Watoto wetu wanahitaji uimara wa hisia na akili katika kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa sasa. Watoto wanakutana na matatizo mbalimbali—kuanzia masomo, mahusiano ya kijamii, hadi athari za teknolojia—na ni muhimu kuwasaidia kuimarisha hali yao ya kihisia na kisaikolojia.
Kauli chanya, yaani maneno ya kujihamasisha yanayowatia moyo na kuwajengea imani binafsi, ni nyenzo yenye nguvu inayosaidia ukuaji wa kiakili na kihisia kwa watoto. Makala hii itaangazia umuhimu wa kauli chanya kwa watoto katika kukuza na kuimarisha hisia na akili. Tutatumia mifano halisi, maoni ya wataalamu, ushahidi wa kisayansi, na ushuhuda wa wazazi kulielezea hili
Sayansi inasemaje kuhusu kauli chanya?
Kauli chanya huchochea mabadiliko chanya katika akili za watoto. Tafiti zinaonesha kuwa ubongo wa binadamu unaweza kuunda njia mpya za neva kutokana na mawazo yanayorudiwa mara kwa mara. Dk Caroline Leaf, mtaalamu wa neva na mwandishi maarufu, anasema: “Unapowaza kwa kusudi kuhusu mambo mazuri, unaimarisha njia za neva zinazosaidia kujiamini, kustahimili, na kujifunza.”
Utafiti uliochapishwa mwaka 2016 katika jarida la Social Cognitive and Affective Neuroscience ulionesha kuwa kujihamasisha kunaamsha sehemu za ubongo zinazohusiana na motisha. Kwa watoto, ambao ubongo wao bado unakua, kurudia rudia kauli chanya kunaweza kuwasaidia kujenga msingi wa kujiamini na ustahimilivu.
SOMA ZAIDI: Fahamu Mbinu Zinazoweza Kuimarisha Mawasiliano Kati ya Mtoto na Mzazi
Dk Laura Markham, mtaalamu wa saikolojia ya familia na mwandishi wa Peaceful Parent, Happy Kids, anasema: “Watoto hujifunza kutoka kwa maneno wanayoyasikia mara kwa mara. kauli chanya zinawasaidia kufuta athari za ukosoaji au ujumbe hasi wanaoweza kukutana nao.”
Wazazi na walimu wameshuhudia matokeo mazuri ya kauli chanya kwa watoto. Kwa mfano, Mariamu, mtoto wa miaka sita aliyekuwa na hofu ya kushindwa kufanya mitihani yake vizuri, alianza kuambiwa na bibi yake kila siku awe anajiambia, “Ninaweza kujifunza kutoka kwa makosa yangu” na “Nina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri.” Baada ya miezi michache, alionesha ujasiri mkubwa wa kujaribu maswali magumu na hata kusaidia wenzake shuleni, alieleza bibi yake.
Walimu pia hutumia kauli chanya kuimarisha mshikamano na motisha darasani. Kauli kama, “Sisi sote tunaweza kujifunza na kufaulu” au “Kila siku ni fursa nyingine ya kujitahidi kuwa bora kuliko jana; zinawasaidia wanafunzi kujenga utamaduni wa kushirikiana na kuhimiza maendeleo ya pamoja.
Tafiti zinaendelea kudhihirisha kwamba kauli chanya zina nguvu katika kuimarisha kujiamini kwa mtoto. Watoto wanaoambiwa mara kwa mara kuwa wanaweza kufanikisha mambo flani huwa na mtazamo wa kujiamini hata wanapokutana na changamoto.
Kauli chanya zinasaidia kujenga ustahimilivu wa kihisia, kauli kama “Ninaweza kufanya jambo lolote nikijiamini” huwapa watoto mbinu za kukabiliana na hali ngumu kwa ujasiri na matumaini, hivyo inashauriwa kuwahimiza watoto kujinenea mazuri na sisi wazazi pia kuendelea kuwatia moyo kwa kuwanenea mazuri na kuwasifia wanapofanya vizuri katika mambo mbalimbali ikiwemo masomo, vitendo vyenye kuonesha tabia njema pamoja na kujituma katika na kazi za nyumbani.
SOMA ZAIDI: Tukumbushane Mambo Muhimu Tunayohitaji Katika Kuwaandaa Watoto kwa Mwaka Mpya wa Shule
Kauli chanya pia hukuza ari ya kujifunza kwa watoto. Dhana ya “Ninajifunza kutokana na makosa” huwafanya watoto wasihofu kushindwa bali waone kila changamoto kama fursa ya kujifunza. Pia, wanaposikia kauli za kuwatia moyo mara kwa mara wanakuwa na msukumo binafsi wa kutaka kujifunza zaidi na kufanya vizuri katika nyanja mbalimbali za maisha yao.
Mzazi mwenye uwezo wa kutoa kauli chanya mara kwa mara kwa watoto anaaminika kuwa na utulivu wa kihisia hivyo kauli hizo huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha mahusiano ya familia.
Wazazi wanaowaambia watoto kauli chanya hujenga uhusiano wa karibu zaidi na watoto wao. Kwa mfano, tukiwaambia watoto wetu “Ninafurahia juhudi zako,” kunawafanya wahisi kuthaminiwa na hivyo huonesha ushirikiano katika majukumu wanayopewa ndani ya familia pamoja na kuamini kwamba familia ndiyo kimbilio panapokuwa na chngamoto.
Wazazi waliojaribu mazoezi ya kutoa kauli chanya wameeleza kuona mabadiliko makubwa kwa watoto wao. Mfano, Bi. Lydia, mama wa watoto watatu, anasema: “Tulianza mazoezi haya na wajukuu wangu kwa kusema kauli rahisi kila asubuhi kama, ‘Leo ni siku nzuri, Mimi ni mwerevu, Mimi ni mzuri, Mimi nina uwezo mkubwaa’ na nimeona wakiwa na mtazamo wa matumaini zaidi.”
Hivyo basi, kila siku asubuhi, tuwaambie watoto kauli chanya kama, “Leo nitaweka juhudi zaidi kuliko jana” au “Mimi napenda kuwa mimi’. Kabla ya kulala, tuwaambie watoto kauli zinazochochea shukrani kama, “Ninashukuru kwa mafanikio yangu ya leo.”
SOMA ZAIDI: Sikukuu Zisitufanye Tuzembee Ulinzi wa Watoto Wetu. Waovu Hawalali Tukisherehekea
Tunaweza kuandika taarifa chanya kwenye karatasi na kuviweka sehemu zinazoonekana kama kioo cha bafuni au kwenye begi la shule la mtoto. Pia, tuwaulize watoto waelezee mambo wanayojivunia na waandike kauli zinazochochea mambo hayo wenyewe.
Tunatumaini kuwa makala hii imetukumbusha jinsi gani kauli chanya ni nyenzo yenye nguvu inayoweza kusaidia watoto wetu kujiamini na kukuza mtazamo mzuri wa maisha. Kama Dkt. Leaf anavyosema, “Maneno tunayoambiana yanaweza kuwa msingi wa sauti ya ndani tunayobeba maishani.”
Kauli hizi sio kwa watoto tu, hata sisi wazazi tunaweza kufanya zoezi hili kwa ajili ya maendeleo yetu wenyewe. Tukichukua hatua sasa, tunaweza kujenga kizazi kinachojiheshimu, kinachostahimili changamoto, na kinachoamini katika uwezo wao wa kufanikisha ndoto zao.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.