The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

TCRA: Hatujatoa Tamko au Agizo la Kufungia au Kupiga Marufuku Mtandao Wowote wa Kijamii Tanzania

Mamlaka hiyo imeeleza haya ikijibu barua ya wadau wa Kikundi Kazi Cha Masuala ya Mitandao (IGTWG)

subscribe to our newsletter!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeeleza kuwa haijatoa tamko au agizo lolote  la kufungia au kupiga marufuku mtandao wowote wa kijamii Tanzania.

Mamlaka hiyo imeeleza haya ikijibu barua ya wadau wa Kikundi Kazi Cha Masuala ya Mitandao (IGTWG), wadau  walioomba kikao na Mamlaka hiyo inayohusika na ustawi na uratibu wa mawasiliano Tanzania ili kujadili kwa uwazi baadhi ya misukumo iliyokuwa ikitolewa ya kutaka kufungia mtandao wa kijamii wa X zamani ukijulikana kama Twita.

“TCRA kama taasisi inayosimamia sekta ya mawasiliano haijatoa tamko au muongozo wa kufungia au kupiga marufuku mtandao wowote wa kijamii Tanzania,” imeeleza barua hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA, Dr. Jabir K Bakari.

“TCRA inachukua hatua za kiuratibu pale panapoonekana kuna uvunjifu wa sheria na kanuni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” iliendelea fafanua barua hiyo.

Kikundi Kazi Cha Masuala ya Mitandao kinachoundwa na taasisi mbalimbali zaidi ya ishirini zinazoangalia masuala ya uhuru, haki na wajibu mitandaoni, pamoja na fursa zake kilifikia hatua hiyo ya kuomba kikao kufuatia kampeni iliyoanzishwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, pamoja na baadhi ya viongozi wa dini wakitaka mtandao wa kijamii wa X zamani ukijulikana kama Twita ufungiwe kwa madai kuwa unatumika kusambaza maudhui ya ngono.

Mtandao huo unaotoa fursa mbalimbali za mijadala ikiwemo ajira kwa baadhi ya vijana ni mtandao wenye watumiaji zaidi ya laki 6 nchini Tanzania. Wadau hao waliomba kuwepo na majadiliano ya wazi ili kuweza kupata muafaka, hasa baada ya aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano Nape Nnauye kuandika kuwa wanafuatilia mjadala huo.

Akizungumza baada ya kupokea mrejesho huo, mratibu wa wadau hao Asha D. Abinallah  ambaye pia ni Mkurugenzi wa taasisi ya Tech & Media Convergency (TMC) ameonesha kufurahishwa na mrejesho kutoka TCRA.

“Kwanza nafurahi kwamba Mamlaka wamechukulia kwa umakini hili jambo na wameweza kulijibu, wamewasilisha hoja tatu na hoja ya tatu ilikua ni kupongeza kikosi kazi,” anaeleza Asha akiongea na The Chanzo.

Aliongeza zaidi: “Pamoja na kwamba wao TCRA hawakutoa tamko hilo, lakini walitutia wasiwasi baada ya kufuta akaunti zao ambazo tuling’amua zimefutwa baada ya siku tano au saba toka yale matamko ya wale viongozi wa dini na wale viongozi wa chama cha tawala kutoka. Wao kufuta akaunti zilizokuwa na wafuasi wengi na kubaki katika mitandao mengine ya kijamii ilitupa wasiwasi.”

Wadau wengi wa mawasiliano ikiwemo vyombo vya habari na makampuni ya mawasiliano wameendelea kuonesha kuridhishwa na mwenendo wa taasisi hiyo ambao kwa kiasi kikubwa umejikita katika mashauriano na wadau katika masuala mbalimbali ikiwemo changamoto za kisheria.

Hali hii imeonekana kukua katika miaka ya hivi karibuni,hasa baada ya mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita kubadili mambo na kutaka sekta ya habari na mawasiliano kukua huku misingi ya sheria, maadili na utawala bora ikifuatwa.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts