Kigoma. Katika Kijiji cha Simbo kilichopo Wilaya ya Kigoma iliyopo mwambao mwa ziwa Tanganyika, simulizi ya mabadiliko ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira inajipambanua kupitia juhudi za mbunifu mmoja ambaye ameamua kutazama mabaki ya mchikichi kwa jicho la kitofauti.
Wakati wengi wakiona makapi na maganda ya ngazi kama takataka zinazopaswa kutupwa, kwa Hassan Kilanoza, hayo ni malighafi inayobadilisha maisha ya mamia ya vijana na baadhi ya wanawake mkoani hapo.
Kilanoza, mkulima mbobevu aliyekaa katika kilimo cha mchikichi kwa miaka 28, sasa amegeuka kuwa tunu ndani ya halmashauri hiyo baada ya kuasisi mfumo wa uchumi rejeshi unaotumia kila sehemu ya zao la mchikichi bila kupoteza kitu chochote.
Kupitia kiwanda chake kidogo ambacho The Chanzo imekitembelea ameweza kutafuta kuwa suluhisho la changamoto ya nishati na mabadiliko ya tabianchi halihitaji teknolojia ya anga za juu, bali ubunifu na uthubutu.
Chikichi inavyosarifiwa
Kilanoza anaeleza kuwa kwa upande wake zao la mchikichi hutengeneza bidhaa 14 na hivyo hakuna kitu wanatupa kama takataka kwa kuwa mchakato wa uzalishaji kiwandani kwake kila hatua inazaa bidhaa mpya.
Anasema huanza na tunda la mchikichi, linalojulikana kama ‘ngazi’ ambalo baada ya kukamuliwa kwa ajili ya kupata mawese, mabaki yanayopatikana kama mise, makapi, na maji ya mnyemwe (maji machafu ya mnyemwe) hayadhuru mazingira.
“Maji hayo yanatumika kutengenezea mbolea na gesi (biogas), mise ikikamuliwa zaidi hutoa mafuta ya kutengenezea sabuni za kienyeji maarufu kama ‘sabuni za Kigoma’ pamoja na sabuni za kuoga ambazo tuauza kwa shilingi 1,000 kwa mche na kipande,” anasema Kilonaza.
Katika mchakato huo makapi hutumika kuwashia moto, maganda ya mise hutumika kama kuni na hivyo shughuli zote zinazohitaji moto hapo kiwandani hutumia maganda ya mise kupikia ikiwemo kuchemsha ngazi na mafuta.
“Hata haya makapi na maganda ya miwa tunayatumia kama nishati ya kuendeshea shughuli za kiwandani. Badala ya kutumia kuni, tunatumia maganda hayo kuwasha moto kwa ajili ya kuchemshia ngazi na mafuta, hivyo kusaidia kupunguza matumizi ya kuni.”
Utunzaji wa Mazingira
Kilanoza anatumia maganda ya mchikichi na taka nyingine ngumu kuzalisha mkaa banifu ambao una uwezo wa kudumu kwa zaidi ya saa 12 bila kuzimika, hauna moshi, na unauzwa kwa bei rafiki ya shilingi 400 tu kwa kilo moja.
Takwimu za kutoka Global Forest Watch, Tanzania inaonesha kuwa zaidi ya hekta 2,000,000 za misitu zimepotea kati ya mwaka 2001 hadi 2023 hii ni kutokana na kuongezekana kwa shughuli za kibinaadamu, ukataji wa miti na athari za mabadiliko ya tabianchi.
SOMA ZAIDI: Mwalimu wa VETA Kigoma Abuni Kifaa cha Kusaidia Wenye Usikivu Hafifu
Wataalamu wa mazingira wanasema kwamba uzalishaji wa gunia moja la mkaa wa kawaida wa kilo 100 unahitaji kukatwa kwa miti kati ya mitatu hadi mitano.
Ila kwa upande wa mkaa banifu uzalishaji wa tani 10 wa mkaa huo kwa siku, anasadikiwa kuokoa kati ya miti 300 hadi 500 kila siku ambayo ingekatwa kuzalisha mkaa wa kawaida, huu ni mchango mkubwa katika kuifanya Kigoma kuwa ya kijani na kulinda vyanzo vya maji, ikiwemo Ziwa Tanganyika.
“Kwa uzalishaji huu wa mkaa banifu, tunapunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa mkaa wa kawaida unaochochea ukataji wa miti. Hivyo, teknolojia hii inasaidia kuhifadhi misitu, kulinda mazingira na kuhakikisha vyanzo vya maji vinaendelea kuwa salama.” anasema Kilonoza.
Ajira na Mafunzo kwa Jamii
Kupitia ubunifu wake, Kilanoza ameajiri watu 15 wakiwemo wanawake 10 na wanaume watano ujuzi ambao anautoa hapo umewafikia vijana zaidi ya 108 ambao sasa nao wamekuwa walimu wa kusambaza ujuzi wa kutengeneza mkaa banifu na gesi kwa ada ya shilingi 50,000 hatua inayopunguza wimbi la vijana wanaokaa mtaani wakisubiri ajira za Serikali au kujihusisha na tabia hatarishi.
Katika miaka miwili iliyopita, kupitia mradi wa VOICES unaofadhiliwa na Shirika la Catholic Church Services (CRS) amefanikiwa kuwa mwalimu kwa jamii nzima ya Mkoa wa Kigoma akiwafundisha vijana, wanawake na wanaume juu ya uchumi rejeshi ambapo amefanikiwa kuwa na madarasa ya watu wanaozidi 700.
Mageuzi ya Teknolojia
Mbali na nishati, Kilanoza amefanya mageuzi ya kiufundi ambapo ametengeneza mashine 60 za kisasa za kuchakata ngazi na mise kwa ajili ya wakulima wenzake.
Anasema hatua hiyo imetatua changamoto ya mawese kuharibika kwa haraka kwani wananchi wanadai kuwa mashine za asili zilikuwa zikiozesha mawese na kupunguza ubora wa bidhaa sokoni.
“Tumeboresha teknolojia kwa kutengeneza mashine za kisasa za kuchakata ‘ngazi’ na mise, na tayari tumetengeneza mashine zaidi ya 60 kwa ajili ya wakulima wenzetu,” amesema Kilanoza.
Kwa kueneza teknolojia hii, amesaidia kuinua ubora wa mafuta ya mawese yanayozalishwa katika eneo lake na ndani ya mkoa ambao sehemu kubwa ya wakazi wake wanategemea zao la mchikichi kama zao la biashara na kujipatia kipato.
Mchango wa wadau na Serikali
Licha ya kuungwa mkono na jamii, Serikali na wadau mbalimbali wanaendelea kumuunga mkono Kilanoza katika kukuza ubunifu wake. Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Kigoma, Ramadhan Mpasiwakomu anasema anaendelea kupambana kumtafutia fursa za kifedha kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili aweze kukuza shughuli zake za kutunza na kuhifadhi mazingira.
“Tunajitahidi kumtafutia fursa za kifedha kupitia Benki ya Kilimo ili aweze kuongeza uzalishaji na kuendeleza ubunifu wake,” amesema Mpasiwakomu wakati akizungumza na The Chanzo.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, George Vangesauli, anasema humshirikisha katika maonyesho mbalimbali ya kilimo na biashara, ikiwemo Sabasaba, kwa lengo la kutangaza ubunifu wake na kufanya ujulikane zaidi kitaifa na kimataifa.
“Tumekuwa tukimshirikisha katika maonyesho kama Sabasaba ili kupata nafasi ya kuutangaza ubunifu wake na kuwafikia watu wengi zaidi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi na serikali inamtambua na kuthamini mchango wake,” amesema Vangesauli.
SOMA ZAIDI: Mazungumzo na Mchimbaji Mdogo wa Madini Kigoma, Tanzania: ‘Bado Hatujatambuliwa Ipasavyo’
Wadau wa maendeleo wanaendelea kuona fursa za kusaidia jamii kupitia ubunifu unaolenga kutatua changamoto za mazingira na kuongeza kipato. Simon Mwanjera kutoka Catholic Relief Services (CRS) anasema kupitia mradi wa VOICES, Kilanoza anatarajiwa kupata ruzuku itakayomwezesha kujenga kiwanda kikubwa zaidi cha mkaa banifu.
“Tunamuunga mkono kupitia mradi wa VOICES ili aweze kupata ruzuku ya kujenga kiwanda kikubwa zaidi, kuongeza uzalishaji na wakati huo huo kusaidia kuondoa taka za mchikichi zinazotokana na shughuli za kilimo katika kijiji cha Simbo na maeneo ya jirani,” amesema Mwanjera.
Matarajio na ndoto zake
Licha ya mafanikio haya makubwa, safari ya Kilanoza bado inakabiliwa na changamoto ya mtaji wa kutosha ikiwemo fedha za kununua mashine nyingi zaidi zitakazomwezesha kufanya utengenezaji wa mkaa akibainisha kuwa mashine moja ya kisasa inagharimu zaidi ya shilingi milioni 10.
“Tunahitaji mashine zaidi ili kuongeza uzalishaji, lakini mashine moja ya kisasa inagharimu zaidi ya shilingi milioni 10, hivyo ni changamoto kubwa kwetu kuweza kuzinunua kwa uwezo wetu wenyewe.” Kilanoza anabainisha.
Changamoto nyengine ambayo inaendelea kwa sasa ni suala la kukatika kwa umeme mara kwa mara anadai inarudisha nyuma kasi ya uzalishaji, jambo linalomlazimu wakati mwingine kuuza kwanza kidogo alichozalisha ili kupata fedha za kuendelea na mzunguko mwingine.
Adela Madyane ni mwandishi wa habari anapatikana mkoani Kigoma. Unaweza kumpata kupitia vek3cutes@gmail.com