Leo, Mei 19, 2021, katika Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa, kwa kutumia kifungu cha 91 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kama ilivyofanyiwa Marekebisho mwaka 2019, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP) imesema haina nia ya kuendelea na shauri la uhujumu uchumi No.03/2020 lililokuwa linanikabili mimi na wenzangu 15. Hivyo basi, Mahakama imetuachia huru kwa sharti la kwamba kifungu hicho hakitawazuia Jamhuri kutukamata tena kama wataona inafaa.
Namshukuru Mungu kwa kunijalia roho ya uvumilivu na subira. Licha ya kukaa mahabusu kwa siku 33 mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 kumalizika, sikuwahi kujuta kufanya siasa na kuwa mgombea udiwani wa kata ya Berege kwa mwaka 2020 kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Niliamini haikuwa dhambi na sikuwa namkosea Mungu na sikumkosea binadamu yeyote kwa uamuzi wangu ule kwa sababu ilikuwa ni haki yangu ya Kikatiba kama raia wa Tanzania.
Kukamatwa, kupigwa, kukaa jela na mahabusu kumenipa funzo kuu na la maana sana katika maisha yangu. Nitakuwa mpumbavu sana kutomshukuru Mungu kuyaruhusu haya kwa sababu faida nilizozipata ni kubwa kuliko yasingetokea. Nimepata faida ambazo pengine jicho la nyama haliwezi kuona faida hizo.
Wakati napitia yote niliyopitia, hasa nikiwa jela, nilikuwa nayakumbuka maneno ya mwanafalsafa mmoja aliyewahi kusema, “Every struggle in your life has shaped you into the person you are today or you will be tomorrow. Be thankful for the hard times, they can only make you stronger. Make your own path and never give up; storms make people stronger and never last forever. No matter what happens to you, never, never lose hope and never forgets the power of intentions and desires. Stay strong.” Kwa tafsiri yangu ya Kiswahili ni kwamba, “Kila changamoto uliyopitia maishani imekujenga kuwa hivyo ulivyo sasa na utakavyokuwa badae. Kuwa mwenye shukrani kwa kila nyakati ngumu unazopitia, zinaweza kukufanya uwe imara zaidi. Fanya njia yako mwenyewe na usife moyo kamwe; dhoruba huwafanya watu kuwa na nguvu na haidumu milele. Haijalishi kinachotokea kwako, usipoteze tumaini kamwe na kamwe usisahau nguvu ya nia na matamanio. Kuwa thabiti.”
Usiogope
Nilikuwa nikiacha kuisikia sauti yenye ujumbe wa maneno hayo wakati ule nikiwa Gereza la Mpwapwa na Gereza Kuu Isanga; nilikuwa muda mwingi nasoma Biblia kutafuta faraja ya moyo na akili yangu. Na ndiyo kwa mara ya kwanza nikagundua neno “USIOGOPE” limeandikwa mara 366 katika Biblia Takatifu. Nikapata wasaa kutafakari kwanini kitabu hiki kitakatifu kimeliandika neno hili “USIOGOPE” mara nyingi hivi? Nikauambia moyo wangu, “Usiogope kwa yatakayokupata. Kesho yetu ni njema sana na haya tunayopitia yanakuandaa kwa ajili ya kesho yetu njema na nzuri.”
Niliamini kama nitakuwa sina kosa kwa niliyokuwa nayapitia basi, “Fimbo ya udhalimu haijawahi kukaa juu ya fungu la wenye haki. Na wenye haki wasije inyoosha mikono yao kwenye upotovu.” (Zaburi 125:3). Niliyafurahia mateso niliyokuwa nayo na niliyopitia kwa ajili ya wana Berege. Hayakuwa mateso kiuhalisia bali lilikuwa ni funzo la kunikomaza mimi, wenzangu na jamii yetu. Tumekuwa bora sana kuliko huko nyuma. Na tumekomaa haswaa katika kuipigania jamii yetu ya Berege na kutoa mchango wetu katika taifa letu.
Kwa kiwango cha pekee niwashukuru washitakiwa wenzangu 15 katika kesi hii, kwani toka kukamatwa kwetu na mpaka kufikia leo hii tumekuwa wamoja na hata siku moja hakuna aliyeonesha hofu na kukata tamaa. Sina cha kuwalipa na mtabaki kuwa ndugu muhimu sana katika maisha yangu. Shida, matatizo na changamoto humsaidia binadamu kuwajua ni akina nani haswa ni ndugu zake, rafiki zake, na pengine husaidia kuwafahamu hata wasiokutakia mema wanakuwazia nini na wanasema nini kipindi ambacho zipo dalili za anguko lako kwa mujibu wa macho yao. Namshukuru sana Mungu kwa funzo hili.
Nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassani kwani kauli yake kuhusu kesi zisizo na maana naamini imekuwa ni matokeo ya DPP kusema hana nia ya kuendelea na kesi iliyokuwa inatukabili mimi na wenzangu 15. Tukutakie kila la kheri katika kulirudisha taifa letu kwenye misingi ya HAKI, UHURU NA DEMOKRASIA YA KWELI. Tunaamini ukimaliza kwenye haya uliyoanza nayo, hutaweza kutuacha bila Mchakato wa Katiba Mpya katika Taifa letu.
Takwa la Katiba Mpya
Namuomba Mama Samia, Rais wetu, ashughulike na mifumo. Licha ya kwamba matamshi yake yanatia moyo na faraja, tunaomba aende mbali zaidi kwa kuhakikisha taifa letu linapata Katiba Mpya na tunafanya mabadiliko ya sheria kandamizi na zinazowaonea na kuminya haki za raia. Taifa letu lilifikia mahali pabaya sana. Sisi wengine tulichobakiza kwako na tunachotamani kukiona ni hili la kubadili mifumo mibovu ambayo ni matokeo ya sheria za ajabu.
Nawashukuru ndugu, jamaa na marafiki zangu kwa maombi, michango na kujitolea kwenu kwa hali na mali. Mungu awabariki sana. Nawashukuru mawakili wetu mliosimama nasisi toka mwanzo mpaka mwisho, akiwemo Wakili Msomi Jebra Kambole, Wakili Josephat Mbeba, Wakili Fred Kalonga na wengine. Mungu awabariki sana wasomi.
Ninawashukuru sana wana Berege kwa kura nyingi mlizonipigia, nawashukuru kwa upendo wenu na kuniunga mkono katika hatua zote. Berege ina sehemu na chumba nyeti sana katika moyo wangu. Siku zote ninaamini ili pengine nije kuwa mtu wa maana katika uso wa dunia ya leo, ni kuja kuyatumia maarifa niliyonayo au nitayojaaliwa kwa manufaa ya jamii yangu niliyotokea ambayo hasahasa ni Kata ya Berege kwa kuanzia.
Ujumbe wangu unabaki kuwa: Mapambano ya kuipigania haki, yamekuwa sehemu ya maisha yangu. Niliyaishi, ninayaishi na nitaendelea kuyaishi. Na hapo ndipo amani ya moyo wangu ilipojificha. Safari ya haki ndio kwanza imeanza. Aluta Continua, Victoria Ascerta.
Deogratias Cosmas Mahinyila ni mwanasheria na mwanafunzi wa uwakili katika Shule ya Sheria ya Tanzania. Mnamo Oktoba 2020, Mahinyila aligombea udiwani kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Kata ya Berege, wilayani Mpwampwa, mkoani Dodoma. Yeye na wezake 15 walikamatwa na kupewa kesi ya uhujumu uchumi iliyowafanya wakae mahubusu kwa siku 33 mpaka DPP alipoamua leo, Mei 19, 2021, kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi yake.