Saada Osman, mjane wa aliyekuwa Katibu wa Bunge Yasin Osman, amemuangukia Rais John Magufuli akimtaka amsaidie kurejesha umiliki wa kiwanja namba 578 kilichopo Upanga, Dar es Salaam ambacho anadai kutapeliwa na rafiki yake wa karibu. Saada, 75, amelazimika kutoa wito huo kwa Rais Magufuli baada ya juhudi zake za kupigania haki yake hiyo kwenye mamlaka za chini kugoma kuzaa matunda kwa kipindi cha takribani miongo miwili sasa.
“Kila nikiuliza [kuhusu kesi yangu] naambiwa kuna wakubwa wanahusika,” Bi Saada, mama wa watoto watatu anasema kwa masikitiko wakati wa mahojiano maalumu na The Chanzo nyumbani kwake, Mtaa wa Mindu, Upanga. “Kwangu mimi wakubwa ni wawili. Mkubwa wa mbinguni ni Mungu na mkubwa wa hapa duniani ni Rais. Sasa kama hao wote wateule wa Rais wanashindwa kulitatua [suala langu], basi namuomba Mheshimiwa Raisi Dk John Pombe Magufuli unisaidie. Kwa sababu [Mwendesha Mashtaka] ni mteule wako ambaye hakuna mwengine anayeweza kuingilia, waziri [William] Lukuvi ni mteule wako, [Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai], [Mkuu wa Jeshi la Polisi], hawa wote ni wateule wako. Sijuwi wanafanya mambo hayo kwa msukumo wa aina gani.”
Sakata la Bi Saada linaanzia mwaka 1973 baada ya aliyekuwa mumewe kuhamishwa kikazi kwenda Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza lakini akafariki miaka minne tu baadae, mwaka 1977 akimuachia Bi Saada watoto watatu wenye miaka saba, mitatu na miwili. Mazishi ya Yasin Osman, aliyekuwa Katibu wa Bunge chini ya Spika Adam Sapi Mkwawa, yalifanyika Dar es Salaam na punde tu baada ya kumzika mumewe Bi Saada akarudi London, Uingereza.
Saada anaiambia The Chanzo kwamba alilazimika kurudi London kwa sababu huko alikuwa ameshaanza kazi katika Commonwealth Parliamentary Association na watoto wake wawili walikuwa wameshaanza shule za Serikali za kusoma bure. Anasema: “Niliona bora niendelee na kazi yangu kule ili niweze kusomesha watoto. Nilikuwa nafahamu ningerudi Tanzania, ningekuwa peke yangu na watoto [na] nisingekuwa na uwezo wa kuwaendeleza kimasomo.”
Wosia wa mirathi
Kabla ya kufariki, Yasin Osman aliandika wosia akibainisha kuwa warithi wa mali yake ambayo ni kiwanja Namba 578 kilichopo Mtaa wa Mindu, Upanga, Dar es Salaam, karibu na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, chenye hatimiliki Na. 186211/6 wawe ni watoto wake. Kwa sababu watoto walikuwa wadogo, Saada Osman, mama yao, akalazimika kuwa mlezi wa mali hiyo ili aje awape watoto wakishakuwa wakubwa. Lakini watoto hao wameshakuwa na Bi Saada ameshindwa kuwapatia mali walioachiwa na baba yao kwa sababu mali hiyo haipo tena mikononi mwake. Amedhulumiwa.
Saada anamshutumu rafiki yake wa zamani ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kisheria kuhusika na utapeli huo wa mali ya watoto wake. Saada na rafiki yake huyo walikuwa marafiki wa karibu wakati wakifanya kazi katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kabla ya yeye Saada kwenda Uingereza. Walikuwa wakiaminiana sana kwenye mambo mengi na ni katika mazingira hayo basi Saada alipohitaji mtu wa kumsaidia kusimamia kiwanja chake hicho alikwenda kwa rafiki yake huyo.
Hata alipoondoka kwenda Uingereza baada ya kumzika mumewe, Saada hakuondoka na nyaraka za nyumba. Zote, ikiwemo hati miliki na wosia, aliziacha kwa rafiki yake huyo. Lakini ili rafiki huyo awe na nguvu ya kisheria kufanya kile Saada anamtaka afanye, ilibidi Saada ampe kitu kinachojulikana kwa kimombo kama Power of Attorney. Kwa lugha rahisi hii ni nyaraka ya kisheria inayompa mtu mwengine mamlaka ya kufanya kitu au maamuzi kwa niaba yako. Saada alimpatia rafiki yake huyo nyaraka hiyo mnamo Januari 19, 1988.
Lakini badala ya kutumia nyaraka hiyo kufanya kama Bi Saada alivyotaka, rafiki yake huyo aliitumia kujipa umiliki wa mali isiyokuwa yake na kusababisha kesi ambayo imeenda kwa takribani miaka 20 bila kupatiwa ufumbuzi. Saada anasimulia kwa uchungu: “Iliniuma sana sana kwa sababu [rafiki yangu] ana uwezo mkubwa, na mimi alikuwa anazijua shida zangu nnavyopambana kulea watoto peke yangu London mpaka hapa nilipofikia. Kwanza sijaweza kuamini kabisa kama angeweza kufanya jambo kama hilo.”
Utata Power of Attorney
Saada alifahamu kwa mara ya kwanza kwamba umiliki wa kiwanja hicho umebadilika mwaka 1997 lakini alikuja kuthibitisha mwaka 2005 alipokuja Tanzania na kujionea mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika kiwanja hicho bila ya yeye kuwa na taarifa yoyote. Pamoja na mambo mengine, Saada aliona kwamba kulikuwa na nyumba mpya zimejengwa kwenye kiwanja na kulikuwa na watu tayari wanaishi. Pili, kiwanja sasa kilikuwa kimegawanywa sehemu mbili, 578A na 578B. Baada ya kufuatilia sana katika Wizara ya Ardhi Saada aligundua kwamba rafiki yake, kwa kutumia Power of Attorney, mnamo Januari 4, 1996, alikiuza hicho kiwanja kwa shilingi milioni 18 kwa watu sita tofauti ambapo na yeye, Saada, pia alipewa nyumba moja, hivyo kuwa na milki ya 1/7 ya kiwanja.
Changamoto anayokabiliana nayo Saada ni kwamba kila anapokwenda kutafuta haki yake hiyo anaambiwa kwamba hawezi kusaidiwa kwa sababu alimruhusu rafiki yake huyo kufanya aliyoyafanya kwa kumpa Power of Attorney. Lakini Bi Saada anakataa, akisema kwamba mambo yote yaliyofanyika kuhusiana na mali yake yamefanyika kinyume na sheria na yeye alimruhusu rafiki yake huyo kufanya mambo yanayokubalika tu kisheria.
“Kweli nimempa mamlaka yote kwa sababu nilimuamini, sikufikiria kwamba angekuja kunitapeli,” anasema Bi Saada. “Lakini vile vile, Power of Attorney hii inasema kuwa mimi nitakubali vitendo vyote ikiwa vimefanyika kwa mujibu wa sheria. Kufuata kanuni na sheria za nchi. Lakini mambo yote aliyofanya yeye yamefanyika kinyume na sheria: kauza mali bila kutoa mikataba, jambo hilo halikubaliki, ameendeleza ujenzi bila kuomba vibali kutoka mamlaka husika, haikubaliki.”
Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) pia iligundua kwamba Power of Attorney hiyo haikukidhi vigezo vya kumruhusu rafiki yake Saada kufanya mambo aliyoyafanya. Kwenye barua yake kwenda kwa Waziri wa Ardhi William Lukuvi ambayo nakala yake The Chanzo imeiona, TAKUKURU inasema Power of Attorney hiyo ni batili kwani inakosa sahihi ya donor (mchangiaji) na donee (mchangiwa) na kuitaka Wizara iingilie kati.
Wakati wa mahojiano na The Chanzo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo alisema kwamba kwa mujibu wa uchunguzi wao, TAKUKURU ilibaini mapungufu kwenye hatua ya Wizara ya Ardhi ya kufanya uhawilisho wa sehemu ya kiwanja kilichouzwa bila ya kujiridhisha vya kutosha namna kiwanja hicho kilivyouzwa. Mbungo anasema: “Kwa sababu kumbukumbu za [Wizara ya Ardhi] hazikuwahi kuonyesha akina Saada kupeleka ridhaa ya kuhawilisha miliki ya ardhi hiyo.”
Barua ya TAKUKURU kwenda kwa Waziri Lukuvi iliandikwa mnamo Agosti 26, 2019 na The Chanzo inafahamu kwamba mpaka muda wa kuandaa habari haikuwa imefanyiwa kazi. Mbungo anaiambia The Chanzo: “Kwa bahati mbaya sana hakuna sheria inayomlazimisha anayeshauriwa na [TAKUKURU] kutekeleza ushauri unaotolewa na wataalamu wa rushwa. Inategemea [na] utashi wa taasisi kufuata huo ushauri. Naweza kusema hii ni moja ya udhaifu wa sheria tulizonazo.”
The Chanzo ilipomuuliza Waziri Lukuvi kuhusiana na suala hilo, alituelekeza kwa Kamishna wa Ardhi wa mkoa wa Dar es Salaam Idrissa Kayera ambaye aliomba muda wa kufuatilia suala hilo na kurudi kwetu lakini mpaka muda wa kuandaa habari hii alikuwa hajafanya hivyo.
“Wizara ya Ardhi lazima, lazima wawe makini, wasikilize vilio vya wananchi,” anasema Bi Saada. “Maanake 2015, kabla ya uchaguzi, Waziri Lukuvi aliitisha mkutano pale wizarani, tukaenda. Mimi hata nilioneshwa kwenye taarifa ya habari ya TBC1 na Channel 10. Nimewaambia matatizo yangu, nikamkabidhi [Waziri] nyaraka zangu ambaye alimpa nyaraka hizo Waziri Angela Kairuki, Kairuki akampa hizo nyaraka Kamishna wa Ardhi [Nathaniel] Mathew, akatuambia tumpe miezi mitatu, hiyo ilikuwa kabla tu ya kampeni za uchaguzi wa 2015. Mheshimiwa Lukuvi aliporudishwa tena wizarani nikamwandikia tena barua ya kumkumbusha ahadi yake. Lakini mpaka leo, 2021, hakuna chochote kilichofanyika.”
Wito kwa mamlaka za nchi
Hakuna jengo la Serikali ambalo Bi Saada hajaliingia. Ameshakutana na kila aina ya madhila yanayowakuta watu kama yeye wanaopigania haki zao. Ameshafukuzwa kutoka ofisi ya Serikali aliyodhani atapokelewa na kusikilizwa. Mahakamani nako kesi zake kadhaa zimetupiliwa mbali.
“Nimeshakaa vikao na DCI mara mbili anasema [kwenye kesi yangu] hakuna jinai ya aina yoyote. Na jalada [la kesi yangu] limefungwa, lakini hivi karibuni lilifunguliwa tena, na upelelezi ulikuwa unakwenda vizuri kitengo cha fraud (utapeli) lakini kwa bahati mbaya DCI amezuia upelelezi huo kuendelea. Sifahamu kwa sababu gani,” anaeleza Bi Saada.
The Chanzo ilimtafuta DCI Robert Boaz kutaka kufahamu kwa nini ofisi yake inadhani hakuna jinai kwenye kesi ya Bi Saada lakini akakataa kujibu maswali yetu akimtaka mwandishi afike ofisini kwake. Hata hivyo, alipoulizwa ni lini na saa ngapi atakuwepo ofisini hapo ili mwandishi aende kumuona, DCI Boaz hakujibu na hivyo kufanya kikao hicho kutokufanyika.
Shaaban Rajabu Khatibu ni msaidizi wa Bi Saada katika harakati zake za kutafuta haki yake. Shaaban ni mzoefu wa kufuatilia migogoro ya ardhi akiwa ni moja kati ya wahanga waliowahi kudhulumiwa ardhi zao na kumchukua miaka zaidi ya 10 kupigania urudishwaji wa mali yake. Anaeleza nini cha kufanya kama mamlaka za Serikali zinataka kumsaidia Bi Saada: “Kwanza kabisa, mamlaka hizi ambazo ni za kiuchunguzi, kwa nini wameshindwa kwenda kuchunguza wizara ya ardhi, ile Power [of Attorney] ilisajiliwa kwa misingi ipi? Kanuni zilifuatwa? Na aliyesajili ile Power of Attorney ni nani?”
Wito huu unaungwa mkono na Fahma Osman, mtoto mkubwa wa Bi Saada ambaye anaziomba mamlaka za Tanzania kuingilia kati kesi ya mama yake ili waweze kupata haki yao. Anasema: “Nyaraka mbili zinazomtesa mama yangu zilipaswa kuchunguzwa kwa umakini na polisi na TAKUKURU kubaini nani kasajili nyaraka hizo na nani kauza mali yetu. Lakini wameshindwa kufanya hivyo. Power of Attorney haikukidhi vigezo vya kusajiliwa kitu ambacho kinafanya nyaraka ya uhawilishaji mali kuwa haramu. Mama yangu atatimiza miaka 76 mwishoni mwa mwezi huu [Februari, 2021], mimi na ndugu zangu tunaiomba wizara [ya ardhi] kumsaidia mama yangu kutatua jambo hili kulingana na wosia na hati miliki.”
Mamlaka hazisaidii wanyonge
Uzoefu wa kupigania haki yake umemfundisha Bi Saada mambo mengi na kama angepata nafasi ya kukutana na Rais Magufuli, hiki ndicho angemwambia: “Mheshimiwa Rais, naona kama wateule wako – naweza kusema hiki? – wateule wako labda, sijuwi nitumie neno gani, wanakudanganya. Kwa kweli hawasaidii wanyonge, maanake hata ukijirabu kuonana nao na kuwaeleza shida zako zinaingia sikio moja zikatoka sikio la pili, yakaishia hapo hapo. Husikilizwi kwa makini na wakafuatilia na wakamsaidia mzee, myonge. Hamna hiyo kabisa.”
Si mamlaka za Serikali tu ambazo zimekuwa kikwazo katika harakati za Bi Saada kupata haki yake. Shida zake zimemgeuza mtaji kwa baadhi ya wanasheria na waandishi wa habari wasio na maadili. Hali imekuwa mbaya zaidi kwa waandishi wa habari ambao zaidi ya mara moja wamemtaka atoe pesa kubwa ili waweze kutoa habari yake.
“Kuna gazeti moja tulikuwa tunakwenda vizuri na mhariri, mara ya mwisho akaniletea jumbe za simu kama za kutatanisha hivi, kutaka nionane naye nje ya ofisi, mimi nikamkubalia, nikamwambia sawa tukutane wapi na saa ngapi, baada ya hapo tena akaingia mitini. Sasa mimi sijuwi azma yake ilikuwa nini,” anasema Bi Saada.
Lakini pamoja na yote haya, Bi Saada ameamua kusimama imara katika kupigania haki yake akiamini kwamba kama ni haki yake basi ataipata tu. Huu ndiyo ushauri wake kwa Watanzania wote ambao wanapigania haki zao muda huu: “Wito wangu kwa Watanzania, msivunjike moyo wala msiache kupigania haki zenu. Kwa kuwa bado mko hai, mnavuta pumzi, mnaweza kwenda, piganieni haki zenu na msitoe rushwa yoyote. Mimi naambiwa mambo yangu hayaendelei kwa sababu sitoi rushwa. Mimi nasema tena na tena sitotoa rushwa hata siku moja kwa sababu mimi napigania haki yangu na kama ni haki yangu siku moja itafika Insha’Allah nitaipata.”
Unaweza kuangalia mahojiano na Bi Saada hapa
Kwa miaka zaidi ya 20, Saada Osman amekuwa akipambana kuhakikisha anapata haki yake bila mafanikio. The Chanzo imefanya habari hii kumsaidia kupata haki yake. Kama unafahamu kitu chochote kuhusiana na kesi yake kinachoweza kusaidia upatikanaji wa haki yake au unafahamu mtu mwengine yeyote anayepitia changamoto kama hiyo, basi wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kuona namna tunavyoweza kushirikiana katika kupaza sauti.