The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Simulizi ya Kijana wa Mjini Aliyetaka Kupata Utajiri wa Haraka Kupitia Kilimo

Kwangu mimi, msemo kwamba ‘Mkitaka mali mtazipata shambani’ haukuweza kufanya kazi. Badala ya kupata mali, mimi nilipata ajali.

subscribe to our newsletter!

Miaka kadhaa iliyopita nikiwa nasoma Chuo Kikuu, ilikuwepo hamasa kubwa kwa vijana kuwekeza katika kilimo, hasa vijana wasomi ambao wanamaliza vyuo na kujikuta hawana ajira kutokana na changamoto ya ajira iliyopo hapa nchini kwetu, Tanzania.

Ohooo, tulihamasishwa sana kufanya kilimo, hasa kilimo cha tikiti maji na kutokana na hamasa zile wengi wetu tulijiona tunachelewa kwani wahamasishaji walikuwa wanatupigia mahesabu ya kuwekeza laki tatu huku ukipata faida ya Shilingi milioni 10 baada ya mavuno. 

Mimi, akili yangu ilitamani sana kufanya kilimo, lakini nilisema wakati haujafika, ukifika nitalima ili nijionee na kuneemeka na neema hizo za kuwekeza laki tatu na kupata Shilingi milioni 10. Ndoto hizi zilikua kila kukicha nikitamani kufanya kilimo, lakini changamoto za hapa na pale hazikuniruhusu kufanya hivyo hadi ilipofika mwaka 2019.

Katika malengo niliyokuwa nayo kwa mwaka huo wa 2019 nikishirikiana na mke wangu ilikuwa ni kulima heka 10 za maharage, na tuliweka nia hiyo kutazama faida tunayoambiwa kila siku kuwa ipo katika kilimo. Mnamo Oktoba 2019 maandalizi ya kwenda shamba yalianza, kijana mimi Jovine nikaamua kuliacha jiji la Dar es Salaam na kwenda kijiji cha Mabedini, huko Wilaya ya Manyoni, Singida kwenda kulima maharage.

Safarini Manyoni

Safari ilianza kutokea Dodoma Mjini, ambapo niliongozana na kijana mwenzangu mmoja kwenda huko kijijini tukiwa na baadhi ya mizigo ikiwemo chakula, sufuria za kupikia pamoja na nguo za shamba. Mke wangu alijitahidi kunifungia kila kinachowezekana kwani alijua safari hii haiwezi kuwa fupi na nyepesi. Tukiwa Mjini Manyoni tuliweza kununua baadhi ya vitu vya mahitaji ya kawaida.

Tukiwa Monyoni pia tulikwenda katika duka la vifaa na changamoto ilianzaa hapo tukiwa tunanunua mapanga. Muuzaji akiwa na shauku ya kujua tunakwenda wapi na hayo mapanga, tulimwambia sisi ni vijana wa mjini tunakwenda shambani kulima. Kiukweli alitushangaa kabisa kuona ujasiri huu tumeupata wapi. “Kilimo hakitabiriki ndugu zangu, changamoto ni nyingi, mvua zinaweza kukesekana, jua na wadudu wakashambulia, mmejipanga kweli?” alituuliza muuza mapanga kwa mshangao. “Sitaki kuwakatisha tamaa ila ningekuwa mimi ningewashauri mrudi tu mjini msiharibu nguvu zenu.”

Kiukweli maneno haya yaliniingia moyoni kwani nilikuwa na shauku kubwa ya kulima, hivyo sikutamani kuyasikia maneno kama haya. Safari ya kwenda kijijini ilianza ambapo tuliwapata waendesha pikipiki, maarufu kama bodaboda, wawili wa kutupeleka huko. Tukiwa tunaanza safari, bodaboda aliyekuwa amenibeba mimi akaniuliza: “Bro, safari hii mna mwenyeji huko? Maana naona mizigo ni mingi?” Nikamjibu tunaye. Akanuliza tena: “Kijijini mnakwenda kufanya nini?” Nikamwambia tunakwenda kulima. Aliguna kidogo kabla ya kuniambia: “Bro, kilimo sio kabisa. Kina mambo yake mengi. Ila acha mkajaribu mjionee wenyewe.”

Kiukweli safari hii ilikuwa yenye machungu na masononeko mengi maana kila aliyejaribu kujua tunakwenda wapi hakuwa na maneno mazuri kwetu. Tulijitahidi hivyo hivyo na mchana wa saa saba hivi tukawa tunaingia kijijini pale. Mvua ya kwanza ilitupokea siku hiyo ambapo ilinyesha kwa takribani saa moja hivi. Basi tulijiona kama matajiri maana tulihisi uhakika wa mvua upo na hivyo juhudi zetu tu zingetufanya tupate kilichotupeleka.

Shamba na maandalizi yake.

Mwezi mmoja na wiki tatu zilitosha kuandaa hilo shamba, japo nguvu nyingi zilitumika katika maandalizi yenyewe. Mhhhh, sijawahi fanya kazi ngumu kama hii. Niliona siku hazitembei kabisa. Kila siku kukata miti isiyoisha. Mara kukusanya mara kuchoma, mara hiki mara kile, lakini hatimaye shamba lilikuwa tayari kwa ajili ya kulimwa.

Wakati haya yote yanafanyika, mvua zilinyesha angalau kwa wiki mara moja, na sisi tukaendelea kujawa na imani kuwa mambo yatakuwa mazuri kabisa. Nguvu na pesa zilitumika na mnamo Januari 15, 2020, tulifanikiwa kupanda maharage kwa heka saba tulizofanikiwa kuziandaa. Ilikuwa ahueni kubwa kwangu mimi binafsi, maana niliziona Shilingi milioni 13 zile pale. Nikaamua kurudi mjini ili niendelee kutatufa pesa kwa ajili ya shughuli zilizobaki ikiwa ni pamoja na palizi mbili, kuvuna na kusafirisha.  

Tuliendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa shamba lile, lakini, ooooh hadi nahisi kulia, kile kilichokuwa kinaendelea shambani kilikuwa hakielezeki. Shamba liliota vizuri. Maharage yakachanua vizuri. Ila jua lilipotokea hata hatukufahamu. Mvua iliacha kunyesha ghafla kiasi ya kwamba ilipita wiki mbili hakuna tone hata moja la mvua. Mimi nikawa nakesha na maombi lakini hali haikubadilika. Kijana mwangalizi wa shamba akawa ananitia moyo kwamba maharage yatakaa vizuri ikifika palizi ya kwanza. Basi, nikatuma pesa. Palizi ikafanyika lakini baada ya palilizi hiyo maharage ndiyo yaliendelea kukauka haswa.

Ilikuwa ngumu kuamini kile kilichokuwa kinatokea. Pale nilipoamua kwenda kutembelea shamba lilikuwa halina kitu kabisa. Maharage yalikuwemo lakini yalikuwa machache sana. Kwa sura yalionekana kama watoto wanaoomba msaada na wasijue wapi pa kusaidiwa.

Kutoka milioni 13 mpaka laki moja.

Mahesabu yangu niliyokuwa nayo ni kuwa nastahili kuvuna gunia 98 kutoka kwenye heka saba na nikifanikiwa kuuza nasitahili kupata zaidi ya Shilingi milioni 13. Huu msukumo wa kupata kiasi hicho ndio ulinifanya kila hatua niliyoipitia iwe ya kufedhehesha au kufurahisha. Niliendelea mbele bila kuchoka. 

Tuliendelea na maandilizi yote ya kuvuna kilichopo shambani. Ilikuwa ngumu kukubalina na hali ya shamba ilivyo kwani maharage hayakuwa mengi, yaliyomengi yalikuwa yamekauka na jua, lakini pia isingekuwa busara kuondoka bila kuvuna hicho kilichomo. Tulipiga moyo konde, tukafunga turubai shambani na kuweka kambi ya siku saba ili kuvuna. Tulikuwa tunalala chini. Mbuu ndio waliokuwa wakituzungumzisha usiku kucha. Tulisikia sauti za wanyama wakali wa kila aina. Kama siyo tamaa za kupata utajiri wa haraka tusingelala hapa hata siku moja.

Kazi ilikuwa ngumu maana tuliamua kuvuna wenyewe. Ugumu ulikuwa mkubwa hasa unapofanya kuvuna huku ukijua unachokivuna hakitakuwa na msaada kama ilivyokuwa matarajio ya awali. Ajabu ni kwamba mvua iliyokosekana kipindi chote cha ukuaji wa maharage ilikuwa haikati tulipoanza kuvuma. Ilikuwa ikinyesha kila siku. Kijana mwenzagu akasema ni lazima kutakuwa na mkono wa mtu, si bure. Mimi siamini mambo hayo kabisa.

Basi tuliendelea kuvuna huku tukijipa matumaini ya kuwa hata kama tukikosa ila gunia nane zingepatika. Tulianza kwa nguvu zote ila tulichokipata hata mimi sielewi mpaka sasa. Tulivuna na kuyapiga maharage na kufanikiwa kupata gunia moja na nusu tu. Twaweza kusema kuwa tulifanikiwa kupata mbegu tulizoweka maana tulitumia kilo 100 za maharage. Ilikuwa ngumu mnoo kuamini na kukubaliana na hali halisi. Ilikuwa ni maumivu ambayo sijawahi kupata kwenye maisha yangu yote. Nikawa nawaza: nakwenda kumwambia nini mke wangu aliyenitegemea kuwa nitarudi na burungutu la pesa?

Nilipiga moyo konde na kubeba hayo maharage na kuyapelekeka soko kuu la Wilaya ya Manyoni kwa ajili ya kuuza. Huko nako ilikuwa ngumu maana nilitegemea walau naweza kuuza kilo moja kwa Shilingi 1,800 lakini mnunuzi akanunua kwa Shilingi 1,400 kwa kilo, huku akinisindikiza kwa maneno mengi ya kuwa maharage yenyewe punje zake ni ndogo hazikupata maji ya kutosha. Katika kuuza na kutoa matumizi yote na mkopo niliokuwa nao wa Shilingi 100,000, nilirudi nyumbani na Shilingi 90,000 tu. 

Sijawahi pata maumivu kama yale. Sijawahi kujuta kama kule. Ilikuwa ngumu, ngumu mno kuamini kilichotokea. Ilikuwa ngumu kuamini kama kilichotokea ni ndoto au uhalisia. Uwekezaji uliotugharimu zaidi ya Shilingi milioni tatu, na nguvu zetu juu, lakini nikajitukata narudi nyumbani na Shilingi 90,000 tu? Sitokuja kujisamehe. Ndoto za kupata Shilingi milioni 13 na zaidi, zilizima kama mshumaa uliozimwa na upepo mkali. 

Elimu juu ya bima ya mazao

Waswahili husema majuto ni mjukuu huja mwisho wa safari. Baada ya haya yote kutokea, nilijiuliza maswali mengi sana. Kwa mfano, kwa nini niliamua kuweka nguvu na pesa zangu katika kilimo? Je, wakulima wote wanapitia changamoto kama hizi nilizozipitia? Je, kilimo ni kigumu hivi kama nilivyokiona au ni bahati mbaya tu? Na je, ni kitu gani kinawapa nguvu na msukumo watu wengine wa kuendelea kulima licha ya ugumu huu uliopo?

Sikuwa na majibu yoyote maana nilikuwa kama naota kwa haya yaliyonipata. Lakini katika pekua pekua yangu baada ya changamoto hizi ndio nikakutana na suala la Bima ya Mazao. Kwa mujibu wa Mwongozo wa Bima ya Mazao uliotolewa na Wizara ya Kilimo zipo aina tatu za bima ambazo ni Bima Mseto, Bima za Hali ya Hewa pamoja na Bima za Maeneo Maalum. Kwa changamoto niliyoipata kumbe Bima Mseto ingenisaidia baada ya majanga haya niliyoyapata kama ningefahamu na kupata taarifa mapema.

Wakulima wengi wanapitia changamoto za kukosa kile wanachokitegemea kukipata kwenye kilimo kutokana na majanga tofauti yanayotokea, lakini hawafahamu kama upo usaidizi unauweza kupatikana kutoka kwenye bima. Wakulima hawapaswi kukaa na kulia kama watoto yatima, wanapaswa kusaidiwa, wanapaswa kuelimishwa juu ya bima na uwepo wake.

Jovine Johansen ni mchambuzi wa masuala ya data kutoka kampuni ya Cornerstone Solutions Limited. Kwa maoni unaweza kumpata kupitia jovin.johansen@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.   

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 responses

  1. Pole Jovine na mwenzako. Lakini usikate tamaa. Ungejaribu tena na tena na labda kuna miaka ambayo ungefanikiwa. Pia unaweza kufanya biashara ya uchuuzi wa mazao ya kilimo badala ya wewe kulima mwenyewe. Hongereni kwa kujaribu. Na hongera kwa makala nzuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts