The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Jinsi ya Kuwasaidia Watoto Kuepuka Vishawishi vya Makundi-Rika

Je, wazazi na walezi tunaweza kupunguza uwezekano wa mtoto kuharibikiwa kutokana na msukumo wa makundi-rika? Hakika inawezekana!

subscribe to our newsletter!

Watoto katika umri tofauti wa ukuaji wao wanakutana na vishawishi chanya au hasi kutoka kwa marafiki zao, hii huitwa kundi-rika, au peer pressure, kwa kimombo. 

Je, wazazi na walezi tunaweza kupunguza uwezekano wa mtoto kuharibikiwa kutokana na msukumo wa makundi-rika? Hakika inawezekana! Tunaweza kuwasaidia watoto wetu kusema ndiyo kwa vishawishi chanya kutoka makundi-rika na hapana kwa makundi-rika hatarishi au hasi.

Tuwajue marafiki na wote wanaoshinda na watoto wetu, hasa kama hatujakutana nao ana kwa ana. Tufanye jitihada ya kuwafahamu na kwa nini wanampenda, au kumchukia na tujue ni vishawishi gani walivyonavyo kwa watoto wetu. 

Mwoneshe mtoto unajali rafiki zake na namna hii utafungua milango ya urafiki na kuaminiana baina yako na mtoto wako pamoja na marafiki zake. Tusiwe watu wa kuhukumu tabia, bali tuwe washauri.

Tuzungumze na watoto kuhusu tunu. Tuwaambie watoto nini kitu muhimu kwetu, wajue kama tungependa kuona wakifanya vizuri katika masomo yao, wajali na kuwa msaada kwa watu wengine na kutojihusisha na ngono katika umri mdogo. 

SOMA ZAIDI: Mambo Muhimu Wazazi Tunapaswa Kuwafundisha Vijana Wetu

Kuwa muwazi juu ya tunu zako, za familia na za kibinadamu kwa ujumla na kwa nini ni muhimu kuwa nazo ili iwasaidie kufanya maamuzi sahihi.

Kwa wazazi wenye watoto kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi mitano, watoto wakianza kufanya maamuzi yasiyofaa, au kushawishiwa vibaya na makundi rika, tuwaeuepushe kwa kuwapatia kazi au michezo chanya ya kuwapotezea fikra za makundi rika. 

Ukiona hawabadiliki, tuwaeleze kwa ufupi kwa nini maamuzi yao, au vishawishi, ni hatari na kuwapa mbinu mbadala za kufanya maamuzi sahihi. Kwa mfano, tuwaeleze watoto wetu kuwa si tabia nzuri kutumia lugha za matusi, au kupigana na kuoneana, hata kama tumekasirika. Vilevile, tuchunguze ni wapi kajifunza lugha na matendi hayo.

Kwa wazazi mwenye watoto kuanzia umri wa miaka sita hadi tisa, tuwaalike marafiki wa watoto wetu wacheze nao nyumbani kwetu ili tupate fursa ya kujua tabia zao na mambo gani wanashawishiana. 

Kabla ya kufanya hili inabidi wazazi tufahamiane kwanza na kuelezana malengo ya malezi ya watoto wetu ili tuwe na muelekeo sawa. Tuwape watoto muongozo pale utakapoona wanatoka nje ya mstari. 

SOMA ZAIDI: Tufahamu Kuhusu Ukatili Dhidi ya Watoto, Changamoto Zilizopo na Suluhisho

Tuwajue wazazi wao vizuri, yaani tunu zao, pamoja na majirani, watoto na watu wazima, wanaotuzunguka ili kujua kama lipo jambo hatarishi pasi sisi kujua. Tushirikiane na wazazi au majirani wenye maono kama yetu kwani si rahisi kumlea mtoto pekee yako! 

Tunahitaji timu ya marafiki na wazazi wenzetu kukuza watoto wema katika jamii kama wasemavyo wahenga, kidole kimoja hakivunji chawa.

Kwa wazazi wenye watoto wa miaka kumi hadi 15, hapa hatari ya kudumbukia katika vishawishi vya makundi rika ni dhahiri na vigumu kwa mtoto kujiepusha nayo hata kwa yule mwenye uwezo wa kukwepa vishawishi kama hana muingozo wa mzazi tangu akiwa mdogo. 

Sayansi inasema kunauwezekano wa asilimia ndogo ya vijana hawa kuepuka vishawishi kwa jitihada zao wenyewe endapo wameumbwa na nguvu ya kipekee ya kukabiliana na mawimbi ya vishawishi ambayo huitwa resilient trait kwa kimombo.

Umri huu ni changamoto kwa mzazi kumshawishi mtoto kubadilisha maamuzi kwa kuwa kipindi hiki anapata dhana ya kujitegemea hasa kimaamuzi. Ili kuwasaidia watoto wa umri huu, jadili nao kuhusu changamoto za vishawishi wanavyokumbana navyo wawapo shuleni, mtaani na hata mtandaoni.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Watoto Wanapaswa Kufahamu Kuhusu Siku ya Mtoto wa Afrika?

Kuwa mpole na mvumilivu kwa kuwa mtoto wa umri huu mara nyingi hueleza na kufanya mambo pasi na uoga wa matokeo au madhara yake.

Wazazi wenye watoto wa miaka 16-18, umri huu mara nyingi watoto hufikiri wameshakuwa watu wazima vya kutosha kuweza kujisimamia. Hapa makundi-rika humsukuma kutaka kujua pombe ina ladha gani? 

Sigara, bangi na huanza mara nyingi kudadisi mambo kama busu, ngono, na kadhalika. Hapa mtoto anawaamini marafiki zaidi kuliko wazazi kwa kuamini wazazi zama zao zimepitwa na wakati.

Wazazi tunashauriwa kubadili namna ya kuwasiliana, tuwafanye wajisikie kuwa mtu mzima, huku tukiwausia kuzikumbuka tunu na maadili mema. Tujitahidi tusitumie vitisho kama ‘ukichelewa, usiingie kwangu.’ 

Badala yake, tuwe wawazi juu ya tabia zinazokubalika na kuwaonesha mifano ya watoto wema na wenye mafanikio katika jamii.

Tujenge ukaribu na waalimu na majirani ili kuweza kujua tabia zinazojitokeza akiwa nje ya nyumbani. Pia, wazazi tunashauriwa kutoangalia mabaya tu bali kuwasifia watoto pale wanapofanya vizuri ili kuwapa moyo wa kuendelea kutenda mema.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. I’m very happy to discover The Chanzo Initiative, there is a lot to take from you through my carrier to educate remotely society

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts