The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mwamuzi Omary Mdoe Anastahili Adhabu Kali

Waamuzi wameshapigwa sana na wachezaji na mashabiki kwa kukosea katika kazi yao, sasa waamuzi wenyewe wakianza kurudisha utamaduni huu ni dhahiri kuwa usalama wao uwanjani utakuwa hatarini.

subscribe to our newsletter!

Kuna wanamichezo, hasa wapenzi wa soka, wamefungiwa maisha kujihusisha na mchezo huo maarufu nchini, kwa sababu tu walipingana na mchakato wa uchaguzi, wakaambiwa wamesababisha taharuki.

Wako waliopishana kauli na viongozi wa soka, wakatumikia adhabu ndefu kutojihusisha na mpira wa miguu, hadi kusababisha kuyumbisha ajira zao.

Wako wengine waliopatikana na makosa katika masuala ya usajili na kujikuta wakitwishwa adhabu ya kutojihusisha na mpira wa miguu kwa muda mrefu, pamoja na kwamba ushiriki wao kwenye mchezo huo ndio unaowawezesha kupata chochote cha kula.

Lakini cha ajabu ni hawa wanaojihusisha na mpira wa miguu kwa ridhaa, yaani waamuzi. Hawa wamekuwa wakifanya makosa makubwa, pengine yanayosababisha kuathiri hata ajira za waajiriwa kama wachezaji na makocha, lakini wapo wanadunda na wanaendelea kufanya makosa hayo.

Kamati ya Uendeshaji Ligi inapokutana, inajiridhisha kuwa mwamuzi alifanya kosa, na hivyo hatapangwa katika raundi mbili au tatu zinazofuata, na baada ya hapo, anarejea kuendelea na makosa yake!

Hatujapata tiba

Bila shaka, hatujapata tiba sahihi ya waamuzi wanaovuruga kwenye mechi za ligi, hasa ya juu nchini ambayo imevutia wawekezaji wengi wanaotaka kuona haki ikitendeka ili uwekezaji wao uonyeshe thamani wanayoitegemea.

SOMA ZAIDI: Simba, Yanga Wapaze Sauti kwa Pamoja Dhidi ya Upangaji wa Ratiba Unaobadilikabadilika

Na ukweli kwamba mpira wetu wa miguu haujafikia kiwango cha kutengeneza ajira kwa waamuzi, kinafanya kusiwepo na hatua kali dhidi ya wanaoboronga. 

Na ukweli kwamba sheria za mpira wa miguu zinampa mwamuzi wa kati uamuzi wa mwisho kuhusu tukio kutokana na maoni yake, kunakuwa na woga wa kuchukua maamuzi mazito dhidi yake.

Wenzetu kama Uingereza wamefikia hatua ambayo waamuzi wana chombo chao huru kabisa kinachoitwa Professional Game Match Officials Limited (PGMOL), au Kampuni ya Waamuzi wa Mchezo wa Kulipwa, ambacho kina Ofisa Mtendaji Mkuu.

Chombo kama hicho hakiwezi kulea ubovu wa waamuzi unaojirudiarudia kwa sababu kinajua wanachama wake ni wa aina gani na kimaslahi wanafikiriwaje.

Mwamuzi aliye chini ya chombo hicho hawezi kutoka nyumbani eti anakwenda kuonyesha ubabe wake dhidi ya wachezaji, au timu fulani, bali anaenda kutekeleza moja ya majukumu ya ajira yake yatakayoinufaisha taasisi yake na mchezo wenyewe kwa ujumla.

SOMA ZAIDI: Mashabiki Taifa Stars Watoke Wapi?

Hawezi kujijengea utamaduni kwamba “mchezaji hawezi kunisogelea mimi” hata kama mwamuzi mwenyewe amekosea, bali atakuwa tayari kumsikiliza na kumuelewesha mchezaji alichukua uamuzi huo kwa sababu gani. 

Ndio maana kwa wenzetu, mazungumzo kati ya wachezaji na waamuzi ni ya kirafiki, yenye lengo la kuonyesha hisia za mchezaji kuhusu tukio, na maelezo ya mwamuzi kuhusu uamuzi wake. Ukibisha, hapo ni suala jingine.

Na pengine ndio maana PGMOL wana mpango wa kuanza kutumia utamaduni wa mchezo wa kriketi wa mwamuzi kuwaambia mashabiki waliopo uwanjani sababu za kufanya uamuzi fulani wa tukio tata.

Tayari, Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) limeshajaribu mfumo huo wa kuzungumza na mashabiki, kwa kutumia vipaza sauti vilivyopo uwanjani na vinasa sauti wanavyotumia waamuzi, kutangaza sababu za uamuzi wa tukio fulani kabla ya kuruhusu mchezo kuendelea.

Haya yote yanalenga kuongeza uwazi na kumwajibisha refa kufanya kazi yake kwa weledi zaidi kuliko hivi sasa. 

SOMA ZAIDI: Tumeacha Mapinduzi Kwenye Klabu, Sasa Tunayumbisha Seckretarieti

Kwa sasa, mwamuzi anaweza kuamua lolote na baadaye kuandika kwenye ripoti yake mambo ya uongo yanayoweza kusababisha mchezaji ambaye kwake soka ni ajira, aadhibiwe kwa kuzuiwa kucheza mechi kadhaa, na kuathiri vyanzo vyake vya mapato kama bonasi za mechi, za ushindi na mambo mengine binafsi kama kufunga bao.

Mambo ya kukunjana

Nimetanguliza yote hayo kutokana na tukio la wiki iliyopita la mwamuzi kutaka kurudisha mambo ya kukunjana na, ikiwezekana, kupigana uwanjani yaliyotawala mchezo wa mpira wa miguu kwenye miaka ya sabini hadi tisini.

Nyakati hizo waamuzi, hasa wa kati, walikuwa wakipigwa si kwa sababu ya makosa au kupendelea tu, hata wakati mashabiki walipotofautiana nao kimtazamo katika uamuzi ambao pengine ulikuwa sahihi.

Mechi ya mwisho kubwa kushuhudia mwamuzi akipigwa na wachezaji na kulazimika kukimbia kujiokoa ilikuwa ni kati ya Yanga na Azam kwenye Uwanja wa Uhuru.

Lakini uungwana na ustaarabu umetamalaki katika mpira wa miguu wa sasa na ndio maana wachezaji humuendea mwamuzi wakiwa wameweka mikono yao nyuma, au sehemu nyingine, kuashiria kuwa hawaendi kwa shari bali kuhoji, au kulaumu, kuhusu uamuzi wa refa.

SOMA ZAIDI: Serikali Ianze Kutoa Ruzuku kwa Vyama Teule vya Michezo 

Lakini mwamuzi Omary Mdoe aliona kitendo cha mchezaji wa Mashujaa, Yusuf Dunia, kumsogelea, huku akiwa ametanua mikono yake, kuwa hakifai. Baada ya Dunia kumkaribia, Mdoe alimshika shingoni na kumsukuma. Ni vile tu mchezaji huyo ana nguvu hakuweza kwenda chini, au hakupata akili ya kujiangusha ili itafsiriwe kuwa amempiga ngumi.

Na hata alipomwendea kwa mara ya pili akiwa ametanua mikono yake, refa Mdoe alitumia nguvu zaidi kumkaba shingoni na kumsukumia mbali. Busara ambayo mwamuzi alitakiwa aitumie, ilitumiwa na wachezaji wa Mashujaa ambao walimfuata Mdoe kwa upole, kuzungumza naye, na kumuondoa Dunia kwenye tukio hilo.

Matumizi ya nguvu

Haieleweki ni kwa vipi mwamuzi alitumia nguvu namna ile kwa tukio ambalo halistahili hata kadi ya njano. Maana kama alitukanwa, au kufanyiwa lolote linalostahili adhabu ya kimichezo, refa angetumia mamlaka aliyonayo, ama kumuonyesha kadi nyekundu, au ya njano kwa lengo la kumuonya.

Lakini kwa kuwa inaonekana mchezaji hakufanya kosa lolote la kimpira, mwamuzi hakutoa adhabu yoyote iliyo kwenye sheria za soka, zaidi ya kutumia sheria zake za ubabe kumsukuma mchezaji na kuruhusu mchezo uendelee baada ya tukio kupoa.

Hakuna neno zuri unaloweza kutumia kuelezea kitendo cha refa zaidi ya kukiita kuwa ni “uhuni.” Ule ni uhuni ambao hautakiwi kulelewa hata kidogo katika mchezo huu pendwa.

SOMA ZAIDI: Tufuatilie Sakata la Man City kwa Makini Tukijitathmini 

Tulikotoka ni mbali. Waamuzi wameshapigwa sana na wachezaji na mashabiki kwa kukosea katika kazi yao, sasa waamuzi wenyewe wakianza kurudisha utamaduni huu ni dhahiri kuwa usalama wao uwanjani utakuwa hatarini.

Katika kipindi kama hiki ambacho takriban asilimia 40 ya mechi zote za mzunguko wa kwanza zilizochezwa hadi sasa, lawama nyingi zimekwenda kwa waamuzi, ni muhimu sana kwa wapuliza filimbi hao kuwa waungwana na kukubali kuwa kupewa dhamana ya kuamua mechi, si kupewa tuzo ya ukali dhidi ya wachezaji, ubabe kwa kuwa anaweza kutoa kadi na mambo mengine yasiyofaa.

Moto wa mpira wa miguu ni haki na uungwana, na hivyo tunategemea mamlaka zitunze ari hii kwa kumchukulia hatua kali Mdoe, ikiwezekana kumfungia na kumshusha daraja hadi hapo atakapohitimu mafunzo ya kurekebisha tabia yake.


Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts