Watoto wanapaswa kufahamu kuwa utunzaji wa muda ni muhimu kwa mafanikio yao. Mfano, ikiwa wana kikao, ama wanapaswa kufika shuleni saa tatu, wafike saa 2:45. Wafanye na kuwasilisha kazi zao kabla ya tarehe ya mwisho, iwe shuleni, nyumbani ama kazini.

Yapo mambo mengi watoto na vijana wanaweza kufanya ili kuwasaidia wengine. Kujitolea kutawapa furaha na kujenga uhusiano mzuri na watu katika jamii na kuwapa fursa ya kujifunza maisha mengine wanayopitia watu tofauti na yake waliyoyazoe.

Pia, kuanzia siku watakapopata shilingi yao ya kwanza, waanze kuweka akiba. Wapange matumizi yao kwa busara. Wasitumie pesa zaidi ya wanayoipata na waweke akiba kila wakati kabla ya kutumia. 

Akiba itawasaidia siku za usoni na kuwafunza kuthamini kipato chao na jitihada za wazazi au walezi wao wanazifanya ili kuhakikisha wao wanapata mahitaji bora na muhimu.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwalea Watoto Wetu Kuwa Wenye Furaha?

Vijana na watoto wafahamu kwamba kuna wakati watashindwa, lakini wajifunze kuinuka haraka na kujifunza kutokana na makosa ili kujaribu kufanya vizuri zaidi wakati mwingine. Kufeli mtihani, kushindwa mashindano, au mechi ni sehemu ya maisha na mchakato wa kujifunza. Cha muhimu ni kujifunza kutokana na makosa na kujaribu kufanya vizuri zaidi.

Wazazi na walezi tunapaswa kuchukua nafasi kuwafundisha vijana wetu mambo haya muhimu. Kwa kufanya hivyo, tutawasaidia kujenga maisha yenye mafanikio na maadili mema. 

Kwa pamoja, tunaweza kuwajenga vijana wetu kuwa raia wema na wanaojitambua!

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Andiko zuri sana, Pia wazazi tunatakiwa kuwa wa mfano katika hayo, watoto wanajifunza kutokana na matendo yetu pia. Mfano hawawezi kuwa wakili wema wa muda au fedha kama sisi pia sio mawakili waaminifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts