Waandishi tulikua tukimsumbua sana kwa kumpigia simu na kupanga naye miadi kwa lengo la kufanya mahojiano ili tuweze kupata uchambuzi wake wa hali ya kisiasa na matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea nchini Tanzania, Afrika na ulimwenguni kwa ujumla. Huyu si mwengine bali Dk Bashiru Ally Kakurwa, wakati huo akiwa ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma.
Binafsi, na naamini hali ni hiyo pia kwa waandishi wengine wa habari, nilipohitaji kupata uchambuzi yakinifu wa siasa kutoka kwa wanazuoni utakaoonekana haujaegemea upande wowote wa kisiasa, mara nyingi nilimtafuta Dk Bashiru Ally. Wengine, kwa upande wangu, waliopo kwenye orodha hii ni Profesa Bakari Mohammed na Profesa Issa Shivji.
Siyo uwongo kusema kwamba umaarufu wa Dk Bashiru ulikuwa mkubwa kwa waandishi wa habari za kisiasa na wasomaji wao. Mhariri huyo mwenza wa Miongozo Miwili: Kupaa na Kutunguliwa kwa Azimio la Arusha, kitabu kinachoelezea Azimilo la Arusha, Mwongozo wa TANU wa 1971, Mwongozo wa CCM wa 1981 na Maamuzi ya Zanzibar ya 1991 ambayo yalikuwa nyaraka za kisera za chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM), alikua makini sana alipoongea huku msikilizaji ukiwa hupati shida kuona itikadi za kijamaa ndani yake. Alikuwa akikosoa sana mifumo ya uendeshaji wa nchi katika nyanja za siasa, uchumi na elimu. Wengi wakati huo tulianza kuamini ni mfuasi wa upinzani. Akachochea zaidi hisia zetu baada ya kuhudhuria mkutano mmoja wa chama cha upinzania cha ACT-Wazalendo, chini ya kiongozi wake, Zitto Kabwe.
Mshangao, butwaa na bumbuwazi
Hayati John Magufuli, wakati huo akiwa Rais wa awamu ya tano na mwenyekiti wa CCM ndiye aliyetushangaza wengi na kutufanya tupigwe na butwaa ya kihistoria baada ya kuunda Kamati ya Kuhakiki Mali za CCM mwaka 2017 na kumteua Dk Bashiru Ally kuiongoza. Baada ya kamati hiyo kufanya kazi kwa kipindi cha miezi mitano, Dk Bashiru akateuliwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, hatua iliyowapiga bumbuwazi watu wengi kwani Dk Bashiru Ally hakuwahi kuonekana wazi wazi kuwa mwanachama hai wa CCM.
Hata hivyo, kama ilivyokuja kudhihirika baadaye, hatua hiyo ilikuwa na msukumo binasfi wa Rais Magufuli. Akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2018, hayati Magufuli alikiri namna alivyopata upinzani kumpendekeza Dk Bashiru kwa NEC ya CCM kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kikongwe barani Afrika. Kwa mujibu wa Magufuli, wana CCM walio wengi walikua hawamtaki Dk Bashiru wakisema ni mwanachama wa upinzani. Hata hivyo, Magufuli alisema, akalazimisha Bashiru kuteuliwa. Unaweza kusema, kwa hiyo, Rais Magufuli alimuingiza Dk Bashiru ndani ya CCM kwa lazima.
Kufuatia hatua ya kuwa Mtendaji Mkuu wa CCM, Dk Bashiru alilazimika kuacha baadhi ya misimamo dhidi ya Serikali na kuanza kutekeleza matakwa na maelekezo ya chama chake. Alituambia wanahabari pale Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, palipo na ofisi ndogo za CCM: “Kwa sasa bosi wangu ni NEC.”
Dk Bashiru pia alilazimika kwenda sambamba na kila misimamo ya mwenyekiti wa chama, Magufuli, huku ‘akiwanyoosha’ wana CCM ndani kwa ndani, ikiwemo kwa kupunguza ukubwa wa posho za baadhi ya vikao vya chama na kubana matumizi ili kukiongezea fedha chama. Hatua hizi bila shaka zilimtengenezea maadui Dk Bashiru ndani ya CCM. Kuunga kwake mkono baadhi ya maamuzi tata na sera za Serikali ya chama hicho na kauli kama ile ya CCM kutumia dola kubaki madarakani vyote vilichangia kumtengenezea Dk Bashiru maadui si haba nje ya chama hicho.
Bifu la Bashiru na Zitto, Membe
Moja kati ya wakosoaji wakubwa wa Dk Bashiru ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe ambaye Dk Bashiru zaidi ya mara moja amemualika kujiunga na CCM. Zitto, kwa upande wake, amekuwa akiugeuza mwaliko huo kwa kumtaka Dk Bashiru ajiunge na ACT-Wazalendo, akikiita chama hicho kuwa chama cha kijamaa halisi, badala kusaka vyeo CCM. Uhusiano kati ya Zitto na Dk Bashiru haukuishia kwenye kualikana tu, hata hivyo, bali mpaka kwenye kushambuliana.
Baada ya Dk Bashiru kuanza kumtuhumu Zitto kutumiwa na ‘mabeberu,’ na kufichua siri kuwa yeye na Zitto waliwahi kupanga kuanzisha chama kitakachoitoa CCM madarakani, Zitto naye akadai Bashiru aliyekutana naye UDSM mwaka 1999 siyo yule Katibu Mkuu wa CCM. Mvutano kama huu pia ulitokea kati ya Dk Bashiru na kada wa zamani wa CCM Bernard Membe baada ya wawili hao kuingia kwenye vita kali ya maneno kama inavyoonekana hapa na hapa. Mivutano hii na mingine ilimuibua Dk Bashiru na kuwafanya watu waone uimara na udhaifu wake kama mwanasiasa.
Ndani ya chama chake, Dk Bashiru alipachikwa jina la ‘Katibu Mkuu wa Swamu’ na baadhi ya wana CCM, akiaminika kuwa amewapelekea njaa kwa kuminya baadhi ya posho. Alitumia ripoti ya uhakiki wa mali za chama kudhibiti matumizi ya fedha, kitu ambacho hakuacha kujivunia katika maisha yake kama Katibu Mkuu wa CCM. Kwa mfano, Siku moja, gazeti la Serikali la HabariLeo lilimnukuu Dk Bashiru Machi 3, 2020 akajinasibu kuwa alipoingia madarakani aliikuta akaunti ya CCM ina shilingi bilioni tatu tu ila chini ya uongozi wake imefikisha shilingi bilioni 31. Kuna matawi ya CCM yalikua yakilipana posho mpaka shilingi laki tano kwa kikao, Bashiru alisema, ila yeye amefyeka mpaka imekua shilingi elfu 40 tu.
Bashiru akonga moyo wa Magufuli, lakini si wa Samia
Lakini wakati kauli na matendo yake yakimpatia marafiki na maadau ndani na nje ya chama chake, mtu mmoja ni wazi kwamba moyo wake ulikuwa ukisuuzika na uongozi wa Dk Bashiru. Huyu si mwengine bali Rais Magufuli, mtu pekee aliyehusika na kukua kwa Bashiru kisiasa. Kama ishara ya kuonesha imani yake kwa Dk Bashiru, punde tu baada ya kufariki kwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Magufuli alimteua Bashiru kuziba pengo hilo. Ingawa kikatiba haikua kosa, wadadisi wengi wa mambo walikosoa uamuzi huo wakiamini kwamba Dk Bashiru alipungukiwa sifa, hususan kutokana na ukweli kwamba hakuwahi kuwa mtumishi wa kiserikali na kwamba hajawahi kuwa msimamizi katika nafasi yoyote ya utumishi wa umma zaidi ya kufundisha wanafunzi UDSM na kuwa mtendaji mkuu CCM. Utata zaidi wa hatua hiyo ulitokana na ukweli kwamba baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, haikujulikana kama Dk Bashiru aliacha wazi nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM, kitu kilichopelekea baadhi ya wadadisi kuhoji endapo kama mtu huyo huyo anayeingia vikao vya usalama wa taifa (Katibu Mkuu Kiongozi) ndiye baadae hushiriki vikao vya chama (Katibu Mkuu) au la.
Ni katika muktadha huu ambapo uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Machi 31, 2021, kutengua uteuzi wa Bashiru Ally kama Katibu Mkuu Kiongozi na badala yake kumteua kuwa Mbunge wa kuteuliwa ulitangazwa na kupokelewa kwa hisia na maoni tofauti tofauti na Watanzania. Uamuzi huo ulikuja takribani siku 30 baaada ya kukaa Ikulu kama Katibu Mkuu Kiongozi na wiki mbili tu baada ya kifo cha mteuzi wake. Wakati baadhi ya Watanzania wametafsiri hatua hiyo kama kushushwa cheo kwa Dk Bashiru, wengi wanadhani msomi huyo wa siasa amepandishwa cheo.
Ipo minong’ono mingi kuhusu sababu za Rais Samia kutengua uteuzi wa Dk Bashiru kama Katibu Mkuu Kiongozi, lakini si lengo langu leo kuzungumzia minong’ono hiyo. Rais Samia mwenyewe hakutoa sababu yoyote ya kumuondosha Bashiru hapo na kumpeleka Bungeni na kuijaza nafasi yake kwa kumteua Balozi Hussein Katanga, aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Japan. Mimi pia nisingependa kulijadili hili kwa sasa mbali na kusema kwamba tumeona safari ya Dk Bashiru akitokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama mhadhiri na mchambuzi aliyekuwa akitegemewa na waandishi wa habari na wasomaji wao kwa chambuzi murua zisizoegemea upande wowote mpaka kufikia nafasi ya kuwa raia nambari nne wa Tanzania kwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na sasa kuwa Mbunge anayeenda kuisimamia na kuiwajibisha Serikali ambayo wiki nne tu zilizopita alikuwa akihusika na sera na mipango yake. Je, kwa mtazamo wako, unadhani huku ni kupanda na kushuka kwa Dk Bashiru na kipi unakitegemea kwa sasa kutoka kwake kama mtu aliye na wajibu wa kutunga sheria za nchi?
Charles William ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni charleswilly93@gmail.com au Twitter kupitia @2charlesWilliam. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unaweza kuchapisha kwenye safu hii kwa kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.
One Response
Kwa mtazamo wangu ameshuka, katibu mkuu kiongozi n raia namba nne kwenye utendaji wa serikali. Kutoka kuwasimamia makatibu wakuu wote wa wizara, mpaka mbunge wa kuteuliwa, kama angekuwa c mroho wa madaraka ilipaswa akae pembeni tu.