Tanzania imefikwa na msiba mzito sana. Hili ni tukio la kihistoria la kuondokewa na Rais wakati angali yupo madarakani, jambo ambalo limeipa nchi huzuni na simanzi, lakini pia wananchi na Serikali yenyewe imepatwa na ‘ganzi’ kwa sababu tukio lenyewe halikutarajiwa na hapakuwa na maandalizi ya nini kifanyike. Tunaomboleza na kushiriki ratiba za kumuaga mpendwa wetu Rais John Magufuli kama zinavyotolewa na Serikali, lakini wakati huo huo lazima tujadili mambo mengine ya nchi. Na jambo kubwa kwa sasa ni namna ya kisheria na kisiasa ya kuhamishia madaraka ya nchi mikononi mwa aliyekuwa Makamu wa Rais, na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Katika kile walichokiita mwongozo katika uundwaji wa Serikali mpya kufuatia Mama Samia kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, Chama Cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kilitoa ushauri wa kitaalamu mnamo Machi 19, 2021, kwa Serikali ambao umeibua mjadala mzito sana baina ya wanazuoni na wachambuzi wa masuala ya kisheria na kisiasa. Kwa kifupi, TLS walisema kwenye andiko lao hilo kwamba baada ya usomaji wa pamoja wa ibara ya 51(2) na ibara ya 57(2)(e) za Katiba, imewafanya waseme “kwa kujiamini” kwamba mara tu baada ya Rais kuapishwa anatakiwa kumteua Waziri Mkuu ndani ya siku 14 tokea kuwa kwake Rais. Ibara ya 51(2) inazungumzia uteuzi wa Waziri Mkuu na ibara ya 57(2)(e) inahusu kiti cha Waziri Mkuu kuwa wazi kutokana na kujiuzulu au kwa sababu nyengine yoyote ile. Kwa mujibu wa Baraza la Uongozi la TLS, ‘sababu nyengine yoyote’ katika muktadha wa sasa ni kufariki kwa Rais aliyekuwepo madarakani na kusimikwa kwa aliyekuwa makamu wake.
Mjadala huu umekuwa mpana sana kiasi cha kumuibua Waziri wa Katiba na Sheria Dk Mwigulu Nchemba kwa ajili ya kutolea ufafanuzi suala hili. Akiandika katika ukurasa wake binafsi wa Instagram Machi 20, 2021, Dk Nchemba alisema kwamba hakuna ibara yeyote ya Katiba iliyokiukwa mpaka sasa, na kwamba Ibara ya 57(2)(e) ya Katiba haiwezi kutumika katika muktadha huo. Wadau wengine kadhaa wa masuala ya kisheria wameunga mkono hoja ya Dk Nchemba. Kwa bahati mbaya, hata hivyo, naona kama vile wadau hawa hawajalitazama suala hili kwa mrengo wa kitaaluma na badala yake wamekuwa wepesi kushutumu bila kuwa na msingi wowote. Wanasisitiza zaidi uungwana kuliko jinsi jambo linavyopaswa kufanyika kisheria na nadhani kwa kiasi fulani hoja za namna hii zinapoteza mantiki ya mjadala.
Mianya ya kikatiba
Kwa tathmini yangu, mwongozo wa TLS unagusa ‘matobo’ yaliyopo katika Katiba, ingawa TLS wenyewe hawajaeleza kinagaubaga matobo hayo. Unaweza kudhani TLS walifanya hivyo kwa makusudi kwani pale unapokusudia kutoa mwongozo wa kisheria hupaswi kuikosoa sheria yenyewe. Matobo haya ni pamoja na Ibara ya 3-(3)(a) inayoeleza kuwa Waziri Mkuu atakoma kushika madaraka mpaka siku Rais Mteule ataapa kushika kiti cha urais. Swali la kujiuliza hapa ni je, fasili ya kiongozi anayetajwa katika Ibara ya 37-(5) ina shabihiana na ile ya Rais mteule? Unaweza kujibu la hasha! Lakini TLS wamejibu ndiyo, na kwa maoni yangu pande zote zipo sahihi. Na hili ni tobo la Katiba kwa kuwa haijafafanua kwa kuhusianisha au kutenganisha hizi fasili.
Wale wanaosema siyo, wana hoja ya msingi kwa kuwa Katiba haijaweka wazi mchakato unaohusu kiapo cha Rais Mteule. Katika maana ya kawaida tu, Rais Mteule ni mtu aliyechaguliwa kwa kura kuchukua ofisi ya Rais lakini hajawa Rais bado. Kwa hiyo mchakato unaomfanya awe Rais ni uchaguzi ambapo kwa bahati mbaya mchakato kama huo haupo kwa Makamu wa Rais anayechukua kiti cha Rais baada ya Rais aliyepo madarakani kufariki.
Hoja ya pili wanayoitumia wakosoaji wa mwongozo wa TLS inahusiana na uapaji wa Waziri Mkuu (Ibara ya 51-(1)) lakini pia Mawaziri na Naibu Mawaziri (Ibara ya 55-(1)- (2)). TLS wanashauri, Waziri Mkuu, Mawaziri na Naibu Mawaziri lazima waape kwa Rais aliyepo madarakani. Lakini wakosoaji wao wanasema urais ni taasisi na kwamba mawaziri hawa waliapa kwa taasisi na si kwa mtu. Ni hoja kuntu na yenye mantiki kabisa, hasa pale wanaposema Rais mpya atakapoingia madarakani atakutana na voingozi wa taasisi na mihimili mingine kama Jaji Mkuu, Mkuu wa Majeshi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nakadhalika, ambao wameapa kwa Rais aliyepita. Hatuwezi kusema na hao nao utumishi wao ukome kwa sababu hawajaapa mbele ya Rais mpya. Hata hivyo, bado nashawishika kuungana na TLS kuhimiza kuwa ushauri wao una mashiko, hasa kwa kuzingatia nadharia ya madaraka katika muktadha wa real politik.
Mwanya wa pili wa kikatiba upo katika Ibara ya 55-(1). Ibara hii inasema kuwa “Mawaziri wote ambao ni wajumbe wa Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa Ibra ya 54 watateuliwa na Rais baada ya kushuriana na Waziri Mkuu.” Sasa unajiuliza, nafasi ya Makamu wa Rais ipo wapi katika uteuzi huu? Kwa wale wanaosema tupitie ibara mbalimbali za Katiba ili kupata uelewa wa jumla, labda watatupeleka Ibara ya 47 ambayo inamtaja Makamu wa Rais kama msaidizi mkuu wa Rais. Je, tudhanie kuwa alishiriki katika uteuzi kwa kuwa anasaidiana na Rais? Kwa bahati mbaya ibara hii inamtambua Makamu wa Rais kama ‘msaidizi wa Rais’ na si mshauri. Lakini pia Ibara ya 37-(1) inasema Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote isipokuwa tu pale anapotakiwa kikatiba. Hii ina maana kuwa ni takwa la kikatiba Rais kushauriana na Waziri Mkuu wakati wa kuteua Mawaziri lakini halazimiki kusikiliza ushauri wa Makamu wa Rais kwa kuwa hajatamkwa kikatiba. Hivyo basi, kuna uwezekano Makamu wa Rais asiwe na mkono katika baraza la mawaziri.
Kwa nini baraza jipya la mawaziri?
Mbali na hoja za kisheria, kuna hoja za kisiasa zinazochochea uundwaji wa baraza jipya la mawaziri na Rais Samia Suluhu Hassan. Hii inatokana na ukweli kwamba kisiasa, lawama zote za muhula wa 2020- 2025 tutaziweka kwake na wala siyo kwa mtangulizi wake. Na kimsingi, tunamwita Mama Samia Rais wa awamu ya sita, na si Rais wa awamu ya tano. Hivyo basi, Mama Samia anapaswa kuwa na dira yake ya maendeleo na mamlaka kamili ya kumwezesha kutekeleza dira yake. Tunakiri kuwa alikuwa sehemu ya Dira ya Maendeleo ya 2020-2025 kwa kuwa alifanya kazi na Rais Magufuli, lakini halazimiki kurithi mbinu na mikakati ya kufikia malengo hayo kama yalivyowekwa katika ilani ya chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katiba inamtaja Rais kama Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Pamoja na ukuu huo, Rais amepewa mamlaka ya kutekeleza ajenda yake kwa nchi ikiwemo kuwa na dira ya maendeleo, na kwamba watumishi wa Serikali wote wanatekeleza majukumu yao kwa niaba ya Rais. Lakini kuna mamlaka mahususi zaidi ambayo Rais amepewa kikatiba. Kwa mfano, mbali na madaraka ya kutangaza vita au uwezo wa kutoa msamaha kwa wafungwa, kuna madaraka makubwa ya rais yanayotoa mwanga wa urathi, au legacy kama inavyojulikana kwa kimombo, wake wa baadae katika uongozi. Ukisoma Ibara ya 36(1), utaona kwamba Rais anapewa mamlaka ya kuanzisha au kufuta nafasi mbali mbali za kimadaraka kwenye utumishi wa umma, lakini pia ana mamlaka ya kuteua watu wa kushika madaraka ya uongozi. Watu hawa wanawajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, wakiwemo watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa serikali.
Moja ya maeneo muhimu yanayoguswa na ibara hii ni pamoja na Baraza la Mawaziri na nafasi zingine za uteuzi. Huenda TLS wamesita kusema katika mwongozo wao kuwa ili Rais afikie malengo yake vizuri lazima aunde taasisi na nafasi za madaraka zinazoendana na maono na dira yake na ateue watu wa kuzisimamia nafasi hizo. Hatutarajii Rais mpya atakuwa na maono na dira ile ile ya mtangulizi wake bila kupishana hata kidogo. Na hivyo basi Rais mpya anapaswa kupewa fursa ya kupangalia upya safu za uongozi kuendana na dira yake. Lakini pia, wasaidizi wanapoapa kwa Rais ina mantiki kubwa si tu kuonyesha utii, bali kutengeneza vinasaba vya utendaji kazi ili kufikia malengo husika. Tulikuwa tunashuhudia siku za nyuma kuwa, mara baada ya kuapishwa Rais alikuwa anaandaa semina elekezi kwa wasaidizi wake ili akawape miongozo ya utekelezaji wa majukumu yao. Huku kunaitwa kutengeneza chemistry ya kiutawala, na ni jambo linalompa Rais mpya fursa ya kujipambanua.
Mantiki ya kujipanga upya
Hayati Dk Magufuli (Mungu Amlaze Pema), aliamini katika watu wasomi na wenye weledi na akawateua katika nafasi mbalimbali za utawala katika nchi. Tutamkumbuka kwa hilo kama moja ya legacy yake, kujali weledi na si ujanja-ujanja katika siasa. Na kimsingi wamemsaidia sana katika kupangilia sera na kuzitekeleza. Ni hiari ya Mama Samia kuweka mwendelezo wa sera bila mabadiliko au kubadili kidogo ili kufanikisha malengo ya uongozi wake, lakini hatutegemei atakuwa na falsafa ile ile, kwani falsafa inaendana na haiba ya kiongozi husika.
Falsafa yake inaweza kumlazimisha Mama Samia abadili baadhi ya sera za ndani na nje lakini pia abadili baadhi ya sheria. Na kumteua mtu katika nafasi ya uongozi kuna maana juu ya falsafa na haiba kwa mamlaka ya uteuzi, kwa kuwa wateule hawa wanakuwa wawakilishi wake. Tuchukulie kwa mfano, mambo yanayohusu mahusiano ya kimataifa, falsafa ya kiutawala, sera za ndani za Rais mpya, msimamo, na mtazamo katika maisha zitaakisi sera zake za nje. Na hii pia ina mantiki katika mahusinao ya kimataifa. Kama mtangulizi wake alikuwa mhalisia zaidi katika mahusiano yake ya kimataifa na Rais mpya anadhani Serikali yake itanufaika zaidi ikiwa ya kiasi, au moderate, katika mahusiano yake, Mama Samia atahitaji kuwa na watu sahihi wa kutekeleza hilo. Hataweza kutuma wawakilishi hao hao ambao walikuwa na msimamo mkali huko nyuma, eti leo waende tena wakajadiliane na watu walewale kwa msimamo wa kiasi.
Na katika uwakilishi wa ndani, watumishi wanapaswa kufanya kazi kulingana na utashi wa Rais ambaye wanamwakilisha katika ngazi zote. Sasa kama falsafa ya kiutawala ya Rais mtangulizi haiendani na ile ya Rais mpya, Rais mpya atahitaji watu wapya wa kubeba falsafa hiyo. Kwa mfano, kama kiongozi analenga kuja na falsafa ya maridhiano, uongozi jumuishi, na kushirikisha wanajamii katika kuyafikia malengo ya maendeleo kama Mama Samia alivyodokeza punde baada ya kula kiapo, ni dhahiri kuwa atahitaji wasaidizi wanaoendana na falsafa hiyo. Lakini manguli wa stadi za maamuzi siku zote wanatuonya kuhusu kufanya mabadiliko makubwa katika utawala, na bila shaka mpaka kushika nafasi ya Rais, Rais mpya atakuwa mzoefu na anajua madhara haya bila kuhitaji mshauri mtaalam kutoka ughaibuni.
Urais ni nafasi ya kisiasa. Mtu yeyote anayekuwa Rais, hasa kwa kuchaguliwa, anakuwa ana kundi la wafuasi waliompigania kuingia madarakani. Wafuasi hawa wapo tayari kwenda naye inyeshe isinyeshe, liwake lisiwake. Tunaweza kusema Makamo wa Rais ni sehemu ya kundi hilo, na kwamba anaungwa mkono na ana shabihiana na wafuasi waliopigania tiketi ya urais kuanzia uchaguzi wa 2015 na katika uchaguzi wa 2020. Hata hivyo, kiuhalisia wachambuzi wa masuala ya kisiasa watakubaliana nami kuwa utii wa kisiasa siku zote upo kwa mtu mwenye mamlaka kamili, na katika muktadha huu ni kwa Rais. Na inapotokea Makamo wa Rais anaingia madarakani, na hasa kama ana lengo la kuendelea kuongoza baada ya kipindi cha kumalizia muhula kwisha, ni muhimu aandae timu yake. Hivyo basi, kuna mantiki ya kufanya uteuzi mpya wa wasaidizi wake kwa mujibu wa Ibara ya 36 ya Katiba.
Dkt Richard Mbunda ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na Mhadhiri katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni rmbunda@gmail.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupitia @richiembunda. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.