Unaposikia habari kwamba mtu fulani mwenye ulemavu wa ngozi au albino ameuwawa kwa sababu za kishirikina, huku wauwaji wake wakidhani kwamba wanaweza kutumia viungo vyake kufanikisha malengo yao ya kibiashara, unaweza kudhani hiyo ni habari tu ambayo haina uhalisia. Lakini kwa Maria Dismas Charles, mwanaharakati wa watu wenye ulemavu wa ngozi, hiki ni kisa alichowahi kukutana nacho yeye mwenyewe na kuponea chupu chupu.
Maria, 45, alikuwa anaongea na The Chanzo kuhusiana na harakati zake na changamoto anazokabiliana nazo kuelekea kilele cha sherehe za Siku ya Kimataifa ya Mwanamke inayosherehekewa Machi 8 kila mwaka. Kauli mbiu ya sherehe za mwaka huu ni Choose to Challenge, na shughuli kadhaa zinategemewa kufanyika maeneo mbali mbali duniani ikiwemo Tanzania kama sehemu ya kuadhimisha siku hiyo.
Mkazi huyo wa Dar es Salaam ambaye alilazimika kujiingiza kwenye uanaharakati wa kupigania haki za watu wa jamii yake kutokana na madhila makubwa wanayokutana nayo kwenye maisha yao ya kila siku anaileza The Chanzo kwamba licha ya watu wenye ulemavu wa ngozi kukabiliana na changamoto lukuki kwenye maeneo kama elimu na familia pia kumekuwa na changamoto ya watu hao kuonekana kama vyanzo vya utajiri kwa baadhi ya watu.
Mama huyo wa watoto wawili anasimulia kisa ambacho anasema hawezi kukisahau kwenye maisha yake ambapo aliponea chupu chupu kuangukia kwenye mikono ya watu wasiokuwa na nia nzuri waliotaka kumtumia kujipatia utajiri. Maria anasema kwamba akiwa na kiongozi wake walifunga safari kuelekea Mkoani Kigoma kwa lengo la kuhuisha matawi ya shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu mkoani humo.
‘Nilikuwa na hofu kubwa’
Kipindi hicho ilikuwa ili ufike Kigoma ni lazima abiria walale Kahama, Shinyanga. Maria na kiongozi wake walifikia kwenye nyumba moja ya kulala wageni na kukutana na akina baba kadhaa wakipata ulabu. Wakati Maria anaingia kwenye nyumba hiyo, mmoja ya wale waliokuwa wakipata ulabu akasema, “Albino huyu amekuja kulala humu.” Maria anasema alishtuka na moyo kuanza kumuenda mbiyo kwa kasi ya ajabu.
“Sasa ile nimetoka ili nimfuate mwenzangu kujua ni wapi amelala nikasikia mmoja wa wale wanaume anasema, ‘Yaani huyu dada ni lazima nimpate na nikishampata lazima niende kwa mtaalamu wangu nikachukue dawa,’” Maria anasimulia. “Baada ya kusikia yale maneno niliogopa sana nikamfuata kiongozi wangu na kumuambia kuwa hapa siwezi kulala. Sikumueleza sababu ya kweli ya kutaka kuondoka bali nilimwambia tu sikupapenda na hivyo tutafute sehemu nyengine. Nilijua kama ningemuambia ukweli angewafuata na ingekuwa tafrani hivyo tukaondoka kwenye ile nyumba huku nikiwa na hofu kubwa.”
Hii ilikuwa ni mwaka 2013, kipindi ambacho mauwaji ya watu wenye ulemavu katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikiwemo Shinyanga, yakiwa yameshika kasi. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kati ya mwaka 2000 na 2016, jumla ya watu wenye ulemavu 75 walikuwa wameuwa nchini Tanzania kwa sababu za kishirikiana zinazowahusisha watu hao na upatikanaji wa utajiri. Mauaji haya kwa sasa yamepungua kutokana na juhudi za Serikali za kuyakomesha, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua waganga wa kienyeji wanaohusika na mauaji hayo kwa kuwakamata na kuwafungulia mashtaka.
Hii si changamoto pekee
Wakati hii ikiwa ni changamoto kuu inayowakabili watu wenye ulemavu wa ngozi, Maria anasema kwamba hiyo siyo changamoto pekee. Mwanaharakati huyo anasema kwamba mbali na kisa hicho cha kunusurika kutekwa, pia amekuwa akikumbana na changamoto nyengine nyingi zinazotokana na mitazamo hasi waliyonayo baadhi ya wanajamii kuhusu watu wenye ulemavu.
Ukiachana na unyanyapaa aliowahi kukutana nao katika kupangisha chumba, ambapo baba mwenye nyumba alimnyima chumba kwa sababu ya ulemavu wake, kati ya vitu ambavyo vimeuumiza moyo wa Maria sana katika maisha yake ni kitendo cha mpenzi wake na baba wa watoto wake wawili kushindwa kufunga naye ndoa kutokana na shinikizo kutoka kwenye familia ya upande wa mwanaume.
“Familia yake ilinikataa, hasa dada yake alisimama kidete na kumuuliza kwamba amekosa wanawake wa kuoa mpaka aje anioe mimi,” anasimulia Maria anayefanyakazi na Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi, unaoratibiwa na shirika la Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT). “Basi yule mwanaume aliamua kuniacha na watoto wangu na nimeendelea kuwalea mpaka leo hii. Lakini baba wa watoto wangu alinipenda sana.” Maria amekuwa akiishi mwenyewe tangu wakati huo baada ya mtu aliyempenda kushindwa kuishi naye.
Maria anakiri kwamba zama hizi si kama zile za yeye alizokulia, akibainisha juhudi kadhaa ambazo Serikali na wadau wengine wamekuwa wakizichukua kubadilisha mtazamo wa jamii juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi, kitu ambacho anasema kimesaidia kwa kiasi kikubwa maisha ya watu wa kundi hilo kuboreka.
Maria pia anajivunia ujasiri ambao watu wenye ulemavu wa ngozi, hususani wanawake, wameweza kuuonesha, kitu ambacho anasema kimeendelea kuithibitishia jamii kwamba watu wenye ulemavu wa ngozi wana ujuzi na vipawa sawa na watu wasiokuwa na ulemavu huo na hivyo kuwafanya wapewe haki na heshima wanayostahiki.
“Wakati wetu changamoto zilikuwa nyingi sana kwani watu wenye ulemavu walikuwa hawapewi fursa kama ambavyo sasa hivi inafanyika,” anasema Maria. “Lakini hivi sasa wanawake wenye ulemavu wamekuwa mstari wa mbele katika mambo mbalimbali na Serikali imetambua mchango wao. Hiki ni kitu cha kujivunia.”
Jaqueline Victor ni mwandishi wa habari za afya na kijamii anayepatikana Dodoma, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: jaquelinevictor88@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatilie, au ni mwandishi wa habari wa kujitegemea unayetaka kuandikia The Chanzo, wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.