Moja ya mambo yanayonifanya nitafakari sana kama kijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kiongozi wa vijana ni namna ambavyo kizazi cha sasa cha vijana, hasa Gen Z, kinavyotazama maendeleo ya nchi.
Hiki ni kizazi tofauti na vizazi vilivyopita. Kimekulia katika dunia iliyounganishwa na teknolojia, ambapo taarifa zinapatikana kwa sekunde chache na kila mtu anaweza kuona namna nchi nyingine zinavyoendesha uchumi, miundombinu, elimu, afya na huduma za umma.
Kwa Gen Z, dunia ndiyo darasa lao. Wanapoona video za miji kama Dubai, Singapore, Guangzhou au Pretoria, hawaoni ndoto; wanaona viwango vinavyowezekana kufikiwa. Wanaposoma historia ya mageuzi ya Malaysia, Korea Kusini au Singapore, wanaona ushahidi kwamba uongozi wenye maono, sera sahihi na utekelezaji madhubuti unaweza kubadilisha taifa ndani ya kizazi kimoja.
Kutokana na mazingira hayo, matarajio yao kuhusu maendeleo ni makubwa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu.
Changamoto iliyopo ni kwamba wengi wa Gen Z hawana kumbukumbu ya Tanzania ya zamani. Hawakuiona Tanzania yenye uhaba mkubwa wa barabara, umeme, mawasiliano, au huduma nyingi za msingi. Tanzania wanayoijua ni hii ya leo.
SOMA ZAIDI: Tusidanganyane: Sh200 Bilioni ni Mradi wa Kisiasa wa Watawala, Sio Uwezeshaji wa Vijana Wote
Hivyo, ukiwaambia kwamba zamani hakukuwa na barabara za lami, au umeme ulikuwa unapatikana kwa shida, mara nyingi hawapimi maendeleo kwa kulinganisha na tulikotoka, bali kwa kulinganisha na kile wanachokiona duniani leo.
Kwao, maendeleo yanamaanisha huduma bora, miundombinu ya kisasa, fursa za ajira, teknolojia, usafiri wa uhakika, miji iliyopangwa vizuri na Serikali inayotoa huduma kwa ufanisi. Wanataka kuona matokeo yanayogusa maisha yao kila siku.
Labda ndiyo sababu miradi kama Reli ya Kisasa (SGR) imekuwa ikitajwa na vijana wengi kama moja ya mafanikio makubwa ya Tanzania katika miaka ya karibuni. Ni mradi unaoonekana, unaotumika na unaobadilisha taswira ya nchi.
Hivyo, ni jambo la kutia moyo kuona Serikali ikiendelea kupanua mtandao wa SGR ili kuunganisha kanda mbalimbali za Tanzania. Miradi ya aina hii huwapa vijana ushahidi kwamba taifa linaweza kujenga miundombinu yenye viwango vya kimataifa.
Hata hivyo, kujenga reli pekee hakutoshi. Tunahitaji kuhakikisha kuwa ubora huo unaonekana pia katika huduma nyingine za umma. Umeme wa uhakika, maji safi na salama, hospitali zenye huduma bora, shule zinazozalisha maarifa yanayokidhi mahitaji ya dunia ya sasa, pamoja na mifumo ya kidijitali yenye ufanisi, vyote vinapaswa kujengwa kwa viwango vinavyolingana na matarajio ya kizazi hiki.
SOMA ZAIDI: Ushiriki wa Vijana katika Maendeleo: Tuache Kauli Mbiu, Tujikite kwenye Mifumo
Hapa ndipo ninapoona wajibu mkubwa wa sisi vijana ambao ndiyo viongozi wa leo na wa kesho. Tunapaswa kuacha kufikiria kwa viwango vya kawaida na kuanza kupanga maendeleo kwa kuzingatia ushindani wa dunia. Hatupaswi kuridhika na kufanya vizuri ukilinganisha na jana pekee; tunapaswa kuuliza kama tunafanya vizuri ukilinganisha na mataifa tunayoyatamani kufikia.
Lakini kuna somo lingine muhimu zaidi. Kizazi hiki kina taarifa nyingi kuliko kizazi chochote kilichowahi kutokea. Kina uwezo wa kuchambua, kuuliza maswali na kuwawajibisha viongozi kwa kasi kubwa kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali. Hivyo, viongozi wa kesho hawatapimwa kwa uzuri wa hotuba zao bali kwa uwezo wao wa kutekeleza yale wanayoyaahidi.
Ndiyo maana ni muhimu sana kwa viongozi kuwa waangalifu wanapoweka ahadi mbele ya wananchi. Tusijenge matarajio ambayo hatuna uwezo, au dhamira ya kuyatimiza. Kuaminiana kati ya viongozi na wananchi kutajengwa kwa ukweli, uwazi na utekelezaji wa ahadi, si kwa maneno matupu.
Aidha, ushirikishwaji wa wananchi unapaswa kuwa msingi wa utawala wa kisasa. Wananchi wanapopewa nafasi ya kushiriki katika kupanga na kufuatilia maendeleo, wanajenga umiliki wa maamuzi na kuelewa changamoto zinazokabili utekelezaji. Safari ya maendeleo inapokuwa ya pamoja, lawama hupungua na uwajibikaji huongezeka kwa pande zote.
Swali ambalo linaendelea kunijia ni hili: Mafanikio kwa Gen Z ni nini hasa?
SOMA ZAIDI: Tumezungumza na Vijana Kumi Waliojiajiri Kupata Uzoefu Wao. Hiki Hapa Ndicho Walichotuambia
Naamini kwa kizazi hiki mafanikio hayapimwi kwa historia ya tulikotoka pekee, bali kwa ubora wa maisha wanayoishi leo na matarajio wanayoyaona kesho. Wanataka kuona taifa linaloshindana kimataifa, huduma bora zinazofanya kazi kwa ufanisi, fursa za kujiajiri na kuajiriwa, pamoja na uongozi unaosikiliza na kutekeleza.
Huo ndiyo mtihani mkubwa wa viongozi wa kizazi chetu. Si tu kuendeleza mafanikio yaliyopo, bali kujenga Tanzania ambayo kila kijana ataiona, ataigusa na atajivunia, Tanzania ambayo haitalinganishwa na ilivyokuwa jana, bali italinganishwa na mataifa bora duniani, na isimame kwa kujiamini katika ushindani huo.
Thom Mnkondya ni Mwenyekiti wa UVCCM SENET ya Vyuo na Vyuo Vikuu, mkoa wa Songwe. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia munkondyathom@gmail.com au X kama @Thommunkondya. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.