Kati ya Novemba 25 na Disemba 10 ya kila mwaka, wachechemuzi na wanaharakati wa haki za binadamu huwekeza na hujikita katika Kampeni za Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kote ulimwenguni.
Kampeni hizi ni harakati za kimataifa zinazolenga kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia. Ingawa juhudi nyingi zinalenga kuleta mabadiliko chanya katika sera na mipango ya kidunia, kitaifa na jamii kwa ujumla, bado wazazi na walezi tuna nafasi ya kipekee katika kuwajengea uwezo, uelewa na ufahamu watoto wetu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia.
Mazungumzo yenye tija kuanzia ngazi ya familia kuhusu ukatili wa kijinsia pindi watoto wangali wadogo huchochea huruma, heshima, na uelewa kwa watoto na hivyo kujenga misingi ya jamii salama na yenye usawa na misingi ya kuheshimiana na kuthaminiana, jambo ambalo hudhibiti ukatili wa kijinsia katika maisha ya baadae.
Hakuna umri sahihi wa kuanza kuwafundisha watoto kuhusu heshima na utu, kuwa na wema, na mipaka ya kibinafsi.
Mazungumzo yanayofaa umri wao kuhusu ukatili wa kijinsia yanaweza kuanza mapema na kuwasaidia watoto kuelewa umuhimu wa kumheshimu kila mtu kwa haki na usawa, kuwapa maarifa yanayowawezesha kutambua tabia zisizofaa na kuunda utamaduni wa uwazi ambapo wanajisikia salama kuzungumza masuala nyeti yanayoathiri ustawi wao.
SOMA ZAIDI: Una Mtoto Mwenye Umri Kati ya Miaka Miwili na Sita? Haya Yatakusaidia Kumjengea Nidhamu
Kwa watoto wadogo, hususan wenye umri kati ya miaka mitatu na saba, tunaweza kujadiliana nao mambo kwa urahisi, tukizingatia dhana kama heshima na mipaka ya kibinafsi.
Tuwaelimishe kwamba miili yao ni mali yao, na anaweza kusema “HAPANA” au “SITAKI” ikiwa hawajafurahia jambo lililofanyika kwenye miili yao. Tujitahidi kutumia vitabu na hadithi kama zile za sungura na fisi kufafanua wema na haki unafananaje na unatendajwe. Pia, sisi wenyewe inatupasa kuwaonesha tunaziishi tabia hizo.
Watoto wa umri kati ya miaka minane na kumi na moja wanakuwa na uelewa mkubwa wa mienendo ya kifamilia na kijamii, na huu ni wakati mzuri wa kuanzisha mijadala ya kina zaidi. Tunaweza kuwaeleza maana ya ukatili wa kijinsia kwa njia rahisi, tunaweza kuwaeleza kwamba “ukatili wa kijinsia ni kumdhuru mtu kwa sababu ya jinsia yake.”
Kisha tujadili nao umuhimu wa kupinga uonevu, haswa pale mtu mwingine anapofanyiwa matendo yanayokiuka haki zake. Tusisahau kuwahimiza watoto waulize maswali pale ambapo hawajaelewa ili kutengeneza mazingira ya mazungumzo na mijadala ya wazi kati yetu na watoto wetu.
Pale watoto wakifika miaka 13 na kuendelea, wanakutana na mijadala kuhusu ukatili wa kijinsia shuleni, lakini sana sana mtandaoni na kupitia marafiki zao. Hivyo, ni rahisi kwao kupata elimu ambayo siyo sahihi, au isiyojitosheleza kuhusu ukatili wa kijinsia.
SOMA ZAIDI: Watoto wa Miaka Mitano Wana Harakati Nyingi. Mbinu Hizi Zitakusaidia Kukabiliana Vizuri
Tuwaeleze kwamba ukatili sio kosa la muathirika, bali ni la yule aliyefanya kitendo hicho. Tuwasisitize watoto wetu kwamba kila mtu anastahili kujisikia salama, kuthaminiwa na kuheshimiwa, bila kujali jinsia yake.
Tuwasaidie watoto kuelewa mada hizi kwa utashi kwa kujadili nao kuhusu mahusiano yenye afya na umuhimu wa kuomba na kupewa ridhaa, kuhusu dhana potofu za kijinsia na jinsi zinavyosababisha ukatili na kuwaeleza wapi wanaweza kutoa taarifa wakishuhudia, au kufanyiwa, vitendo vyovyote vya ukatili, sisi wazazi tukiwa mstari wa mbele.
Maswali ambayo yanaweza kutusaidia kuanzisha mazungumzo kuhusu ukatili wa kijinsia na watoto ni kama: Umewahi kusikia neno ukatili? Unafikiri lina maana gani? Unajisikiaje unapoona mtu anatendewa kitu kibaya kwa sababu ya jinsia yake? Ikiwa upo katika hali ambayo hujihisi salama, utamwambia nani, au utachukua hatua gani?
Tunapoendelea kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, tukumbuke kwamba elimu ya usawa wa kijinsia na haki za binadamu huanzia nyumbani. Wazazi tuna uwezo wa kukuza kizazi kinachothamini usawa, heshima, haki na usalama kwa wote.
Kwa kuanzisha mazungumzo kuhusu usawa wa kijinsia mapema, na kuendelea kadri watoto wanavyokua, tunaweza kujenga msingi wa jamii yenye haki na usawa.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.