Dodoma. Zimebaki siku chache kabla hatujauga mwaka 2024 ambao, kusema ukweli, ulikuwa na hekaheka nyingi sana, ukigubikwa na mambo na vijambo vingi viliyoufanya ukimbie kwa kasi ya ajabu, ukituacha wengi wetu na masikitiko ya kupungua kwa siku zetu za kuishi ulimwenguni hapa!
Pengine hakuna tukio kubwa zaidi lililotokea mwaka huu ukilinganisha na lile la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa lililohitimishwa Novemba 29, 2024, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, kwa kutangaza washindi kwenye uchaguzi huo wa wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji.
Kwenye uchaguzi huo, chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), kilitangazwa kushinda kwa asilimia 99, hali iliyoibua maoni na hisia tofauti miongoni mwa Watanzania. Kwa wanachama na wafuasi wa CCM, matokeo hayo yalidhihirisha uungwaji mkono mkubwa wa sera zake miongoni mwa Watanzania.
Lakini kwa wakosoaji, ikiwemo vyama vya upinzani, matokeo hayo yalitokana na rafu ambazo CCM, ikishirikiana na vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi, ilizifanya kwenye zoezi zima la uchaguzi.
Rafu hizi, wakosoaji hawa wanadai, zinajumuisha kuenguliwa kiholela kwa wagombea wa upinzani, kunyimwa barua kwa mawakala wao, uwepo wa kura bandia, na ukatili na fujo dhidi ya wagombea wa upinzani.
Iwe itakavyokuwa, kasoro za msingi zilijitokeza kwenye zoezi hili na hivyo kuwanyima wananchi uhuru mpana wa kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa kidemokrasia wa kuchagua wawakilishi wao. 2025 ni mwaka wa uchaguzi mkuu, na ni matumaini ya wengi kwamba mamlaka husika zitatumia uzoefu uliopatikana kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuboresha uchaguzi huo wa Rais, wabunge na madiwani.
Watoto kupotea
Mbali na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mwaka 2024 pia uligubikwa na taarifa nyingi za “kutekwa,” au kupotea katika mazingira tatanishi, kwa watoto katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Taarifa hizi zilikuwa nyingi sana kiasi cha kuwajaza hofu wazazi na walezi wengi. Kwenye kukabiliana na hofu hizi, wazazi na walezi hawa, muda mwingine, walijikuta wakichukua hatua za hatari, zilizo nje ya mipaka ya kisheria.
SOMA ZAIDI: Tumekusanya Matukio Yaliyoripotiwa ya Watoto Kupotea Tanzania. Haya Hapa Ndiyo Tuliyoyapata
Mnamo Septemba 11, 2024, huko mkoani Geita, kwa mfano, wananchi wenye hasira kali waliwavamia watu wawili waliokuwa wamebeba mtoto mdogo waliodhaniwa kuwa ni watekaji.
Baada ya afisa mtendaji kata kuwabeba washukiwa hao na kuwapeleka polisi, wananchi hao walikwenda kituo cha polisi, wakidai wapewe washukiwa hao wawili ili wawaue.
Polisi waligoma kuwatoa washukiwa hao, hali iliyopelekea fujo na kuwalazimisha polisi kutumia silaha za moto “kutuliza” vurugu hizo, na kupelekea vifo vya watu wawili. Wananchi hao wenye hasira pia walichoma moto gari lililokuwepo katika kituo hicho cha polisi, hali iliyopelekea kukuza dhahma iliyokuwa ikitokea hapo.
Huu ni mfano mmoja tu wa namna gani wananchi walikabiliana na hofu walizokuwa nazo kuhusu kusambaa kwa taarifa za watoto kutoweka katika mazingira ya kutatanisha ambazo, kwa kiasi kikubwa, zilitanda kwenye vyombo vingi vya habari kwa mwaka huu unaoyoyoma wa 2024.
Kuna nadharia nyingi ziliwekwa hadharani kuelezea “kushamiri” kwa matukio haya, moja ikiwa ni kuhusishwa kwake na imani za kishirikina zinazoambatana na matukio ya uchaguzi.
Baadhi ya wachangiaji walijaribu kuonesha kwamba kila ifikapo uchaguzi, matukio haya ya kutoweka kwa watoto hushamiri, ikihisiwa kwamba waliotia nia kugombea wako nyuma ya matukio haya kuimarisha nafasi zao za ushindi kwenye vinyang’anyiro hivyo.
Wakati ni ngumu kuthibitisha madai haya, inawezekana kwa mamlaka husika, kama vile polisi, kwa ushirikiano wa karibu na jamii kwa ujumla, kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto, hususan kwa mwaka tunaokaribia kuuingia, tukibahatika, wa 2025, ambao pia ni mwaka wa uchaguzi na unatarajiwa kuwa na matukio mengi sana.
Utekaji
Linalokaribiana na hili la watoto kutoweka katika mazingira ya kutatanisha ni taarifa za watu kutekwa ambazo zimekuwa zikichukua sehemu kubwa ya mazungumzo rasmi na yasiyo rasmi ya Watanzania katika miktadha mbalimbali.
Taarifa hizi za kutekwa kwa Watanzania, wengi wao wakiwa ni wakosoaji wa Serikali, wafanyabiashara na viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani, zimekuwa zikiliweka Jeshi la Polisi, na Serikali kwa ujumla, kikaangoni, wakitakiwa siyo tu wakomeshe vitendo hivi na kuwarejesha wale waliotekwa, bali pia kuchunguza wahusika wake na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
TAZAMA: Nani Aliyewateka, Kuwapoteza Watanzania Hawa?
Kwenye macho ya Watanzania, kwa kuangalia maoni wanayotoa kwenye vyombo vya habari na njia zingine za mawasiliano, hususan mitandao ya kijamii, Serikali, na vyombo vyake vya utawala, haijaonesha ukali wa kutosha unaoweza kusitisha vitendo hivi, kama inavyothibitika kwa kuendelea kwao kutokea kila uchao.
Baadhi ya Watanzania wamemuangukia Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati na kurekebisha hali hiyo.
Kivumbi CHADEMA
2024 pia ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi ndani ya CHADEMA, na inavyoonekana ni kama vile kinyang’anyiro ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania, licha ya kwamba kitakamilishwa mapema 2025, ndiyo kitakuwa kifunga mwaka kikubwa labda jambo jingine kubwa zaidi lijitokeze kwenye masaa machache yaliyobaki ya 2024.
Kinachonogesha na kuvuta hisia za wengi kwenye uchaguzi huo wa ndani wa CHADEMA ni, pamoja na mambo mengine mengi, uamuzi wa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Tanzania Bara), Tundu Lissu, kuamua kuchuana na Mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe, kwenye nafasi hiyo kubwa ya uongozi wa chama.
Lissu na Mbowe, ambaye ameweka wazi nia yake ya kutetea nafasi yake hiyo, wanamitazamo tofauti kidogo juu ya namna CHADEMA inapaswa kukabiliana na aina mpya za siasa zinazoendeshwa na CCM na Serikali yake, ambazo, kwa kiwango kikubwa, zinafanyika kwa namna inayoonekana kukiuka misingi ya demokrasia ya vyama vingi.
SOMA ZAIDI: CHADEMA Kuelekea 2025: Mivutano Hii Itaiacha Salama?
Lissu anataka chama kiibue ari na hamasa ya wanachama na Watanzania ili waweze kuinuka na kuikataa hali hii, akionekana kuponda na kubeza kile kinachoitwa “maridhiano” kati ya CHADEMA na CCM. Mbowe, kwa upande wake, haonekani kutoona umuhimu wa kutumia “nguvu ya umma” kukabiliana na “uimla” wa CCM, lakini anahimiza, na kutetea, mbinu ya maridhiano.
Kinachoupa mvuto zaidi mchakato huu wa ndani wa CHADEMA ni kambi za wawili hawa ambazo wafuasi wake wamekuwa wakibadilishana maneno makali kwenye mitandao ya kijamii, hali ambayo imewafanya baadhi ya Watanzania wahoji dhamira ya CHADEMA, kama chama cha siasa, kuamini kwenye misingi ya demokrasia inayodai kuipigania.
Kuna maoni kwamba, kama chama hakitachukua hatua za madhubuti kudhibiti hali hiyo, uchaguzi wa chama utaishia kukigawa chama, hatma ambayo si nzuri sana kwa siasa za vyama vingi Tanzania.
Muda utaamua ni kwa namna gani CHADEMA itaendesha uchaguzi wake wa ndani katika hali inayoashiria ukomavu, na kutoka kwenye mchakato huo kikiwa imara na kimoja, badala ya dhaifu na vipande vipande.
Vifo mashuhuri
2024 ilikuwa na matukio mengi sana muhimu kuweza kuyaweka yote hapa kwa pamoja; kujaribu kufanya hivyo ni jambo lisiloingia akilini. Hata hivyo, hatutajitendea haki endapo kama tutamaliza safu hii bila kuwakumbuka baadhi ya Watanzania mashuhuri, ambao mchango wao kwenye ujenzi wa taifa unatambulika kwa wote, walioaga dunia mwaka huu tunaokaribia kuufunga.
Miongoni mwa wale waliotutoka mwaka huu ni pamoja na Ally Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya pili, aliyejulikana miongoni mwa Watanzania kama “Mzee Rukhsa,” kutokana na mchango wake wa kuitoa Tanzania kwenye hali ya mdororo mkubwa wa kiuchumi kwenye miaka ya 1980, aliyeaga dunia Februari 29, 2024.
SOMA ZAIDI: Nitakavyomkumbuka Mwinyi, Mzee Rukhsa Asiyekuwa na Tamaa ya Madaraka
Edward Lowassa, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na mgombea urais aliyeungwa mkono na umoja wa vyama vya upinzani 2015, naye alifariki mnamo Februari 10, 2024, akiacha urathi unaobishaniwa miongoni mwa wafuatiliaji wa mambo Tanzania. Kifo kingine kilichogusa hisia za wengi ni kile cha Faustine Ndugulile, kilichotokea Novemba 27, 2024.
Dk Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni (CCM) na Mkurugenzi Mteule wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), alipata pia kuhudumu kama waziri kwenye nyadhifa mbalimbali Serikalini. Watu wengi walimlilia Ndugulile kutokana na utumishi wake wa umma uliotukuka, uliombatana na utayari wake wa kusikiliza, uadilifu na huduma kwa jamii.
Matukio mengine yaliyoukabili mwaka 2024 na ambayo yataacha kumbukumbuka za muda mrefu kwenye mawazo ya Watanzania ni pamoja na lile la Novemba 16, 2024, ambapo jengo la ghorofa nne maeneo ya Karikoo, Dar es Salaam, lilianguka na kusababisha maafa na majeraha kadhaa.
Ukiachana na majonzi na simanzi ambazo tukio hili lilisababisha, ilitia faraja pia kuona namna lilivyowaleta Watanzania pamoja, hali ambayo si ya kawaida, na ambayo haiwezi kuchukuliwa poa, ukizingatia mambo mengi ambayo yanawagawa Watanzania kwa sasa.
Matukio mengine
Mengine ni kama lile lililomuhusisha Yahaya Nawanda, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, aliyedaiwa kumbaka binti mmoja wa elimu ya juu huko jijini Mwanza, na kupelekea kutenguliwa kwenye wadhifa wake huo.
Ni tukio lililoibua hisia na mjadala mpana miongoni mwa Watanzania, huku maoni yakigawanyika kati ya wale wanaomtetea anayedaiwa kuwa mwathirika wa kitendo hicho na Dk Nawanda.
SOMA ZAIDI: Kesi Ya Nawanda Yapigwa Kalenda Mpaka Septemba
Baada ya kesi kuendelea mahakamani kwa muda kidogo, Nawanda aliachiwa huru baada ya Mahakama kusema hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba Nawanda alifanya kosa aliloshitakiwa nalo.
Tukio jingine lililoshitua nchi ni lile lililohusisha askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kumbaka na kumlawiti mtoto mmoja wa kike aliyetambulishwa kama “Binti wa Yombo,” huku wakijirekodi video wakati wakitenda uhalifu huo.
Ilidaiwa kwamba “kosa” la binti huyo ni kutoka na mume wa afisa mmoja mwandamizi wa Jeshi la Polisi, aliyedaiwa kuwatuma vijana hao “kumuadhibu” binti huyo.
Ilikuwa ni tukio lililoiabisha sana Tanzania, likiwafikirisha wananchi ni kwa namna gani jamii yao imefika katika hatua ya kufanya uhalifu wa aina hiyo, huku ukiwa na uthubutu wa kujirekodi video.
Vijana hao walishitakiwa, na kuadhibiwa kifungo cha maisha jela, ikitegemewa kwamba hiyo itakuwa ni funzo kwa wale wote wanaofikiria kufanya aina hiyo ya uhalifu siku zinazokuja.
Bila ya shaka kuna matukio mengi zaidi ya haya yalitokea Tanzania mwaka 2024. Wito wetu kwako kama msomaji ni kutafakari matukio yote haya tukiwa tunauaga mwaka huu, tukichukua mafunzo yatakayotusaidia kutoa mchango chanya kwenye ujenzi wetu wa pamoja wa jamii tunazozitamani!
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.