Asasi za Kiraia za Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation ambazo zimepewa kibali na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoa elimu, zimepanga kuanza zoezi hilo Oktoba 25, 2024 ambapo wanatarajia kuwafikia wananchi takribani 56,000 kutoka kata 28 za halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro.
Wakizungumza baada ya kuwasili katika ofisi za halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Mwananchi, Joseph Bahebe na Mkurugenzi mwenza wa Mtanzania Foundation, Erick Lutta wameeleza kuwa mafunzo yatatolewa kupitia semina elekezi za siku mbili kwa wakufunzi zitakazofanyika katika maeneo ya Loliondo, Sale, na Ngorongoro.
Jumla ya wakufunzi 28 kutoka tarafa za Loliondo, Sare na Ngorongoro watapatiwa mafunzo hayo, ambapo nao watatakiwa kuwafikia wananchi takribani 200 ndani ya muda wa siku tano, kuanzia Oktoba 26, hadi Oktoba 31, 2024.
Semina ya kwanza inatarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa, tarehe 25 Oktoba 2024, katika Tarafa za Loliondo na Sale, na semina ya pili itafanyika siku ya Jumamosi, tarehe 26 Oktoba 2024, katika Tarafa ya Ngorongoro. Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa watoa elimu wote wanapata uelewa wa kina na mbinu bora za kuwafikia wananchi katika maeneo yao husika.
“Kutokana na mpango huo, jumla ya wananchi 5,600 wanatarajiwa kufikiwa moja kwa moja na Elimu ya Mpiga Kura kupitia mafunzo ya wakufunzi hawa 28,” imeeleza taarifa ya Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation.
Hivyo mkakati watakaoutumia ni kuhakikisha hao wananchi 5,600 kila mmoja wapo anawafikia wananchi 10 ili kuwezesha kufikia wapiga kura 56,000 waliokusudiwa katika zoezi hilo.
Ikumbukwe kuwa mwezi Septemba 17, 2024 Serikali kupitia kwa Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa ilitangaza kusitisha uamuzi wake kupitia tangazi la Serikali Namba 673 la Agasti 2, 2024 ambalo lilihusu kufuta vijiji takribani 25 wilayani humo. Hivyo kupitia uamuzi huo wa Serikali, uandikishaji wapiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeweza kufikia takribani 120,000.
Sambamba na hilo Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation zinakusudia kushiriki katika zoezi la uangalizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, 2024 kote nchini ikiwemo wilaya ya Ngorongoro.