The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ulikuwa Unafahamu Kwamba Kuongopa ni Sehemu ya Makuzi ya Mtoto?

Badala ya kuweka msisitizo kwenye adhabu, tutumie nyakati hizi kama fursa za kumfundisha mtoto kuhusu ukweli, kujituma na kusamehe pamoja na madhara ya kusema uongo.

subscribe to our newsletter!

Kudanganya, kusema uongo au uzushi, kama kunavyotambulika, hututia wazazi katika hali ya wasiwasi. Wasiwasi huu, kiasili, huibuka kutoka katika hitaji la kuwajengea watoto wetu tabia za uaminifu na uadilifu, tukihofia kuwa tabia ya uongo utotoni inaweza kuashiria matatizo ukubwani. 

Wazazi tunashtuka hasa watoto wasemapo uongo kuhusu makosa madogo madogo, kama kutofanya kazi alizoachiwa, au kusema hakufanya kitu ambacho ni wazi amefanya. Uongo wa aina hii huonekana wa kawaida, lakini unaweza kuleta hisia ya kuharibika kwa misingi ya uaminifu kati ya mzazi na mtoto.

Dk Kang Lee, mtaalamu wa saikolojia ya maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Toronto, anatoa mtazamo mpya katika suala hili. Lee anaeleza kwamba uongo wa utotoni ni dalili chanya ya maendeleo ya kiakili.

Hii inaashiria kwamba mtoto wako anajenga fanisi kuu mbili: kusoma akili, yaani uelewa wa kwamba watu wengine wanafikra na ujuzi tofauti na wao, pamoja na kuidhibiti nafsi, yaani uwezo wa kuidhibiti mihemko, huku wakitoa mtazamo mbadala. 

Kwa maneno mengine, kusema uongo ni msingi wa kimaendeleo ya akili unaoashiria kwamba watoto wameanza kutambua kwamba watu wengine hawajui mambo wanayoyajua, na wanajifunza kuitathmini mienendo pamoja na maneno yao.

SOMA ZAIDI: ‘Mzazi ni daktari,’ Je, Kauli Hii Ina Uhalisia Gani?

Amini usiamini, watoto wanaweza kuanza kudanganya tokea umri wa miaka miwili na nusu! Katika umri huu, takribani theluthi ya watoto wote wameanza kusema uongo na kufikia miaka minne , asilimia themanini yao wamejaribu udanganyifu, tafiti zinaonesha.

Pale wafikapo miaka saba, karibu kila mtoto anakuwa, kwa namna moja au nyingine, amepindisha ukweli ili kufunika nyendo zake.

Pale wafikapo miaka saba au nane, uongo unakua sifa jumuishi kwa watoto wote. Watoto katika umri huu huwa mahiri katika utunzi visa vyenye ushawishi ili kuepuka madhara ya makosa au matatizo yao. Lee anadokeza kwamba karibu watoto wote walio katika umri huu watadanganya ili kuficha makosa yao.

Ukweli huu, hata hivyo, haumaanishi kuwa hatima ya watoto wetu ni kuwa watu wasio waaminifu. Badala yake, tabia hii inaashiria ukuaji wa uelewa wao wa mila na desturi za jamii zinaowazunguka pamoja na uelewa juu ya matokeo ya matendo yao. Hapa watoto wanaijaribu mipaka tuliyoweka sisi wazazi au walezi wao pamoja na kuchanganua jinsi ya kujenga mahusiano ya kina zaidi kati yao na sisi.

Chakufurahisha ni kwamba kiwango cha udanganyifu kinaanza kushuka baada ya umri wa miaka nane. Wafikapo miaka 12, kiwango cha udanganyifu kinashuka hadi asililmia 60 na kinaendelea kushuka kadri umri unavyosonga. 

SOMA ZAIDI: Ni Zipi Tabia Zinazoweza Kutufanya Tuwe Wazazi Bora Kwa Watoto Wetu?

Kwa kadri vijana wanavyoanza kujenga maadili na uelewa mpana wa mila na desturi za jamii zao, ndivyo wanavyozidi kuthamini uaminifu na hivyo kupunguza udanganyifu na kuwa waadilifu.

Dk Lee anapendekeza kwamba umri wa balehe katika vijana unaweza kutazamwa kama kipindi cha uaminifu, au ukweli, kwani vijana hawa hujenga uelewa wa kina zaidi juu ya mema na mabaya na wana uwezo mkubwa wa kuchukuliana, kusamehe au kuelewa hisia au hali za wengine. Matokeo yake ni wana uwezekano mdogo kudanganya wakilinganishwa na wadogo zao.

Hivyo, mtoto asemapo uongo, kulingana na umri wake, tujitahidi kukumbuka ni sehemu ya kawaida ya ukuaji. Badala ya kuweka msisitizo kwenye adhabu, tutumie nyakati hizi kama fursa za kumfundisha mtoto kuhusu ukweli, kujituma na kusamehe pamoja na madhara ya kusema uongo.

Tujenge mawasiliano ya wazi na tutengeneze mazingira salama ya kusema ukweli. Mzazi ndiye kielelezo cha kusema kweli daima kwa mtoto. Kwa njia hii, tunaweza kuwaongoza watoto wetu kuipitia hatua hii ya asili ya maendeleo na kuwasaidia waweze kukua kuwa watu waaminifu, waadilifu na wenye kujielewa.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *