Mwanaharakati wa haki za binadamu, Maria Sarungi Tsehai ametekwa na kikundi cha watu watatu wenye silaha jijini Nairobi leo majira ya saa tisa na dakika kumi na tano mchana.Taarifa hiyo imetolewa leo Januari 12, 2025, na Shirika la Utetezi na Ulinzi wa Haki za Binadamu, Amnesty International.
‘Maria Tsehai, mhariri wa habari na mtetezi wa haki za binadamu ametekwa na watu watatu wenye silaha waliokuwa kwenye Noah nyeusi, katika eneo la Chaka, Kilimani, Nairobi majira ya saa tisa na dakika kumi na tano leo mchana,” taarifa hiyo ilieleza.
Kenya ni moja kati ya nchi iliyoghubikwa na matukio mengi ya utekaji, hasa wa wanaharakati, matukio yaliyoshamiri katika nchi za Jumuiya ya Arika Mashariki. Hata hivyo sehemu kubwa ya matukio haya yamekuwa yakitokea kwa raia wa Kenya mpaka katika siku za hivi karibuni.
Mnamo Oktoba 2024, raia kadhaa wa kadha kutoka Uturuki wanaodaiwa kukimbia nchi yao kwasababu za kisiasa walitekwa jijini Nairobi jambo lililosababisha mashirika mbalimbali ikiwemo Umoja wa Mataifa kukemea jambo hilo.
Pia mnamo Novemba 16, 2024, Kiongozi wa chama cha upinzani cha Uganda, Forum for Democratic Change (FDC), Dr Kizza Besigye, alitekwa jijini Nairobi na kupelekwa Uganda, ambapo alisomewa mashtaka mbalimbali katika mahakama ya kijeshi na kesi yake bado inaendelea.