Ni kama vile kuna makubaliano fulani ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali inayoiongoza kwamba ni mwiko kwa watendaji na maafisa wake waandamizi kuvujisha siri za “ushindi” wa chama hicho tawala nchini wa wagombea wake kwenye chaguzi mbalimbali zinazofanyika nchini kwa ajili ya kupata viongozi wa ngazi mbalimbali.
Na inaonekana pia chama na Serikali inayachukulia kwa umakini mkubwa makubaliano haya kiasi ya kwamba punde tu baada ya afisa, au mtendaji fulani, kuonekana kuyakiuka, utumishi wake hukoma papohapo. Hii imetokea angalau mara mbili ambapo viherehere vya wanasiasa wa CCM vilisaidia kututhibitishia yale ambayo wengi tumekuwa tukiyasema, kwamba hakuna uchaguzi wa huru na haki hapa Tanzania.
Kisa cha hivi karibuni kabisa ni kile kilichomuhusisha Marko Henry Ng’umbi, aliyetumbuliwa kama Mkuu wa Wilaya ya Longido masaa machache baada ya video iliyomuonesha akijisifu kushiriki kwenye kuharibu chaguzi kusambaa mitandaoni. Ng’umbi alikuwa akiwaambia madiwani aliokuwa akiwahutubia kwamba wasidhani walishinda kihalali, bali ni kwa njia haramu za CCM, nyingine zikihusisha mambo yaliyofanyika “maporini” ambayo hakuyaweka wazi.
Kauli ya Ng’umbi ilikuja takriban miezi miwili kabla ya ile ya Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, aliyewaambia wananchi huko Bukoba, mkoani Kagera, kwamba ushindi hautokani na upigaji wa kura, bali unatokana na nani anayehesabu kura na kutangaza matokeo, kauli ambayo wengi wanaihusisha na kutenguliwa kwake kama Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Ng’umbi na Nnauye wote ni wateuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan, na lazima nikiri kwamba inatia moyo kumuona kiongozi huyo mkuu wa nchi akichukua hatua zinazoashiria, angalau kwa baadhi yetu, ingawaje ni ngumu sana kujua maamuzi yake yanasukumwa na nini haswa, kutokufurahishwa kwake na majivuno hayo ya wasaidizi wake.
Kauli hatari
Kauli kama hizi ni za hatari sana kwani zinawasukuma watu wasiwe na imani na michakato ya kidemokrasia, kama vile chaguzi, na hivyo kuwafanya wananchi wengi zaidi wasione mantiki ya kujitokeza na kupiga kura. Hatua hiyo inaweza kuwa na madhara mengi kwa nchi, yale ya muda mfupi na yale ya muda mrefu.
SOMA ZAIDI: CCM Hawako Tayari kwa Mageuzi Lakini Suluhu Siyo Kususia Uchaguzi
Madhara ya muda mfupi ni kwamba unapokuwa na watu wachache zaidi wanajitokeza kupiga kura, huku wengi wakiisusia michakato hiyo, Serikali yoyote itakayoundwa kutoka kwenye michakato hiyo itakosa uhalali utakaoiwezesha kutekeleza sera na maamuzi mbalimbali. Maana demokrasia ni utawala wa wengi, sasa uhalali unaotolea wapi pale wengi wanapogoma kushiriki kwenye michakato hiyo?
Na pale unapokuwa na watu wengi zaidi ambao hawana imani na michakato ya kidemokrasia unakuwa unatengeneza tatizo kubwa, na la muda mrefu, ambalo ni lile linalohusu ulinzi na usalama wa nchi. Watu wanaposhawishika kwamba kura zao si chochote, si lolote wanaweza kulazimika kutafuta mbinu zingine mbadala za kuelezea ukinzani wao dhidi ya Serikali iliyopo madarakani, ikiwemo kujihusisha na vitendo vya kigaidi, na kadhalika.
Ni kwa msingi huu ndiyo naipongeza hatua ya Rais Samia ya kuwaondoa kutoka kwenye nafasi za uongozi wateule wake wanaotoa kauli zinazotishia kulipeleka taifa kwenye mwelekeo huo. Hatua hiyo inatuma ujumbe kwamba hayuko tayari kuwa na wasaidizi walio tayari kufanya vitendo vya kiharamia, na kuwa na ujasiri wa kujivunia hadharani vitendo hivyo.
Hatua za ziada
Lakini pia ningependa kumsihi Rais asiishie tu kwenye kukerwa na watu wanaojivunia kunajisi michakato ya kidemokrasia na kwenda mbele zaidi kwa kujenga taasisi imara zitakazozuia vitendo hivyo kufanyika na hivyo kufanikisha chaguzi huru na za haki hapa nchini kwetu.
Maana ukweli ni kwamba wanasiasa hawa hawajasema uongo, wamethibitisha tu kile wadau wengi, wakiwemo vyama vya upinzani, asasi za kiraia, na waangalizi huru wa uchaguzi, wamekuwa wakikilamikia mara kwa mara, kwamba CCM, kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, imekuwa ikiingilia michakato hiyo kwa upendeleo wa wagombea wake, ikiwemo hata kuwaengua wagombea wa upinzani kwa sababu zisizoeleweka, na hivyo wagombea wao kupita bila kupingwa.
SOMA ZAIDI: Mwenezi Khamis Mbeto: CCM Ndiyo Baba wa Demokrasia Tanzania
Rais Samia ana wajibu wa kuzuia hili pia lisitokee kwa kutekeleza mapendekezo ambayo wadau kadhaa wa demokrasia na uchaguzi wamekuwa wakiyatoa kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na imani na michakato hii na kupunguza uwezekano wa CCM, na vyombo vya dola, kuiingilia na kuinajisi na hivyo kuiondolea uhalali wake.
Kuna mengi Rais Samia anaweza kufanya, kama ambavyo wadau wameshabainisha tayari, lakini angalau kwa sasa anaweza kuzuia hili la TAMISEMI kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hapo Novemba, na kuiruhusu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kusimamia michakato hiyo kama sheria inavyoelekeza.
Rais pia anaweza kuharakisha utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwani hatua hiyo inaweza kuleta mageuzi kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na kudhibiti nafasi zao kwenye chaguzi. Pia, Rais anaweza kufikiria kufufua mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya, mchakato ambao wengi wanaamini inaweza kutoa majibu ya changamoto nyingi za kiuchaguzi zinazoikabili Tanzania.
Ni muhimu kwa Rais Samia kufanya hivyo kama kweli anataka tumuamini kwamba amedhamiria kuhakisha uhuru na haki kwenye michakato ya uchaguzi. Kutumbua wateule wake wanaojisifu kunajisi chaguzi tu hakutakuwa na faida kubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla kama hatua hiyo haitaambatana na hatua zingine zinazolenga kujenga taasisi imara ya kidemokrasia na kiuwajibikaji.
Ukweli ni kwamba, kama hilo halitafanyika, kutumbuliwa kwa wanaojisifu kunajisi chaguzi kutakuwa na faida hasi kwa wananchi, na taifa zima, kwani kutawafanya watendaji na maafisa wengi ndani ya CCM na Serikali kuacha kufichua ukweli huo mchungu, na matokeo yake ni kwamba mnufaika mkubwa wa hatua hiyo itakuwa ni CCM na Serikali yake ambayo inaonekana kuwa tayari kutumia madhaifu ya kitaasisi yaliyopo nchini kutimiza azma yake ya kubaki madarakani.
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.