The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Iringa Kwenye Mkakati Wa Kubadilisha Maisha Ya Watoto Wenye Ulemavu

Imani potofu, umasikini na umbali wa shule kumewafanya wazazi wengi kuwaficha watoto wao wenye ulemavu hivyo kuwanyima fursa ya kupata elimu. Serikali ya Mkoa wa Iringa inataka kubadilisha hali hiyo. 

subscribe to our newsletter!

Flora Kanagwe, mama wa miaka takribani hamsini na mkazi wa  Kihodombi, Iringa amekuwa akilea mjukuu wake, Sharon Sadick, 13, aliyetelekezwa na mama yake, Faustina George, siku chache baada ya Faustina kujifungua ikidaiwa kwamba ni baada ya mama huyo kubaini kwamba Sharon ni mlemavu wa viungo.

Bi Kanagwe, anayeishi mwenyewe tu na mjukuu wake, hupiga picha ili kujiingizia kipato. Mara nyingi huwa anaifanya kazi hiyo akiwa na mjukuu wake huyo mgongoni. Nilikutana naye akiwa eneo la Soko Kuu la Mjini Iringa akitafuta wateja wa picha ambao pia hata hivyo huwapata kwa kazi sana. Uso wa Kanagwe si uso wa watu wenye furaha kutokana na changamoto nyingi zinazomkabili, za maisha na malezi pia.

Kwa sauti iliyojaa simanzi na majonzi, Bi Kanagwe anasema kwamba miaka 13 iliyopita alikuwa akimuuguza Fausta katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa ambaye alibahatika kujifungua salama. Lakini wakati wakiendelea kumuuguza Fausta, Kanagwe akashangaa kuona binti yake huyo ametoweka na kutokuonekana tena.

“Mama yake alipoona mtoto anaumwa sana na ni mlemavu aliondoka na mpaka leo hajarudi,” Bi  Kanagwe anasimulia kwa upole wakati wa mahojiano maalumu na The Chanzo. Kanagwe ana amini kutoweka kwa binti yake kunatokana na hali aliyonayo mjukuu wake ya ulemavu wa viungo. Anafafanua: “Mtoto alizaliwa lakini alikuwa anaumwa sana. Kuugua kwake kulimpa wasiwasi binti yangu. [Baada ya kutoweka] nilijaribu kumtafuta bila mafanikio. Nikakata tamaa ikabidi niamue kumlea tu na kwa kweli naamka na kulala naye. Sina mtu wa kumuachia.”

Bibi Flora Kanagwe akibeba mjukuu wake kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake ya kila siku

Mama huyo anaeleza kwamba hali hiyo ilimpelekea kufikiria kuacha shughuli yake inayomuingizia kipato ya kupiga picha. Ili asiache kazi, Kanagwe akaamua kuwa atambeba mjukuu wake mgongoni akienda mitaani kutafuta wateja wa kupigwa picha. Hatua hii aliichukua baada ya kuomba misaada kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali ili mjukuu wake apate angalau chakula na kumudu gharama nyingine za maisha ikiwamo matibabu lakini bila mafanikio. Anasema:  “Ni ngumu sana kupata mahitaji yake nisipopiga picha! Mgongo unauma kwa kumbeba lakini sina cha kufanya. Ikiwa nitapata msaada wa baiskeli ya miguu mitatu pengine itanisaidia, mateso ya kumbeba yatapungua.”

Siku zote Bi Kanagwe aliamini kwamba kama angepewa msaada wa mjukuu wake huyo kufanyishwa mazoezi ya viungo, hali isingekuwa kama ilivyo sasa. Kwa bahati mbaya sana, mama huyo hakufanikiwa katika hilo.

“Mtoto aliendelea kukua, mwanzoni alikuwa halii wala haongei lakini baadaye akaanza kulia kwa sauti hivyo ikabidi niwe nambeba na kutembea nae mitaani ninako piga picha,”  Kanagwe anaiambia The Chanzo. “Nashukuru Mpango wa Serikali wa kuwatambua naamini watanisaidia. Mtoto anahitaji elimu ya kujitambua na kujihudumia pamoja na mazoezi ya viungo. Haya yote sijaweza kumsaidia.”

Sensa ya utambuzi watoto wenye ulemavu

Mjukuu wa Kanagwe ni kati ya watoto 276 wenye mahitaji maalumu waliotambuliwa kupitia sensa iliyoendeshwa na Serikali ya Mkoa wa Iringa uliopo katikati mwa Tanzania ya kuwaibua watoto hao ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kukomesha ubaguzi dhidi yao unaowafanya wawe nyuma katika kupatiwa huduma za msingi kama vile elimu.

Sensa hiyo maalumu ilitokana na ukweli kwamba licha ya uwepo wa elimu inayopinga unyanyapaa kwa kundi la watoto wenye ulemavu nchini Tanzania bado kuna baadhi ya jamii zinazoendelea kuwatenga, kuwatekeleza, au kuwaficha watoto hao kutokana na imani potofu ikiwemo imani kwamba kuzaa mtoto mwenye ulemavu ni laana au mkosi.

Kitendo cha kuficha watoto walemavu kimekuwa ni changamoto kubwa inayowakabili watoto wenye ulemavu Mkoani Iringa kwani imewafanya kukosa haki zao za msingi kama vile kupata huduma za kijamii. Jambo hilo ni kinyume kabisa na Sheria namba tisa ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 ambayo inataka haki sawa kwa watu wenye ulemavu ikiwamo elimu, ajira, nafasi za uongozi na kuboresha miundombinu. Kuficha watoto walemavu pia kunakinzana na Sera ya Elimu ya Tanzania inayotambua kwamba elimu ni haki ya kila mtu bila kujali hali aliyonayo.

Akiongea na The Chanzo wakati wa mahojiano maalumu, Afisa Elimu wa Mkoa wa Iringa Germana Mung’aho anasema kwamba zoezi la kuwafichua watoto wenye uhitaji maalumu lilitokana na ukweli kwamba hakukua na njia nyingine ya kuwasaidia watoto hao mkoani humo zaidi ya kupita kwenye jamii na kuwafichua. Anasema Mung’aho: “Kila mtoto ana haki ya kupata elimu na huduma zote za msingi bila kujali hali yake. Tumeshapita mkoa mzima, tumewatambua  na sasa tunafanya tathmini kujua aina ya ulemavu na huduma anayohitaji mtoto.”

                                     Afisa Elimu wa Mkoa wa Iringa Germana Mung’aho

Sensa hiyo ya kuwaibua watoto wenye mahitaji maalumu katika mkoa wa Iringa iliwalenga watoto wenye umri wa kuanza shule. Lakini kwa mujibu wa Afisa Elimu Taaluma wa Wilaya ya Iringa Vijijini, Vumilia Chaki iligundulika pia kwamba wapo watoto wengine wenye umri mkubwa ambao wamekosa fursa ya kujiunga na shule.

“Ulemavu sio laana wala mkosi,” anasema Chaki, ambaye anasikitika kwamba licha ya hatua hiyo ya Serikali bado baadhi ya wazazi hawajawapeleka watoto wao shuleni. “Mtoto anazaliwa kama mtoto mwingine na anahitaji huduma zote za msingi. Hili limefanya tupite kutafuta hawa watoto.”

Chaki anabainisha kwamba kutokana na kusuasua kwa wazazi kuwatoa watoto wenye ulemavu ili wasome wao kama wadau wa elimu wataendelea na kampeni hiyo mpaka watakapofanikiwa. Hata hivyo, Chaki anajaribu kuwaelewa wazazi ambao wanagoma kuwatoa watoto wenye ulemavu ili waende shule. Kwa mujibu wa maelezo yake, hali duni ya kipato, umbali wa shule na waliko watoto vyote vimechangia kuwafanya baadhi yao kukosa huduma za msingi.

“Unakuta mtoto yupo kilometa tatu kutoka ilipo shule, huna usafiri na wazazi wanakipato duni. Hii inafanya wasiwapeleke licha ya elimu kuwa bure. Ndiyo maana tumeamua kuwatambua ili kuona namna bora za kuwasaidia,” anasema Chaki.

Kipato duni na umbali wa shule ni sababu zilizotajwa na Selina Chuma, mkazi wa Ibumilayinga, Iringa ambaye hakumpeleka shule mtoto wake mwenye ulemavu Justine Gama, 8. Wakati wa mahojiano na The Chanzo, Chuma anasema kutoka sehemu anapoishi mpaka shuleni ni mbali sana na kwamba hana uwezo wa kumpeleka.

“Mtoto akifika shule elimu ni bila malipo, lakini huko shule anaendaje? Atavaa nini? Na chakula je? Kwa hiyo, unaona bora abaki nyumbani tu,” anasema Chuma, huku akibainisha kwamba hafanyi hivyo kwa sababu hampendi mtoto wake. “Mwanangu alizaliwa akiwa mlemavu, hajalemaa ukubwani hivyo kwa kipindi chote cha malezi nimekuwa naye karibu. Sijawahi kumtelekeza, nampenda sana.”

Wadau wataka zoezi liwe la kitaifa, endelevu

Mung’aho ameieleza The Chanzo kwamba sera ya elimu haibagui na ni mkakati wa Mkoa wa Iringa kuhakikisha kwamba wote wanasoma bila pingamizi. Anasema watoto wametambuliwa kutokana na aina yao ya ulemavu kama viungo, uoni, kutosikia, ulemavu wa akili, na wataandaliwa mazingira kulingana na ulemavu wao.

“Kuna watoto wanaweza kusoma elimu jumuishi wakichanganywa na wenzao. Wengine hawawezi kusoma shule za kawaida. Kwa hivyo, hawa wote lazima tuwatambue ili wakasome shule maalum. Hakuna ulemavu ambao hauwezi kupatiwa huduma kulingana na aina yake,” anasema Mung’aho.

Kinachofanyika kwa sasa kwa mujibu wa Mung’aho ni kuandaliwa kwa mazingira ya kuwapokea watoto ambao tayari wameshaibuliwa ili waweze kusaidiwa kulingana na ulemavu wao. Anasema: “Kama ni miundombinu inakarabatiwa na wale wenye mahitaji maalum wanapelekwa shule maalum. Tunataka kila mtoto asaidiwe.” Mkakati mwingine unaotekelezwa ni kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na upatikanaji wa wataalamu watakaosaidia watoto hao kupata ujuzi stahiki.

Kumekuwa na wito wa kufanya zoezi la kuwatambua watoto wenye mahitaji maalumu kuwa la kitaifa na endelevu huku wasomi kama Jimson Sanga ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Iringa akitaka kuwe na bajeti inayowagusa watoto wenye mahitaji maalum mapema kabisa ili wakishatambuliwa wasibaki kuwa mzigo wa wazazi.

Tumaini Msowoya ni mwandishi wa habari wa kujitegemea wa habari za watoto na kijamii aliyepo Iringa, Tanzania. Anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni msowoyatuma@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatile, au ni mwandishi wa habari wa kujitegemea unayetaka kuandikia The Chanzo, wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts