The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mwenezi Khamis Mbeto: CCM Ndiyo Baba wa Demokrasia Tanzania

Asema nia ya CCM ni kutokomeza siasa za chuki Tanzania.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Idara ya Itikadi na Uenezi – Zanzibar Khamis Mbeto Khamis amesema kwamba sababu ya chama hicho tawala nchini kutafuta maridhiano na vyama vya upinzani ni kwa sababu ya hadhi iliyonayo kama baba wa demokrasia Tanzania.

Mbeto alitoa tathmini hiyo wakati wa mahojiano maalum na mwandishi wa The Chanzo Khalifa Said yaliyofanyika Machi 15, 2023, pale kada huyo alipotembelea ofisi za chombo hicho cha habari zilizopo Msasani, Dar es Salaam. 

“CCM ni baba wa demokrasia na sisi tunaamini kwenye siasa za maridhiano, [kwamba] ndiyo siasa pekee zinaweza kuisaidia Zanzibari kwa leo,” alisema Mbeto kwenye mahojiano hayo. “Tutoke kule kwenye siasa za chuki.”

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo na hapa Mbeto anaanza kwa kuelezea historia fupi ya maisha yake ya kisiasa ndani ya CCM:

Khamis Mbeto Khamis: Majina yangu, kama ulivyotangulia kusema, naitwa Khamis Mbeto Khamis. Nimezaliwa [mwaka] 1977 katika wilaya ya Wete, mkoa wa Kaskazini Pemba. Na nimesoma Shule ya Msingi Kisiwandui, kipindi kile kulikuwa na uhamisho wa wazee wetu kufanya kazi kutoka Pemba kuja Unguja na kutoka Unguja kuja Pemba. Mimi nikabahatika kuzaliwa katika kisiwa cha Pemba. Lakini baadaye nikarudi nikaanza Shule ya Msingi Kisiwandui.

Nakumbuka ilikuwa mwaka 1983 nikaanza pale, nikasoma. Wakati nasoma shule ya msingi, nikasoma shule tofauti. Unajua wazee wako wakiwa watumishi wa Serikali wanahamishwa, lakini nikasoma baadaye sekondari nikarudi  tena Pemba nikasoma Utaani, nikaja kumalizia Tumekuja. Nikasoma Taasisi ya Kiswahili lakini pia nikajiunga na chuo, nikasoma IPS, mambo ya manunuzi.

Nilipomaliza pale, nikasoma masomo mbalimbali mengine lakini wakati kipindi hicho – maana unataka historia ya kisiasa – wakati tunasoma mwaka 1994, vuguvugu la vyama vingi linaanza, wakati wa Dk Salmin [Amour, Rais wa Zanzibar], kuliibuka lile vuguvugu la maskani, kama unakumbuka, sisi ni miongoni mwa waanzilishi pale Zanzibar eneo moja pale sehemu ya Miembeni, inaitwa Sokita Masika. 

Mimi nilikuwa katibu wa vijana kipindi hicho, zamani kabisa, baadaye nikaendelea, unajua sisi ni kizazi cha mwisho, wazee wetu ni watu wazima ambao ndiyo walioanzisha ASP na CCM huko, sasa mzee wangu alikuwa pia ni balozi.

Sasa wakati mimi nasoma, huku nafanya kazi za mzee, zile za ubalozi, unajua, baadaye tukaenda nikawa ni balozi sasa wa shina, nimekaa kama balozi wa shina kama miaka kumi na tano. Sikuja tu nikawa Mjumbe wa Halmashuari ya Taifa [ya CCM]. Nilikaa nikawa balozi, nikawa Mjumbe wa Halmashauri ya Tawi, Mjumbe wa Halmashauri ya Kata, Mjumbe wa Halmashauri ya Jimbo, wilaya, mpaka mkoa, mpaka nikawa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.

Na hiki ni kipindi cha pili nakuwa Mjumbe wa Halmashauri ya Taifa na katika kipindi changu cha mwanzo nilibahatika, kama kada, kupata mafunzo maalumu. Nilibahatika kwenda China kwenda kusoma masuala ya siasa, uongozi na itikadi na mambo mbalimbali. Lakini pia nilipata nafasi kwenda tena Afrika Kusini, nilipata mwaliko wa [chama cha] ANC kwenda kupata mafunzo mbalimbali  ya chama. 

Kwa hiyo, chama nakijua. Nimeanza nacho mbali mpaka hapa nilipofikia. Lakini pia nimewahi kufanya kazi mbalimbali za Serikali, niliteuliwa kuwa ni Kamishna wa Bodi ya Utalii, imenipa fursa ya kutembea nchi nyingi tu duniani, kama miezi sita nyuma nilikuwa niko Italy kwenye jukwaa la uwekezaji na Uholanzi sasa.

Baadaye sasa, baada tena, unajua chama kila baada ya miaka mitano kunakuwa na chaguzi za chama. Baadaye tena nikagombea tena Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, nikachaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.

Baadaye, Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi [Dk Hussein Ali Mwinyi] basi akaniteua nimsadie katika Idara ya Itikadi na Uenezi kule Zanzibar, ambayo ndiyo nafasi ambayo naendelea nayo mpaka sasa hivi.

The Chanzo: Tunashukuru sana. Kwa hiyo, hukuibuka tu kama ambavyo umezungumza wewe mwenyewe. Unajua mimi pia nimesoma Wete?

Khamis Mbeto Khamis: Wete ipi? 

The Chanzo: Utaani.

Khamis Mbeto Khamis: Na mimi nimesoma Utaani lakini mimi ni mkubwa zaidi. Nakumbuka nasoma ilikuwa [mwaka] 1994, kama hivyo. Kabla ya uchaguzi [wa 1995], baada sasa ya lile vuguvugu kidato cha kwanza linakua, unajua siasa za mwanzo zilikuja na kasi kipindi kile cha [Benerd] Mapalala. [Baba] akasema hapana, Serikali mimi ndiyo imenileta huku basi akaturejesha Unguja nyumbani ili kuendelea na masomo yetu ilikuwa 1993 au 1994.

The Chanzo: Sawa sawa, asante sana.

Khamis Mbeto Khamis: Mimi nimesoma Shule ya Sekondari Kizimbani pia, na kumaliza Darasa la Nane, tumewahi kumaliza Darasa la Nane, mimi nilifanya mtihani pale Kizimbani pale, kuingia sekondari tukaja zetu Utaani.

The Chanzo: [Mwaka] 1994 mimi nilikuwa na miaka miwili, sawa. Asante sana kwa utambulisho huo hapo. Mtazamaji, Komredi Mbeto hapa, hivi karibuni tulimuona akishiriki kwenye mkutano wa chama cha upinzani ambacho ni chama cha ACT Wazalendo. Bila shaka chama mshirika pia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na ulikuwa umevalia sare zako pia za Chama cha Mapinduzi na kwenye macho ya baadhi yetu kile hakikuwa kitu cha kawaida, siyo kuvaa nguo, namanisha kwa kada mwandamizi wa Chama cha Mapinduzi kuhudhuria kwenye mkutano, ACT walikuwa wanazindua ‘Brand Promise’ yao pale [Hotel] Verde na wewe ukahudhuria. Ile hatua ilishajihishwa na nini, nini kilikusukuma ukasema kwamba inabidi niwepo kwenye huu mkutano?

Khamis Mbeto Khamis: Kwanza, CCM ni baba wa demokrasia na sisi tunaamini kwenye siasa za maridhiano, [kwamba] ndiyo siasa pekee zinazoweza kuisaidia Zanzibari kwa leo. Tutoke kule kwenye siasa za chuki. Bado miongoni mwetu viongozi wa siasa tuna viashiria vya chuki kwa sababu ukiangalia historia zetu sote sisi ni ndugu, tunakutana pahala moja ama pengine.

Sasa ndani ya CCM tunaamini maridhiano ni jambo pekee ambalo linaweza kusaidia Tanzania na Wazanzibari kwa ujumla. Sisi tulipata mwaliko kama chama cha siasa, kama walivyovialika vyama vingine, lakini wewe unajua kwa CCM kuhudhuria kwenye jukwaa kama ile inakuwa ni ngumu. 

Mimi nikajitolea, nikawambia wakubwa zangu bwana mimi nitaenda pale kama kukiwakilisha chama, na nilikwenda pale kama mlivyoona, nikapeperusha bendera, na kila kitu. 

Sasa yaliyotokea pale ndiyo ukomavu. Unajua CCM, imekomaa kwenye siasa na bahati nzuri sasa mimi nilianza, kiongozi wangu, Mwenyekiti wangu [taifa, Rais Samia Suluhu Hassan] akaja akafuatia, tulimuona kwenye mkutano wa BAWACHA katika CHADEMA. 

Maana yake nini? Sisi tunapeleka ujumbe kwamba siasa si uadui, siasa si kukashifiana, kutoleana matusi, kashfa ambazo hazina maana. Tujenge nchi, tushindane kwa hoja, na ukizingatia, wewe umesema, kwamba Zanzibar tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa, tunaita SUK. 

Serikali ile haikuja kwa matakwa ya mtu tu, ile Serikali imefanywa kikatiba kabisa. Unakumbuka kulikuwa na mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar, mabadiliko ya 10, ndiyo ikaruhusu sasa kwamba tuwe na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. 

Maana yake ni  nini? Chama kitakachoongoza kwa kura za Urais na kura za majimboni kitaunda Serikali. Kwa maana kitatoa Rais na Makamu wa Pili wa Rais. Chama kinachofuata kwa kura kitatoa Makamu wa Kwanza wa Rais. 

Lakini uwiano wa mgawanyo wa nafasi mbalimbali za mawaziri itategemea namba ya majimbo ambayo yaliyopatikana kwenye ule uchaguzi na ndiyo maana tumeenda kwenye uchaguzi, tumemaliza, Serikali imeundwa ina sura ya Umoja wa Kitaifa ambayo inaendelea. Kwa maana hiyo, kitendo changu cha kuhudhuria pale kama CCM ni mlezi kwa kwa vyama vyote.

Kwa sababu CCM ni chama kikubwa ambacho kinasimamia demokrasia ya nchi hii na kina wajibu [wa] kuwalea na kuwafundisha siasa hivi vyama vingine kwamba siasa si chuki, ugomvi, si kudogoana. 

Mnaweza mkafanya siasa kwa njia ya amani tu na mkawa mnashindana kwa hoja, mimi nitasema hili, kesho wewe njoo utoe ufafanuzi kwa uzuri zaidi ili kuipinga hoja yangu. Na huko ndiko CCM tunataka tuelekee. 

Maana yake tumesema, sisi kama CCM tunajiangalia kama kioo, tunauchukulia upinzani si kama maadui, ni kama kioo, [kinachotusaidia] kujiangalia na kujitathimini.

The Chanzo: Umezungumza vizuri sana kuhusiana na umuhimu wa maridhiano, kuondokana na siasa za chuki, na namna CCM mnavyoitumia upinzani kama kioo. Na nilikuwa nataka kufahamu kutoka kwako ni kwa kiwango gani hayo mawazo ambayo wewe unayaamini yamekita mizizi ndani ya Chama cha Mapinduzi?  Na nakuuliza hivi kwa sababu umemzungumzia Mwenyekiti wa taifa wa CCM Mama Samia Suluhu Hassan alipokuwa kule kwenye mkutano wa BAWACHA alizungumza kwamba hata yeye ndani ya chama chake alipowauliza baadhi yao kwamba nataka niruhusu mikutano hadhara ya vyama vya upinzani kuna – kwa kutumia neno lake – kuna wahafidhina fulani walikuwa hawafurahishwi na hilo.  Unadhani ndani ya CCM,  kwa mfano, hayo mawazo yako uliyonayo yametawala kiasi gani?  Ni kwa asilimia ngapi watu ndani ya CCM wanayaamini na kuyakubali?

Khamis Mbeto Khamis: Unajua wako watu tofauti, wanaamini siasa zile za matusi, za kugombana, kubaguana, ndiyo tija. Wengine wanaishi, ndiyo mitaji yao. Lakini, ukiangalia sura sasa ya Chama cha Mapinduzi, viongozi wakuu wenyewe hawataki siasa hizo. Na kwa kweli siasa hizo zimeshapitwa na wakati. Watanzania ndiyo sisi sisi. Kila ukiona kila chama kina lengo la kumnufaisha Mtanzania na Mzanzibari.

Wewe umesema ulihudhuria uzinduzi wa ‘Brand Promise’ ile  wanaita, kushafahamu, japokuwa wamenakili mambo ya Dubai wakaonesha pale maghorofa na nini, wakati tukichukulia, zile nchi hazikuendelea kwa miaka ishirini au thelathini, wamechukua takribani miaka mia ndiyo wamefikia pale, lakini katika kufanya siasa wameonesha pale kwamba sisi tukipata tutafanya hivi.

Ni vizuri lakini sisi tayari tunao mkataba huu, ilani ya Chama cha Mapinduzi. Yale waliyoyasema [ACT-Wazalendo] yote yamo [kwenye ilani ya CCM] na ndiyo maana unaona CCM inajenga mabarabara, inajenga shule za ghorofa nchi nzima, inajenga vituo vya afya, inatoa maboti ya kisasa, inafanya mambo mengi kabisa kwa sababu ndiyo mkataba baina ya sisi [na] wananchi [unavyotaka].

Kwa maana hiyo, wako watu ndani ya Chama cha Mapinduzi wanatamani turudi tulipotoka, tuumizane, tupigane mabomu. Ile sasa hivi haipo na ndiyo maana watu hao wapo kwenye CCM na wapo kwenye ACT Wazalendo. 

Bahati nzuri mimi, nikupe siri tu, nusu ya viongozi wa ACT Wazalendo ni wenzangu, kwa sasa sisi ni Wazanzibari. Tumesoma, tumecheza pamoja. Sasa ifike pahala kwamba kuwa mimi CCM si adui, ukanivunjia heshima yangu, wala kuwa wewe ACT Wazalendo au CHADEMA au chama kingine chochote si uadui. 

Tushindane kwa hoja mwisho wa siku matokeo itakayotoka inayomnufaisha Mtanzania. Kwa maana hiyo, sisi tunaamini CCM kwamba tunaweza tukafanya siasa za kistarabu bila kuwatukana watu [na] bila kuwavunjia watu heshima. 

Na nakwambia tatizo hili tunalo ndani ya ACT Wazalendo, mnao viongozi wenu waandamizi wakipanda kwenye jukwaa lazima amseme mtu, lazima aseme mtu. Sasa mimi naona siasa hizo zimepitwa na wakati. Sema hoja, mimi nimetoa hoja, wewe ile hoja yangu ijibu tu, na mimi nikisikia nitaijibu tu na hizo ndiyo siasa za wenzetu sasa hivi huko duniani wanavyokwenda.

Sasa, kwa kweli, tuna kazi ya kuelimisha na kupitia vyombo vya habari – nyinyi sasa – ndiyo tusaidiane kuwaelimisha watu kwamba siasa ni kujenga hoja tu na unaweza ukatoa maoni yako vizuri tu bila kumtaja mtu, wala ukamsukuma mtu [na] ukamdhalilisha mtu. 

Kwa sababu leo mimi ni kiongozi wa kisiasa lakini mimi nina familia, leo nina familia Unguja nzima, Unguja na Pemba, ushafahamu? Mimi nimelelewa na mama yangu yuko Pemba, Shumba Mjini kule, kwetu, ushanifahamu? 

Sasa [Pemba] kwetu [mimi], tuna nyumba Chasasa [Wete], kushanifahamu? Ukinidhalilisha kuna jamaa zangu kule, ushanifahamu bwana? Watakupenda. Wewe nizungumzie kile ninachokizungumza mimi kitolee maelezo zaidi lakini si kunidhalilisha mimi. Maana mimi nasimamia sera ya chama changu na wewe unasimamia sera ya chama chako, haina maana sera zetu tunazosimamia tuvunjiane heshima.

The Chanzo: Umezungumzia kwamba wanaweza wakawepo, kwenye vyama vyote, watu ambao wao wangependa kuona siasa za chuki zikiendelea na vitu kama hivo lakini, kwa mfano, tukibaki ndani ya CCM, kwa sababu wewe ni msemaji wa CCM, sidhani kwamba watu, au viongozi waandamizi wa CCM, hususani Mwenyekiti wa taifa Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi ni miongoni mwa watu hao, sivyo?

Khamis Mbeto Khamis: Hao siyo na ndiyo maana ukaniona nipo hapa na ukaniona nimeenda kwenye mikutano wa ACT Wazalendo na ndiyo maana ukamuona Mwenyekiti ameenda kwenye mkutano wa CHADEMA. 

Maana mimi ninapokwenda pahala, mimi ni kiongozi mwandamizi wa chama, ujue nimepata baraka zote za chama kabisa kuhudhuria kwenye lile eneo. 

Sasa wao wenyewe wanapenda kuendesha siasa ambazo ni za kistarabu basi. Lakini wapo wahafidhina washazoea siasa zile za kufukuzana, kudogoana, kutengana na kubaguana. 

Kuna vyama vingine hata wewe ukienda wanakuona siye tu, hata kama uwe vipi. Na kuna watu wengine vilevile wa vyama vingine wanakuona vilevile siye kutokana na zile siasa za chuki. 

Zanzibar ndiyo maana tumefanya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuondoa hizi za chuki kabisa, yaani mtu kuwa CCM anakuona kama shetani, au mtu kuwa ACT unamuona kama sijui dudu gani sijui, wakati ndiyo hao tumesoma shule ya msingi, sekondari tunakutana kwenye shughuli, maziko, tunaoleana.

The Chanzo: Sasa mtu, unajua, anaweza akijiuliza swali, kwa mfano, unajua kama mimi najiuliza swali kama hivyo ndivyo, unaielezea vipi sasa hatua ya Dk Mwinyi, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa [CCM] Zanzibar kumrejesha Idarous Faina kama Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, [mtu] ambaye, kusema kweli, chama mwenzenu kinachounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa haikufurahishwa kabisa ambapo wao wanadhani kwamba inaenda kinyume na hiyo spirit ya maridhiano. Hilo unalizungumzia vipi, unazungumzia vipi kwamba tumekubaliana kwamba siasa za chuki siyo nzuri, maridhiano ni muhimu, lakini wakati huohuo mtu ambaye chama mshirika wa Serikali hakimkubali, hakimuafiki, kwamba wanamhusisha na kile kilichotokea kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, anarudi kwenye wadhifa wake uleule. Hili unalielezea vipi?

Khamis Mbeto Khamis: Mimi kwanza nikufahamishe kwamba Idarous Faina alikuwa Mkurugenzi wa Tume kabla Dk Hussein hajawa Rais. Lakini ikumbukwe kwamba kuna mamlaka ambayo Rais wa Zanzibar anafanya kazi anaongozwa na Katiba ya nchi, sasa kama Katiba ya nchi imempa ruhsa ya kumteua mtu yeyote, hata wewe anaweza akakuteua kwa sifa zako ukamsaidia kwenye eneo fulani, hilo la kwanza. 

Lakini la pili, hivi unatarajia mtu ambaye ni mshindani wako, ushafahamu, akalalamika juu ya mtu fulani, kwa nini unalalamika juu ya mtu fulani, iwapo ingetokea labda Rais angemteua labda [Ismail] Jussa kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, hivi wao wangesemaje, au CCM wangesemaje? 

Sasa hayo yanasemwa lakini kiongozi ukishateuliwa anapimwa kwa kazi zake, maana mkurugenzi wa tume anaongozwa kwa sheria na taratibu, na kuna makamisaa wale, haongozi tume peke yake.

Lakini  kwa kiasi kikubwa unapokwenda kwenye uchaguzi hakuna mtu anakubali kushindwa. Kila siku ukishindwa utakuja na sababu, sababu siyo mtu. Kama tumekwenda kwenye uandikishaji wa daftari, daftari sote tumelikagua, tukasema daftali hili liko sawa, watu wakaenda kwenye uchaguzi, orodha ile ni sawa, wakapiga kura. Sasa ukiniambia Faina kaharibu wapi mimi sijui. Na hakuna kitu kibaya kama kuingia kwenye mamlaka ya Rais.

The Chanzo: Unajua hapa tunajadili, wewe umezungumza vizuri kabisa, umeweka msingi mzuri kwamba ni muda sasa tukaachana na siasa za chuki, maridhiano, na vitu … 

Khamis Mbeto Khamis: Kwa nini wamchukue Faina sasa, kafanya nini?

The Chanzo: Ni kwamba wanamhusisha na uharibifu [wa uchaguzi], wanavyosema wao.

Khamis Mbeto Khamis: Wanavyosema wao, wewe hujathubitisha? 

The Chanzo: Sijathibitisha kabisa lakini ni muhimu kwa sababu hawa ni chama kikuu cha upinzani na ni washirika wenu kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, yaani siyo chama tu cha kawaida, ni chama kikuu cha upinzani chenye wafuasi wengi, lakini pia na ni mshirika wenu kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Na umezungumza kuwa Rais ana mamlaka, ni kweli, lakini Komredi wewe unafahamu kabisa kwamba Faina siyo tu mtu yeyote, ni mtu ambaye alikuwepo kwenye Tume ya Uchaguzi na kilichotokea wenzenu ndani ya ACT Wazalendo wanakihusisha na yeye. Sasa hiyo, najiuliza, unaielezea vipi hiyo ndani ya muktadha wa maridhiano?

Khamis Mbeto Khamis: Na ndiyo maana nikakwambia kwamba Faina ni mtumishi wa umma, kuhamishiwa kwenye taasisi yeyote ya kiserikali ni jambo la kawaida. Uchaguzi ni mifumo, Faina hapigi kura zote yeye peke yake, ni mifumo. 

Sasa wao wenzetu, kama wanahisi kuna mifumo ya tume ya uchaguzi haiko wazi, hayo wapeleke malalamiko, na ndiyo maana tuna kitu kinaitwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ambapo yeye ndiyo mwamuzi wa kuangalia mchezo wa haki kwenye siasa. 

Sasa  Rais ana mamlaka ya kumteua mtu, huwezi wewe ukamwambia hapana akiwekwa huyu mimi sishindwi. Hivi kuna mtu anataka kushindwa? Nikuulize wewe, kila siku unataka TV yako chaneli hii [ya The Chanzo] iwe juu sawa, akitokea mtu ukahisi kama anakuletea ushindani utamtengenezea maneno tu. 

Na ndiyo maana wazee wanasema ukitaka kumuua mbwa, mpe jina baya, lakini nchi na taasisi zinaongozwa kwa sheria na taratibu. Sasa kama wanaona Faina kavunja taratibu, waseme taratibu ipi, hilo la kwanza.

Lakini umesema hawa ni wenzetu, tunashirikiana katika kuongoza Serikali na ndiyo maana kila Waziri, Makamu wa Rais ana mamlaka anafanya shuguli zake kama kawaida. 

Sasa kungelikuwa kuna sheria imesema mkurugenzi wa tume kuna moja, mbili, tatu sifa hizi ndiyo za mkurugenzi hapo ungesema hapana, Rais kakiuka taratibu. Sasa masuala ya wao kuhisi kama yule ni tatizo mimi nadhani siyo tatizo. Leo watasema mkurugenzi Faina, kesho watasema labda taasisi za muungano tatizo, yaani vyombo vyetu, tatizo, wakati na wao ni raia wana haki ya kupiga kura.

Sasa haya mambo tuyaache kwa sababu unapofika utaratibu watu wanakaa wanaorodhesha yale malalamiko yao, na ushahidi kabisa watu wanalalamika na ushahidi kabisa. 

Kwa mfano, tulifanya uchaguzi mdogo wa Pemba kule jimbo la Konde, wenzetu wakasema kuna mapungufu yamejitokeza, tazama uungwana wa CCM, wakayachukua, wakayaweka vizuri, wakayapeleka kwa mwenyekiti wetu wa taifa, Dk Samia Suluhu Hassan, basi walipopeleka, na wakapeleka kwenye tume inayosimamia hicho kitu, basi umeona maamuzi.

The Chanzo: Lakini kwa nini CCM Zanzibar mkasubiri mpaka haya malalamiko yamefikishwa kwa Mwenyekiti wa taifa wakati nyinyi mpo pale?

Khamis Mbeto Khamis: CCM sisi hatusimamii uchaguzi, CCM sisi ni chama cha kisiasa, wanaosimamia uchaguzi [ni tume], ipo kikatiba, kisheria. Wao ndiyo wanasimamia uchaguzi, siyo sisi. Hata sisi tunalalamika kwenye uchaguzi, au hujawahi kusikia CCM inalalamika? 

Tunalalamika chaguzi ngapi Pemba? Tunalalamika. Lakini tunapolalamika, tume inaanglia je, malalamiko wanayoleta CCM ni ya msingi? Malalamiko mangapi yanatupiliwa mbali, Pemba? Hivi nikuulize wewe, hivi Pemba hakuna wana-CCM? 

The Chanzo: Wapo.

Khamis Mbeto Khamis: Mbona nyuma hata CCM ikikishindwa tunaaminishwa kwamba CCM Pemba haiwezi kushinda,  ama haipati kura, huo ni ukweli? Mbona kule hawalalamiki? Lakini ikitokea Unguja, wanalalamika. Sasa ndiyo kazi ya vyama siasa. Chama cha siasa chochote kina malengo ya kupata na kufanikiwa.

Sasa kama anaona pahali hajafanikiwa analalamika, hata CCM na sisi tunalalamika kwa Pemba. Lakini mengine tunasikilizwa, mengine hatusikilizwi. Sasa kwenye suala hilo la demokrasia viko vyombo vinasimamia, nilikutajia wapo hao nani, hao Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini ziko tume huru zinafanya kazi zao kwenye masuala ya uchaguzi.

The Chanzo: Labda tukiwa tunajaribu kumalizia malizia, pale mwanzoni kabisa ulizungumzia suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Nilikuwa nataka kupata tathimini yako, unautathimini vipi muelekeo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa pale Zanzibar.

Khamis Mbeto Khamis: Mimi kwanza suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa, nimekwambia mwanzo, ni suala la kikatiba, siyo la mtu. Na Serikali ya Umoja wa Kitaifa haijafungwa kwa CCM na ACT Wazalendo tu, chama chochote kitakachopata wingi wa kura – inaweza ikaja CUF, inaweza kuja CHADEMA, inaweza ikaja SAU, CHAUMA – chama chochote kile kwa sababu lile ni suala la kikatiba. 

Sasa, mpaka sasa hivi tunaendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa na sisi tunaheshimu kwa sababu jambo lipo kwenye Katiba. Na sisi CCM kila siku tuko wazi tunasema kwamba kama kuna jambo ambalo wenzetu wanahisi, maana ile Serikali kwa sasa inaongozwa na CCM na ACT,  basi waje kwenye chama watuambie kwamba jamani sisi tunahisi moja, mbili, tatu basi tutayatazama tukihisi yana msingi tutakwambia wenzetu jamani kwenye hili basi wenzetu wanakuja kutulalamikia. Lakini wewe unatoka unaenda kusimama kwenye majukwaa ya kisiasa, unatukana, unashtumu.

The Chanzo: Sisi The Chanzo hapa tumejaribu kuongea na wananchi, baadhi ya wananchi wa Zanzibar kuhusiana na tathimini yao ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na moja kati ya suala kubwa lililoibuliwa na wao ni kwamba wanadhani kuna haja ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kufikishwa mpaka ngazi ya chini, isiwe katika ngazi tu ya kitaifa, kwamba mawaziri, mpaka huku ngazi ya chini kwenye mikoa, au ngazi ya shehia. Hilo kwenye CCM labda mnalitafakari, mnaliona pia?

Khamis Mbeto Khamis: Mimi nadhani hakuna jambo ambalo halizungumziki. Ndiyo maana nakwambia jambo lolote kukaa mezani, mkajenga hoja, mkazungumza tu, hivi leo ulitarajia wewe Zanzibar kutakuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwa CCM ilivyokuwa? Mbona imekuwa, tumepiga kura za maoni, tumekuwa. 

Mimi nakwambia jambo lolote mnapokaa mezani, lakini pia unapokuwa na heshima ya kuomba jambo kwa utaratibu, yanazungumzika tu, hakuna jambo hata moja [ambalo haliwezekani] kwa sababu sote tunafanya jambo mwisho wa siku Mzanzibari ndiyo afaidike.

Haya mambo yanatekelezeka tu lakini, lazima mkae mzungumze, mpange, mheshimu mamlaka, muende kwa lugha nzuri, msiwe mnaomba jambo kwenye viriri, siyo utaratibu.

Mfano mimi nimekuja hapa kwenye studio yako, tuko ndani tunafanya mahojiano vizuri kabisa, sasa leo hata ukiniomba jambo kwamba mwenezi nina tatizo labda la taasisi fulani niombee wewe ndiyo mwajiri, nitakuombea, lakini ungenirusha tu kwenye vyombo vya habari bwana mwenezi kitu fulani, haiwezekani. 

Sasa mimi nadhani hakuna jambo ambalo halizungumziki, kwenye masuala ya kuwahudumia watu. Kila kitu kinazungumzwa. CCM wao hawana shida na kuzungumza na mtu yeyote kabisa. 

Ndiyo maana nikakwambia tumekutana na CHADEMA, kwa mfano, Mama [Samia] ameunda Kikosi Kazi, sawa? Kimeratibu maoni, kimechukua, akayasikiliza, sawa? Yamesikilizwa. Ndiyo maana leo unaona tuna mikutano ya hadhara. 

Mwanzo ilizuiliwa wakamuomba wanataka Katiba Mpya, Mama akasema sawa, tutalifanyia kazi. Kuna mambo, hata Dk Mwinyi alisema, kuna mambo ya muda mfupi, muda wakati na muda mrefu. Tunahitaji uwanja mpana tuzungumze, tuweke maslahi mbele ya taifa, yote yanazungumzika.

The Chanzo: Ni mapendekezo gani Dk Mwinyi ameyatekeleza kutoka kwenye kile Kikosi Kazi chake?

Khamis Mbeto Khamis: Likiwemo moja hilo la vyama, mikutano ya hadhara kwa sababu ufahamu chama kinakuwa cha kitaifa, unaporuhusu, Rais wa Jamhuri ya Muungano anaporuhusu shughuli za kisiasa zifanyike moja kwa moja anashauriana na Rais wa Zanzibar kwa sababu hakuna chama kiko [Tanzania] Bara tu, watafanya shughuli zao Bara [na Zanzibar]. 

Ukiona jambo limefanyika Tanzania, ujue na Dk Mwinyi kwa kule Zanzibar amebariki, amezungumza na Mwenyekiti wake wakaona kuna haja turuhusu na ndiyo hilo moja pia faida.

The Chanzo: Lipo jingine lolote ambalo hatulifahamu?

Khamis Mbeto Khamis: Yapo mengi tu, kwa mfano, kulikuwa na makesi mbalimbali ya wanasiasa yamefutwa. Wewe unajua, unashanifahamu, sasa kuna mambo mengi kabisa ndiyo maana amesema kuna ya muda mrefu na kuda mfupi kabisa.

The Chanzo: Sawa sawa. Komredi Mbeto mimi nakushukuru sana, ulikuwa ni wasaa mzuri sana wa kuzungumza na wewe. Labda kwa sababu tulianza na wewe binafsi, labda pengine tukiwa tunamalizia turudi kwako wewe binafsi, labda unaweza kuwashirikisha watazamaji wetu ni funzo gani kubwa ambalo wewe umelipata kwenye maisha yako yote haya na harakati zako zote za kisiasa? Nadhani itakuwa sehemu nzuri ya kufungia mahojiano yetu.

Khamis Mbeto Khamis: Mimi nadhani kwenye masuala ya siasa, kwenye maisha yote, ni ustahimilivu. Ustahimilivu kwa sababu siyo wote wanakutakia mafanikio, sawa? 

Kila siku  kuna mtu anataka akuone uko hatua ile ile, sasa unapopanda hatua, unapokuwa na uwezo, watu wengine wanakuwa wanahofia ule uwezo wako. 

Sasa la msingi ni kuvumilia tu na kustahimili ipo siku Mungu atasema sasa wakati umefika fulani aonekane uwezo wake ambao siku nyingine ulikuwa hauonekani.

Sasa mimi nasaha [zangu] kwenye maisha ni kustahimili na kuvumilia na kusamehe. Ukiwa na moyo wa kusamehe basi mambo yatakwenda tu, hakuna shida.

Mahojiano haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na Asifiwe Mbembela na kuhaririwa na Lukelo Francis. Stephan Gimbi, Joseph Kiraty na Nassor Nassor walisimamia uzalishaji wa mahojiano haya. Kwa mrejesho, tuandikie: editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *